Mafundisho ya biblia
“ Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo. ” Wakolosai 2:11
“Tohara” ilikuwa ni jambo muhimu sana kwa watu wote waliotokea Yuda,au Wayahudi. Katika agano la kale wale wasiotahiriwa walihesabika kama wamataifa,yaani watu wasiokuwa na Mungu halisi,au waabudu miungu. Na kwa sababu hiyo,ilikuwa ni mwiko kwa wanawake wa Kiyahudi kuolewa na wanaume wasiotahiriwa ( Mwanzo 34:13-14).
Hivyo kwa tohara ya Wayahudi iliwatenga na mataifa mengine katika suala zima la kuoa na kuolewa. Lakini haikuwa katika kuoa na kuolewa tu,bali hata katika wokovu kwamba asiyetahiriwa hawezi kuokoka.Hali hii iliendelea hata katika baadhi ya watumishi katika agano jipya- ( Matendo 15:1).
Hivyo “tohara” katika agano la kale ilimaanisha mambo mawili;
1. Kuingia katika agano na Mungu – Mwanzo 17:11
2. Kutengwa na uchafu
Katika agano jipya,tohara si ya wanaume peke yao bali ni ya kila aaminiye katika Kristo Yesu. Katika agano jipya kila aliyeokoka,ameingia katika agano jipya na Mungu kwa njia ya kumwamini Kristo. Na anapaswa ajiepushe na uovu kwa gharama yoyote ikibidi hata kufa na afe akiikwepa dhambi. Biblia inasema “uwe mwaminifu hata kufa ” Ufunuo 2:10
Hivyo,“Tohara ya Kristo” ni “Kuuvua utu wa kale” Neno kuuvua utu wa kale lina maanisha kuuvua mwili wa nyama au kuacha tabia za mwilini ulizokuwa nazo kabla ya kuamini (Wagalatia 5:19 – 20). Kitendo cha kukataa kurudi nyuma kule ulikokuwa zamani kabla ya kumpokea Kristo,kuvua utu wa kale. Lakini ni vyema ujue ya kwamba “utu wa kale” ni tabia zote za shetani,hivyo una uwezo wa kuziacha moja hadi nyingine.
Ni mchakato wa kila siku wa kujifunza Neno la Mungu,kudumu katika fundisho ( Matendo 2 :42)
na kujitahidi sana kuliishi neno,ndio dawa kamili ya kuuvua utu wa kale. Na hiyo ndio tohara ya Kristo. Hivyo,mchakato huu ni wa maumivu makubwa ya kukubali kutoa muda wako kwa Bwana,kujitahidi kufanya mazoezi ya kiroho kama vile kufunga na kuomba,kutoa sadaka kwa uaminifu wote,tena kukubali kuwaacha watu fulani katika maisha yako,na hatimaye
kuambatana na watu wa Mungu. Maumivu na usumbufu ni lazima kwa sababu ni “tohara” kwa maana kama ilivyo tohara ya mikono inavyouma,ndivyo tohara ya Kristo pia ina maumivu yake na usumbufu wake,utakaokuhitaji uwe na uvumilivu ili utu wa kale,uchafu wa dhambi zote viweze kukutoka.
Kumbuka lengo la “tohara ya Kristo” ni wewe umpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, upate kuwa hai. ( Kumb.30:6)
Kwa msaada zaidi,na maombezi + 255 683 877 900
What’s app + 255 746 446 446
Na Mch.G. Madumla.
UBARIKIWE.
Like