YUSUFU AMEFANANA NA YESU.
- Mch. Gasper Madumla
- Oct 3, 2018
- 3 min read
Updated: Sep 30, 2022

Kwa ufupi.
Sikuwahi kuitambua siri hii kubwa kwa miaka mingi iliyopita. Kwa maana nalifikiri Musa ndiye hasa aliyefanana sana na Yesu kwa maana Musa alitumwa kuwakomboa Israeli utumwani Misri na Yesu naye alikuja kutukomboa pia,Ni kweli kwa namna fulani Musa amefanana na Yesu kwa kazi ya ukombozi,Lakini kumbe kuna mtu mwingine tena anayeitwa Yusufu,naye amefanana na Yesu kitabia.
Ukweli ni kwamba simulizi zote katika biblia zinamwelezea Yesu,hata simulizi ya Yusufu mtoto wa Yakobo inamwelezea Yesu,Lakini tujifunze namna ambavyo Yusufu anavyofanana na Yesu.Yusufu mtoto wa Yakobo ni kana kwamba amevaa kivuli cha Yesu.Ufanano wake upo katika “ mtindo wa maisha yake kwa ujumla” . Ebu angalia mfanano huu;
• Yusufu alipendwa na babae,Yesu naye ni mwana wa pekee aliyependwa na Mungu.( Mwanzo 37:3 na Mathayo 3:17,Yoh.3:16)
Ingawa Yakobo alikuwa na watoto wengi,lakini Yusufu ndiye aliyependwa sana,sio kwa sababu ni mtoto wake wa mwisho maana ingelikuwa hivyo basi Benyamini ndiye angelipendwa kuliko wengine kwa maana Benyamini ndio wa mwisho. Biblia inatuambia sababu moja wapo ya Yusufu kupendwa na babae kwa maana alikuwa ni mwana wa uzee wake,lakini pia mbali na hilo Yusufu alikuwa na neema na kwa sababu hiyo,Yusufu hakufanya maovu kama ndugu zake ( Mwanzo 37:5)
• Yusufu ni mchungaji wa kondoo,Yesu naye ndiye mchungaji mwema. ( Mwanzo 37:2 na Zab.23 yote). Utofauti ni kwamba Yusufu alichunga kondoo kama kondoo, Yesu anatuchunga sisi ambao tu kondoo wake,Yeye huitwa mchungaji mwema.
• Yusufu aliwafunulia ndugu zake,Yeye ni nani hasa ;Yesu naye anena wazi wazi Yeye ni nani. ( Mwanzo 37:5-11 linganisha na Luka 18:31-34,Yoh.11:49-51)
Yusufu alipoota ndoto zake,aliwaambia ndugu zake. Zile ndoto zilikuwa zinamtambulisha kuwa Yusufu ni nani hasa. Ijapokuwa ndugu zake ndio waliotafsiri zile ndoto,lakini kusema ukweli walikuwa hawajui wasemalo ni kama vile Mungu aliwatumia tu kutamsfiri kwa usahihi walakini hakujua nini wanasema. Pia mwangalie Yesu, Kwenye Yoh.11:49-51,utamkuta kuhani mkuu mmoja aliyeitwa Kayafa,aliyetabiri kifo cha Yesu pasipo hata kujua anasema nini. Pia ukisoma andiko la Luka 18:31 Yesu anawafunulia juu ya kifo na kufufuka
kwake,lakini wanafunzi wala hawakujua nini Yesu anasema.
• Yusufu aliuzwa na Yuda,Yesu naye aliuzwa na Yuda. ( Mwanzo 37:26-28 linganisha na Mathayo 26:14-16,47-50)
Yuda aliyemwuza Yusufu, alimwuuza kwa vipande 20 vya fedha na yule Yuda aliyemwuza Yesu alimwuuza kwa vipande 30 vya fedha. Hawa wakina Yuda hatari sana,dah! Wapo kimaslahi zaidi. Hata leo makanisani wapo,kaa nao makini!!!
• Watu walimkusudia mabaya Yusufu,lakini Mungu alimkusudia mema,alionewa. Yesu naye alikusudiwa mabaya,lakini Mungu alimkusudia mema,alionewa ( Mwanzo 50:20,40:15 linganisha na Isaya 53:3-5 )
• Yusufu alikuwa na Mungu,Yesu naye ni vivyo hivyo.(Mwanzo 37:23 linganisha na Yoh.14:9)
• Yusufu hakulalamika katika mambo yote aliyoonewa,Yesu naye hakulalamika ingawa alionewa.
Nilipomwangalia kwa ukaribu Yusufu tangia mwanzo wa kufanyiwa vitimvi na ndugu zake kwenye ile sura ya 37 Mwanzo. Sikuona akilalamika kwamba anaonewa,nikajaribu kusoma nikishuka chini. Nilichokuwa nikitafuta mahali palipoandikwa kwamba alinungunika,hata alipokuwa kwa Potifa na kusingiziwa kesi ya ubakaji,lakini Yusufu hakulalamika wala kujitetea-tetea.
Alipotupwa gerezani,bado Yusufu alikaa kimya na kumwachia Bwana apigane nao wanaopigana naye tena hata aliposimama kwa Farao bado hatuoni malalamiko yoyote ya Yusufu, kumbuka kwamba ;Yote alionewa tu!!! Yesu naye ni zaidi ya hivyo,akishitakiwa kwa uongo na ushahidi wa kutengenezwa lakini Yesu alikaa kimya zaidi neno lake aliwaambia “ wewe wasema” .Sasa mpendwa nikuulize,mbona leo tumekuwa watu wa kulia lia tunapoonewa? Mbona tumekuwa watu wa kujitetea sana pale tunaposingiziwa au kuzushiwa jambo? Je ni kweli tunafanana na Yesu? Jihoji wewe mwenyewe upoje katika eneo hili.
• Yusufu alikataa ofa ya kulala na mke wa Potifa kwenye mazingira tulivu kabisaa,naye akashinda jaribu,Yesu naye akashida yote ulimwenguni,pamoja na kila jaribu. ( Mwanzo 39:6-12 na Yoh.16:33)
• Kumbuka;
Yusufu aliyashinda hayo,kwa kuwa Mungu alikuwa pamoja naye. Yusufu amekuwa kielelezo cha vijana na watu wote kwamba inawezeka kuepuka uovu,zinaa na mengineyo. Hata leo bado inawezekana,ukiwa na Mungu hakuna lolote litakalokushinda. Yesu yu hai,ndiye awezeshaye yote hayo maana Yeye ni Mungu kamili,ukiwa naye utayashinda yote. Moja kati ya jambo muhimu ni kwamba unatakiwa“ ufanane na Yesu katika yote uyafanyayo“
Ikiwa fundisho hili limekubariki,basi ningependa kusikia kutoka kwako kwa kuniandikia msg au kunipigia kwa namba zangu zilizopo hapo juu.
Pia kwa msaada zaidi pamoja na maombezi,waweza kunipigia sasa.
Kwa mawasiliano piga kwa +255 683 877 900
Na mch. Gasper Madumla.
What’s app ni +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments