WEWE U NANI?/ WHO ARE YOU?
- Mch. Gasper Madumla
- Mar 26, 2019
- 4 min read
Updated: Sep 30, 2022

Wewe u nani? Ni swali jepesi kweli lakini ni swali gumu sana kwa maana kile unachoweza kujibu kwa haraka kinaweza kikawa si sahihi. Kama utafanikiwa kuongea na watu watatu tu na kuwauliza swali hili kwa kila mmoja akwambie yeye ni nani hasa? Basi hapo tegemea kupata majibu mengi kuliko utakavyodhania;Kwa sababu majibu utakayoyapata ya kwanza yatatofautiana na majibu ya pili ikiwa kama utawauliza tena swali hilo hilo,hii ni kuonesha kuwa wengi hatujitambui sisi ni akina nani? Yohana mbatizaji naye aliulizwa “ wewe u nani? ” naye akafaulu kujibu vyema. Swali aliloulizwa Yohana lilikuwa linataka aeleze yeye ni nani kwa kile alichokuwa anakifanya.
“Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani? Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La.” Yoh. 1:19-21
Najaribu kufikiria mazingira ya kihuduma ya Yohana mbatizaji aliyokuwa nayo,nashindwa kupata picha halisi. Lakini bila shaka hayakuwa mazingira mepesi kama ya siku za leo. Kwa sababu Yohana alikuwa mtu wa polini mwenye kuitengeneza njia ya Bwana. Makuhani na Walawi walitumwa kutoka Yerusalemu kumfikiria Yohana mbatizaji kwa sababu Yerusalemu ilisiikia kazi aliyoifanya Yohana mbatizaji, na wakachanganyikiwa,wengine wakadhani ni Yesu,wengine ni Eliya n.k . Wajumbe hawa walipomfikia Yohana mbatizaji hawakusita kumwuuliza “ wewe u nani? “
Yohana mbatizaji akakubali kabisa kwamba yeye sio Kristo. Ukumbuke hapo Yohana mbatizaji amevuma kipindi hicho,lakini Yohana mbatizaji hakuona maana kujiita yeye ni Kristo kwa maana ni kweli siye Kristo. Wakamwuuliza tena “wewe u Eliya?“naye akawaambia mimi siye Eliya,hata alipoulizwa “wewe u nabii yule?”alikataa pia hilo na Kisha akajitambulisha yeye ni nani hasa.
Kwa sababu ya jina lake lilisikika,ilikuwa ni rahisi kujikuta akijitambulisha “yaa! Mimi ni Kristo bhana! Au Aah siyo Kristo lakini ni Eliya. Au angelisema mimi siye Kristo wala Eliya lakini mimi ni nabii ” kama angelewa lewa na ulevi wa cheo kama wengine wanavyolewa na vyeo.
Usiendeshwe na cheo ulichonacho.
Moja ya tabia ya mtumishi wa Mungu aliyemnyenyekevu ni kuendeshwa na Roho wa Mungu na sio vyeo. Watu waione kazi na sio cheo chako kwa maana kule kujiita majina makubwa makubwa kuna maana gani. Mwenye majina hayo ukimwuuliza wewe u nani? Utasikia “mimi ni mashine ya Yesu,mzee wa Yesu,katapila la Yesu,Nabii wa Bwana mwenye upako wa kufungua n.k” Sasa Hayo majina si wewe? Wewe u nani? Yohana mbatizaji alikuwa na Roho mtakatifu,lakini baba wa watu alijitambulisha vile tu alivyo. Sipati picha kama mtumishi wa Mungu wa kizazi hiki halafu akutane na watu waliotumwa na dini nyingine wamwuulize “wewe u nani? Je ni nabii “ kisha utaona majibu yake hapo.
Cheo hakina maana yoyote kama kuifanya kazi ile ya Bwana. Mtu hata kama asikuite kwa cheo,hawezi kualibu kile alichokiweka Bwana ndani yako. Watumishi wa leo hupenda kueshimiwa wakiitwa kwa majina makubwa makubwa! Hapo ndipo husikia raha na heshima,lakini hali hiyo haikuwa kwa Yohana mbatizaji wala haikuwa kwa Yesu.
Sisi ambao tumepewa neema kidogo ya kuchunga,au wale waliopewa neema ya utumishi pale wanapoulizwa wajitambulishe,wewe u nani. Wengi utawasikia “ mhh,mimi ni nabii wa afrika mashariki na kati pamoja na ukanda wote wa maziwa makuu,ni Dr.(dokta) mtume,na mchungaji…”
Khaaa! 😁😁😁😁 . Kwani ukisema tu mimi ni fulani… Si inatosha kabisa!!!
Lakini hii yote ni kutaka kuwaambia watu wewe u nani ujenge heshima lakini ukweli ni kwamba utakuwa hujajibu swali,wewe u nani hasa.? Leo imefika wakati hata watenda kazi nyumbani mwa Bwana hawataki kuitwa wao ni watenda kazi. Wakiulizwa “wewe u nani” utasikia “mimi ni mtumishi wa Mungu aliye juu sana kisha ndipo anataja jina lake“. Kwani ukisema “mimi ni John myendakazi wa Bwana.. ” si inatosha kabisa!
Au mwimbaji tu wa kanisani utasikia “mimi ni mwimbaji wa kimataifa,Bwana amenipa jina la upako naitwa fulani ” Khaa! Ndio nini mtu kujiita mwimbaji wa kimataifa halafu hata morogoro hawakujui,tena hata hujawahi kuimba,nini kuimba hata kupajua hupajui!!!! Halafu,oooh mimi ni mwimbaji wa kimataifa! Kwa nini usiseme tu mimi ni fulani… Basi yatosha hilo jina lako.
“Wewe u nani? “ kujibu swali hili,haliitaji kuwa na madoido,wewe jibu tu kwa ufupi. Kama ni mwalimu sema mimi ni mwl. Gasper wa shule ya chekechea… Na kila mtu atakuelewa vyema kisha kile kilichopo ndani kitapewa nafasi nzuri. Kumbuka ya kwamba karama iliyopo ndani yako haitaji cheo cha nje,wala kubustiwa kwa aina yoyote bali kama kuinuka itainuka tu kwa wakati wa Bwana.
Kuwa wewe halisi.
Lengo kubwa la ujumbe huu ni kukutaka wewe uwe wewe, na si wewe uwe yule. Mara nyingi tumejikuta tukishindwa kujitambua sisi ni kina nani kwa sababu ya kuishi maisha ya watu wengine. Kwa kuwa tunajitahidi kukwepa uhalisia wetu,tumejikuta tukipata taabu sana kukopi na kupesti maisha ya watu wengine. Ebu fikiria mtu anayeweza kujitambulisha katika nafasi fulani isiyo yake,jinsi atakavyokuwa akihangaika ili awe kama mwenye nafsi hiyo.
Fikiria kwa Yohana mbatizaji kama angelijitambulisha kuwa yeye ni Kristo, kitu gani kingefuata? Je wale wajumbe wa Yerusalemu wangepelekaje habari huko Yerusalemu? Au je Kristo mwenyewe angemwonaje? Mimi sijui bhana ingekuwaje!!!!
Hakuna mateso mabaya ayapatayo mtu yule anayejaribu kuishi maisha ya mtu mwingine. Nenda kamwuulize mtu wa namna hii,kisha atakwambia anavyoangaika ili afanane na mtu mwingine. Umewahi kuona mtu ameulizwa wewe u nani? Alafu akajinyanyua kwa kujipachika cheo. Halafu halaiki ya watu wanamcheki tu! Wakitarajia kuyaona yale aliyojitambulisha. Sasa kitakachofuata ni kuanza kuigiza angalau afanane na kile alichojitambulisha,sasa si shughuli hiyo nakwambia!!!! Patamu hapo🏃🏃🏃🏃🏃
Umeona sasa! Shida yote ya nini hiyo? Si angesema tu mimi ni fulani yatosha! Tambua wewe huwezi kuwa kama mimi,na mimi siwezi kuwa wewe. Kila mmoja ni wa utofauti,na kwa sababu hiyo kubali kuwa wewe hasa. Ondoa namna ya kupenda vyeo,kwa maana vitakusumbua tu. Mimi hata mtu akiniita jina la Gasper tu,akaondoa cheo,ni sawa kabisa na maisha yatasonga mbele vyema kabisa. Sipo kwa cheo bali kwa ajili ya kusudi la Mungu tu. Umeelewa ujumbe huu?
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe.
Kwa msaada zaidi na MAOMBI piga ;+255 683 877 900
Whatsapp namba+255 746 446 446 .
Na Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comments