DAWA YA MOYO MBOVU
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 12, 2022
- 3 min read
Updated: Aug 30, 2022

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Tafsiri ya haraka ya moyo mbovu ni moyo wa kutokuamini au ni moyo uliokosa Imani
“ Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai.” Waebrania 3:12
Neno “moyo mbovu” linatafsiriwa kama moyo uliokengeuka katika Imani. Au ni moyo mbaya ambao dhamiri yake imekufa ndani yake. a sinful heart. Mtu mwenye moyo mbovu ni yule ambaye utu/Nia yake ya ndani imekufa, Kwa hiyo kuiba,kuzini,kudanganya n.k kwake sio ishu.
Hivyo aweza kufanya dhambi au ubaya fulani na akaona ni sawa atendavyo bila hata kuhukumiwa moyoni. Mfano,akaua,au kuzini Kisha akaona hakuna ubaya kabisa katika hayo aliyoyafanya. Mtu mwenye moyo mbovu ni yule aliyefikia katika hatua ya “ ukengeufu” ( hatua ya juu ya kupoa kiimani)
Kumbuka;
“Ukengeufu ” ni hatua ya juu ya kuwa na moyo mbovu kwa kujiondoa katika imani ya kweli kwa makusudi hasa hasa kwa wale waliokwisha onja kipawa cha wokovu yaani wakaokoka na baadae wakaamua kwenda njia zao binafsi. Watu wa namna hiyo Wana moyo usio na toba! Lakini pia ukengeufu ni hatua ya kufa kiroho
Biblia imejawa mifano mingi ya watu waliokuwa na moyo mbovu wa kumwacha Bwana Kwa haraka hata wengine wakakengeuka. Ebu tazama mkutano wa wana wa Israeli kipindi kile walipokuwa wanamsubiri Musa aliyekwenda mlimani kuzungumza na Bwana.
Biblia inasema,watu walipoona Musa anachelewa kurejea chini basi walimkusanyikia Haruni wakidai kutaka kupewa Mungu mwingine atakaye kwenda mbele yao maana hawajui kama Musa Yuko hai au lah! ( Ukisoma habari hii katika Kutoka 32:1-2) utagundua hawa watu walikuwa na moyo mbovu sana wa kutokuamini,walikengeuka!
Ebu fikiria hapo,kumbe kuna watu ambao wanapoona wanayemtegemea au wanachotegemea kuja kimechelewa ni wepesi kurudi nyuma na kujitafutia njia zao mbadala Kwa kuamini imani yao ya Mungu na kuweka katika vitu! Kwa kufanya hivyo,watu wa namna hiyo hawana tofauti na watu wenye moyo mbovu kama lusanyiko la Israeli kwa kipindi hicho.
Lakini biblia katika andiko hilo hapo juu(Waebrania 3:12),
linatutahadharisha kwamba tuwe makini,tuangalie asije mmoja wetu akawa na moyo mbovu,hii Ina maana kwamba Kila mmoja katika mwili wa Kristo anapaswa kuwa mwalimu na mlinzi wa mwenzake,kwa kuhakikisha pasiwepo na mtu mwenye moyo mbovu! Kwa tafadhali hii,tunauona upendo wa Mungu kwa watu wote,kwa maana hataki hata mmoja wetu apotee Bali kila mmoja aifikirie toba
Dalili za kuwa na mbovu/ mbaya
Zipo dalili nyingi tu zinazo mtambulisha mtu mwenye moyo mbovu. Dalili hizi ni hatua au vyanzo vinavyopelekea moyo mbovu. Nimechua dalili 3 tu,Kwa ufupi nazo ni kama ifuatavyo;
01.Kuchukia Neno
Hii ndio dalili ya kwanza na kubwa ya watu wenye moyo mbovu. Hali kuchukia Neno linapelekea hata kuchukia maonyo, maelekezo ya kawaida kabisa. Na Kwa sababu mtu akilichukia Neno la Mungu ni dhahiri kabisa hawezi kuwa na imani sahihi Kwa maana chanzo cha Imani ni kusikia,na kusikia huja kwa “neno la Kristo ”
Kwa siku za leo,wapendwa wengi hawapendi fundisho bali kuombewa au miujiza. Sasa sio mbaya kuombewa maana ni jambo muhimu sana kwa kila mtu,hata miujiza hakuna asiyetaka,hata Mimi naitaka sana. Lakini ukumbuke,Neno ndio chanzo hayo yote. Ukiona hupendi kabisa kujifunza Neno ujue upo katika hatari ya kutembea katika moyo mbovu wa kutokuamini.
02. Kiburi na hali ya kutaka kuabudiwa.
Kuna watu wanaipinga kweli Kwa uovu. Wakijua ya kwamba kuwa na kiburi ni machukizo kwa Bwana lakini hawaachi tabia hiyo. Lakini si hivyo tu,Bali imefika wakati kuna watu ambao hupenda kuabudiwa kiasi kwamba watu waje wainame na kupiga magoti mbele zao!!! Watu wa namna hii ni lazima wawe na mioyo mibovu au lah! Basi watakuwa wanaelekea kuwa na mioyo hiyo mibovu ( Soma Kwa utulivu Warumi 1:18-25)
03. Kujiona uko sawa wakati wote
Ikiwa wakati wote unajiona wewe upo sahihi na sawa katika Kila kitu kuliko hata wengine ujue una tatizo la moyo mbovu,una shida mahali fulani ingawa bado hujaijua!!! Kwa maana hakuna ajuae kila kitu,na hakuna mtu ambaye yupo sawa wakati wote. Kila mmoja tunafahamu au kujua kwa sehemu na tunakosea Kwa sehemu Kwa maana huo ndio ukuaji wetu. Kwa bahati mbaya wengine leo hujifanya hakuna kitu wasichokijua na kwa sababu hiyo hawezi kujifunza kitu kwa wengine tena hawawezi kumwamini mtu yeyote hii ni dalili na hatua ya moyo mbovu!!!
Dawa kuu ya kushughulikia moyo mbovu wa namna hii ni;
01. Toba na kubatizwa katika Roho mtakatifu kwa upya.
Toba ndio mlango pekee wa kurejea kwa Bwana. Lakini katika kutubu hakuna maana ya kuungama Kwa maneno tu Bali kufanya maamuzi ya dhati ya kumgeukia Bwana Mungu kwa kuamua kuacha njia mbovu za dhambi.
Lakini hiyo pekee haitoshi unahitaji kubatizwa upya katika Roho mtakatifu yaani kujazwa tena ili kusudi moyo wako ufurikishwe na nguvu za Mungu na hapo hakutawa na nafasi ya ukengeufu! Katika kubatizwa katika Roho mtakatifu ni suala la ibada za ujazo kupitia mchungaji aliyejazwa,
Roho mtakatifu atakapoiona kiu yako hutajazwa tu.
Ikiwa umebarikiwa nifahamishe kwa +255 683 877 900
What’s app number ni + 255 746 446 446
Na Mch. G. Madumla
Bình luận