top of page

YOTE YAWEZEKANA KWAKE AAMINIYE.


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi;

Moja ya mkazo mkubwa sana wa mafundisho ya Yesu ni juu ya “imani”. Hali ya kutokuamini haikuanzia leo bali tangu kipindi cha kale hata kabla ya Yesu. Hii inaonesha kuwa tatizo la kutokuwa na imani ni tatizo sugu kweli kweli,na ndio maana mambo mengi yamekuwa yakikwama!!!. Nilipochunguza suala hili,nikagundua kwamba watu wanayo imani kwa Bwana lakini wamekosa kuwa na “hakika” ya kinachotarajiwa. Kwa maana watu wanaamini kuwa Mungu yupo,au Kristo ni Bwana lakini wamekosa hakika ya uwepo wake Bwana. Na kwa sababu hiyo,imani ya watu hao inakuwa ni imani haba,(Imani haba ni ile iliyokosa hakika,imani yenye mashaka). Lakini Yesu alipoona wanafunzi wake wamekosa imani,hata mara nyingi akiwaambia “Enyi wenye imani haba...”. Kwa maana alioona imani waliyokuwa nayo wanafunzi wake.

Kitu ambacho kilikuwa hakitegemewi kuonekana ni kukosekana kwa imani timilifu ndani ya wanafunzi wake,kwa sababu walikuwa na Bwana wakati wote. Ni afadhali kuona watu wengine wamekosa imani dhabiti,kwa maana si wanafunzi wa Kristo. Lakini kitendo cha kuikosa imani nzuri kwa wanafunzi ni jambo la kushangaza!!! Hii inatuonesha maisha halisi ya wakristo/wanafunzi wa Kristo wa leo,namna walivyokosa imani thabiti ingawa wapo pamoja na Kristo. Ninaipenda habari ile ya kijana aliyekuwa na pepo bubu,alipoletwa kwa wanafunzi wa Kristo,ili aombewe na pepo limwondoke (Mathayo 17:14-21,Marko 9:14-29)

Katika Marko 9:14-20,Yesu anasema neno zito sana kwa babaye yule kijana mwenye pepo bubu,na anasema“ Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.” Marko 9:23. Ukisoma vizuri habari yote,utagundua kwamba wanafunzi wa Yesu walikuwa na imani lakini ilikuwa ni imani haba, (walikuwa na imani lakini waliona shaka )nao wakashindwa kumtoa pepo. Kumbe! Imani haba haina matokeo mazuri!!!! Lakini pia baba wa yule kijana naye hakuwa na imani,maana kama angelikuwa nayo basi ni dhahili yeye mwenyewe angeliweza kumwombea kijana wake na pepo lingetoka. (Kwa maana suala halikuwa ni lazima ifanywe na wanafunzi au Yesu,bali suala lilikuwa ni imani kwake Yesu Kristo)

Neno hili “Yote yawezekana kwake aaminiye.”,lina maana kwamba “hakuna gumu lolote litakalomshinda yule anayemwamini Kristo,kwa sababu Kristo Yesu alikwisha yashinda magumu yote” Sasa,…Ukisoma tena kwa ukaribu hapo (Marko 9:14-29) utagundua kwamba,hata Yesu alipomwombea yule kijana mwenye pepo,lakini pepo halikumtoka sekunde ile ile,bali pepo likamtupa yule kijana kwenye kifafa sana,hata watu wakasema kwamba kijana amekwisha kufa!!! Maana yake nini? Hii ina maana;

  1. shetani ni mwongo sana,kiasi kwamba alikuwa akimtazamisha Yesu/Mwombaji kwamba kazi yake ni bure,na hana uwezo wa kushughulika naye. Na ndivyo ilivyo hata sasa,pale unapoliombea jambo fulani gumu,shetani hutumia nafasi kuinuka kwa lengo la kukutazamisha vibaya ili kusudi uache kuliombea!!! Hizo ni hila tu,wewe kaza kuomba kama alivyofanya yesu.

  2. “Watu walisema kijana amekufa” maneno ya watu ni kikwazo kikubwa mno cha kuondoa katika imani. Kijana hakuwa amekufa,lakini watu wakapanda roho ya mauti kwa kijana ili kusudi yule anayeombea aungane noa na kuamini kwamba ameua. Kumbuka;katika kila hali ngumu,kuna sauti za watu kinyume na muujiza wako!,bali wewe usisikilize sauti hizo – Mtazame Yesu,hakujali maneno yao,bali alipishana nayo,na kisha akamwinua yule kijana yu mzima!

  3. Imani huja kwa kusikia Neno la Mungu (Hii ni sawa na kusema,kama unahitaji imani iokoayo,huna budi kukaa kwenye neno la Kristo.Imani haiombwi ili ijaye ndani ya mtu,bali kwa neno la Kristo kisha kujaribiwa katika mengi)

Je unaamini hata katika hilo,bado yupo Mungu? Je unaweza kuvuka sasa? “Ndio” hilo ndio jibu,kwa maana hakuna jambo gumu kama utamwamini Bwana leo,kisha ukaomba kwa bidii. Tunaona mifano mingi ya watumishi wa Mungu waliomwamini Bwana Mungu,na hakuna kilichoshindikana kwao.Mtazame mtu kama Danieli na rafiki zake (Daniel 3 na 6 yote,Paulo -Matendo 28:1-6,n.k)

Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe. Na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900

Whatsapp namba .+255 746 446 446

Mch. G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page