top of page

MVINYO KWA ALIYEOKOKA ?

Updated: Aug 29, 2022



Je ni sahihi kwa mtu aliyeokoka kutumia vinywaji ambavyo ni jamii ya kileo/ pombe?


Bwana Yesu asifiwe…


Kwa ufupi,


Neno “ vinywaji jamii ya kileo ” ni aina ya vinywaji vyote vyenye asilimia fulani ya kileo. Wataalamu wanasema hata vile vinywaji vyenye asilimia 0.0 ya kilevi vina uchache wa kilevi kwa maana namba 0 nayo ni namba. Lakini kuna vilevi/pombe za aina mbali mbali za viwandani pamoja na zile za kienyeji,bila kusahau mbege kwa maana wengine wakila mbege ulewa . 


Kila mmoja wetu amekuwa na mtazamo binafsi kuhusu pombe hasa kwa mtu aliyeokoka. Katika utafiti wangu mdogo nilioufanya kuhusu usahihi wa kutumia vinywaji jamii ya pombe,nimegundua kwamba kuna mpasuko wa kimtazamo kuhusu kileo.

Na kwa sababu hiyo hadi wanazuoni wegawanyika katika kambi mbili. Kambi ya kwanza inaona hakuna shida ya kutumia kileo nao hudai biblia hajakataza popote isipokuwa “ kulewa” ndio Neno limekataza. 


Lakini Kambi ya pili ya kupinga/kambi ya upinzani ya walio wengi husema si sahihi tena haifai kutumia kileo kwa maana ni dhambi.

Kwa mujibu wa mdahalo wa vijana wa Tar.19/6/2022 uliofanyika katika kanisa la Beroya bible fellowship church lilopo Kimara Baruti, mada hiyo ya “matumizi ya mvinyo aliyeokoka “ haikufikia muwafaka kwa maana kulikuwa na pande mbili zilizokuwa zikivutana hata hivyo,


Ilionekana kwa upande fulani si vibaya matumizi ya mvinyo “kama dawa “ kwa mtu aliyeokoka lakini sio sahihi matumizi ya mvinyo kwa matumizi ya starehe

Usahihi wa matumizi ya mvinyo kama dawa.

Ni pale kilevi kinapotumika katika matibabu. Mfano ukisoma katika ( 1 Timotheo 5:23 ) utaona Paulo alimshauri Timotheo atumie mvinyo kidogo kama dawa ya tumbo na magonjwa yampatayo mara kwa mara .


Na kupitia andiko hili ilionekana hata leo kuna baadhi ya dawa zina mchanganyiko wa kileo tunazozitumia mara kwa mara, nyingine ni kwa ajili ya kupunguza maumivu. Lakini baada ya kutumia unahisi kama umelewa hivi? ( Dawa ya vidonda ya spirit nayo inasadikiwa ina mchanganyiko wa kileo)


Lakini tunaona pia mara nyingine mvinyo ukitumika kama dawa ya kufungia majeraha ya mtu aliyeumia ( Luka 10:34). Pamoja na hoja hizo za kitabibu lakini Je sasa ni sawa kutumia mvinyo? Biblia inasema nini kuhusu matumizi ya mvinyo?


  • Lakini ni vyema kabla ya kuangalia biblia ni vyema utafakari jambo hili “ Je ni sahihi kutumia kinywaji chochote ambacho kinaleta matokeo mabaya kwa haraka?


Ni kweli vinywaji vyote vinavyotengenezwa viwandani kwa kemikali kama soda, juice nk vina matokeo mabaya kwa mtumiaji lakini vivywaji vyenye vilevi vina matokeo mabaya zaidi yanayotokea kwa haraka. Mfano mtu akinywa kileo,atalewa kutegemea na uwezo wake lakini pia aweza kupoteza kumbukumbu au kuvurugwa ndani ya muda mfupi tu baada ya kutumia.

Hii inaonesha wazi kabisa kwamba pombe ni hatari kwa afya!!! Sasa kama ni hatari kwa afya swali linakuja “ je ni sahihi kuhatarisha afya yako?” bila shaka mpaka hapo kabla hujaiangalia biblia jibu ni kwamba si sahihi!!! Hivyo kupata usahihi wa pombe hutegemea kwanza matokeo ya pombe.


Biblia inasemaje?


Mithali 31:4-5 (KJV)  “ Ee Lemueli, kunywa mvinyo hakuwafai wafalme, hakuwafai wafalme; Wala haifai wakuu waseme, Ki wapi kileo?Wasije wakanywa na kuisahau sheria, Na kuipotosha hukumu ya mtu aliye taabuni.”


Neno “ wafalme” hapo kama lilivyotumika linamaanisha watu wenye mamlaka na uwezo,ni watawala. Katika agano jipya, wafalme au ukuhani wa kifalme ni watu wa Mungu waliopokea Neema ya wokovu ( 1 Petro 2:9). Wewe ukiwa ndani ya Kristo ni kuhani wa kifalme. Hivyo,ni sawa na kusema “kunywa mvinyo hakuwafai waliookoka (wafalme), …


Na anakataza hivyo ili kusudi hawa watu wa uzao wa kifalme / watu wa Mungu wasije wakatumia kileo na kuisahau sheria ( sheria ni Neno la Mungu) . Wasije wakanywa wakasahau Neno la Mungu. Bwana Mungu alikuwa anajua madhara ya pombe au kilevi kwamba kinaathiri mfumo wa akili,Sasa anakataza kabisa ili watu wake wasiathirike hata wakasahau,au wakaliacha


Neno lake ambalo ni sheria. Hivyo si sahihi kutumia mvinyo au kileo hata kama katika kiwango cha chini. Pamoja na hayo, biblia hajanyamaza kuhusu kileo,mara nyingi inatoa maonyo makali mfano ni katika – Habakuki 2:15

Ukisoma katika (  Luka 1:15) unaona vile Bwana akimpa maelekezo muhimu kuhani Zekaria kupitia malaika Gabriel kwamba mtoto wake atakayezaliwa ambaye ni Yohana mbatizaji kwamba “hatakunywa divai wala kileo” yaani


Neno hilo linaonesha katazo la moja kwa moja kwamba hakuna kileo kabisa kwa mtu wa Mungu ( kwa kipindi kile alikuwa Yohana mbatizaji) ambaye amebeba kusudi maalumu katika mwili wa Kristo.

Mungu angeliweza kusema anywe kidogo, lakini anajua uadui wa pombe kama mlango wa ibilisi hivyo anatamka wazi wazi “kukataza hata kuonja tu” kwa maana pombe ingeliweza kumvuruga Yohana mbatizaji.


Kama katazo hilo limetolewa kwa Elizabeth asitumie kileo kwa maana aliyembeba ni mtakatifu wa Bwana,na huyo mtakatifu asitumie kileo basi hapo Pana maana sana juu ya maisha yetu kama watu wenye kusudi.


Ikiwa kama umebarikiwa nifahamishe na kwa msaada zaidi; piga +255 683 877 900.


What’s app number ni + 255 746 446 446.


Na Mch. Gasper Madumla.


UBARIKIWE.

Comentarios


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page