BABA WA IMANI, IBRAHIMU
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 8, 2022
- 3 min read
Updated: Aug 30, 2022

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Mungu alimchagua Ibrahimu ili awe nguzo ya imani/ baba wa imani kwa watu wote. Hii yote ni kuonesha tu Mungu huchagua kujali hali yake ya maisha kikubwa huangalia sana moyo.
Tena uwainua wanyonge waliokataliwa na kuonekana hawafai,mtu kama Ibrahimu alikuwa ni mtu wa kawaida katika familia ya kawaida tu, lakini Bwana ndiye aliyemkusudia. Kama Bwana alifanya Kwa Ibrahimu basi ni dhahiri aweza kufanya na kwako . Ebu fikiria namna ambavyo Ibrahimu amekuwa nguzo ya imani kiasi kwamba Ukoo wa Yesu unaanzia kwa Ibrahimu ( Mathayo 1:1).
Pamoja na kwamba baba yake Ibrahimu alikuwa ni muabudu sanamu ( Yoshua 24:2) Lakini bado Mungu alimtwaa Ibrahimu katika nyumba ya waabudu sanamu,huo ulikuwa ni mpango wa Mungu. Kumbe mpango wa Mungu hauwezi kuzuiliwa na chochote kile,ndio maana Ayubu anasema “ makusudi Yako hayawezi kuzuilika” Ayubu 42:2b
Hivyo Mungu hakuzuiliwa na mwenendo mbaya wa mzee Tera/babaye Ibrahimu wa kuabudu miungu. Ndiposa nayakumbuka maisha yangu binafsi vile babangu mzee Madumla alivyokuwa mnywaji wa pombe lakini Mungu akanitwaa Mimi na kunipa uchungaji, Mpango wake Mungu hakuzuiliwa na tabia ya mzee wangu.
“Utii wa Ibrahimu ” pale Bwana aliposema naye,lilikuwa jambo la kwanza na muhimu la kumsogeza katika baraka za Mungu hata akawa baba wa Imani kati ya mababa wengi. Inaonesha wazi ya kuwa Ibrahimu aliitambua sauti ya Bwana mapema angali alikuwa akiishi katikati ya waabudu sanamu. Kama ni hivyo,basi alikuwa ni mtu mwenye moyo wa kipekee katika nyumba ya baba yake mzee Tera. Hivyo hakuwa na mashaka kuhusu wito huo.
Kupitia hilo tu,tunaweza kujifunza kwamba unaweza ukaishi katikati ya waovu lakini wewe usiwe mwovu. Lakini pia, inawezekana kabisa kuisikia sauti/wito wa Mungu juu ya maisha yako pamoja huku ukiwa katika nyumba ya waovu. Tena, Mungu anaita mtu sio watu! Kwa maana alimwita Ibrahimu yeye kama yeye,naye akatii.
Ebu fikiria kama Ibrahimu aliposikia sauti ya Bwana ya kutoka katika nchi ya baba yake,kama angelikataa!Hivi angelikuwa baba wa Imani? Au fikiria kama Ibrahimu angelienda kumuuliza / kuomba ushauri Kwa babaye mzee Tera hali ingekuwaje? Nini unajifinza katika hilo?
Mambo machache ya kujifunza kutoka Kwa baba wa Imani, Ibrahimu
01. Alimwamini Mungu,na kumwona kama baba asiyeshindwa.
Namna ya kuamua kuacha yote Kwa ajili ya Mungu si jambo jepesi hata kidogo. Lakini Ibrahimu alimwamini sana Mungu nakumwona Mungu ni BABA asiyeshindwa na chochote. Unajua kama unaye baba wa kimwili tu na akikwambia njoo utoke ulipo na uende mahali atakapokueleza.
Ni dhahiri kama utamwamini basi utatoka bila mashaka na tena utakwenda na hatimaye utafanikiwa. Lakini uhakika wa kujua sauti ya baba Yako ni muhimu sana Kwa maana kama hutaielewa,itakuwa ngumu sana kwenda atakapo baba Yako.
02. Utii
utii ulimsogeza Ibrahimu katika nafasi yake. Wengi Leo wapo nje ya nafasi zao Kwa sababu ya kukosa utii tu. Tukumbuke, Mungu ni yule yule,aliyesema na Ibrahimu ndiye anayesema nawe hata leo lakini tofauti iliyopo hapo ni kiwango cha utii kitaamua namna gani utaendelea katika nafasi.
Kumbuka;
“utii ndio ngazi ya ukubwa na kuinuliwa” Kwa maana Ibrahimu hakufanya maajabu hata kuwa alivyo,Bali utii ndio ilikuwa maajabu yake. Hata leo,endapo kama utaitii sauti ya Bwana Kwa bidii,lazima utainuliwa na kuwa mtu Fulani wa Imani kama alivyokuwa Ibrahimu. Na tunapozungumzia kuhusu utii hatuna maana ya utii wa mambo makubwa saana kukuzidi ufahamu wako,Bali ni utii wa mambo madogo madogo ambayo Bwana amekuwa akisema nawe njia tofauti tofauti labda Kwa kinywa tu cha mchungaji wako!
03. Kujenga madhabahu
Ilikuwa ni tabia ya kiroho ya Ibrahimu ya kumjengea Bwana madhabahu Kila alipokanyaga. Tabia hiyo ilimjengea Ibrahimu nguvu ya kiroho wakati wote. Ebu cheki alipoingia Kanaani,kitu cha kwanza akamjengea Bwana madhabahu ( Mwanzo 12:8). Biblia Inasema akiwa huko njaa kubwa ikaingia,Sasa nguvu ya madhabahu aliyoijenga ikamwinua Ibrahimu na hatimaye akashuka Misri.
unajua Ibrahimu kushukia Misri haikuwa jambo la kibinadamu Bali lilikuwa na maelekezo ya kiungu ambayo Ibrahimu aliyasikia kutoka ndani. Naye akafanikiwa kuikimbia chaa kuu ya kwanza. JIFUNZE,hapo kumjengea Bwana madhabahu popote uendapo.
Unajengaje?
Kumbuka;
Madhabahu ya kwanza ilikuwa ikijengwa Kwa mikono ya lakini ya Sasa ni jambo la kiroho la kujiungamanisha na Bwana pale uingiapo au pale ulipo Kwa kuchagua chumba au eneo utakalofikia,Kisha kukifanya chumba hicho ni chumba au eneo la wewe kukutana na Bwana Kwa ibada.
Mfano; unasafiri kikazi / kifamilia na kuingia mji wa watu/mwingine basi hapo uingiapo basi tafuta mahali pa faragha na uwe unafanya ibada siku Kwa siku mpaka unatoka hilo eneo na Kwa kufanya hivyo utakuwa umemjengea Bwana madhabahu.
Ikiwa umebarikiwa nifahamishe Kwa +255 683 877 900
What’s app number + 255 746 446 446
Na Mch. G. Madumla
Comments