YEYE NI MUNGU WA MUDA.
- Mch. Gasper Madumla
- May 1, 2019
- 3 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
“Mwendee Farao asubuhi; tazama, atoka kwenda majini; nawe simama karibu na ufuo wa mto ili upate kuonana naye; na ile fimbo iliyogeuzwa kuwa nyoka utaichukua mkononi mwako. Nawe umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, amenituma nije kwako, kusema, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia jangwani; nawe, tazama! Hujasikia hata sasa.BWANA asema, Katika jambo hili utanijua ya kuwa mimi ndimi BWANA; tazama, nitayapiga haya maji yaliyo mtoni kwa fimbo hii niliyo nayo mkononi mwangu, nayo yatageuzwa kuwa damu.“ Kutoka 7:15-17
Biblia inasema Bwana amemtuma Musa amwendee Farao “kwenye muda wa asubuhi” na hapo Musa ataweza kuonana na Farao,kwa maana kuna kitu Bwana anataka kufanya kwenye “muda wa asubuhi “ wala sio mchana au wala sio usiku. Bwana alijua muda wa mchana na wa usiku lakini haikuwa makusudi yake ya kudhihilisha nguvu zake,isipokuwa alikuwa amechagua muda wa asubuhi tu,ndipo sasa akamwagiza Musa ahakikishe anamwendea Farao “asubuhi “. Sasa ebu jiulize hivi;
laiti Musa asingelienda kwenye muda huo wa asubuhi ulioamriwa,unafikiri nini kingetokea? Je ule upako/ nguvu iliyoachiliwa tayari kwa ajili ya asubuhi, Musa angelikutana nayo kama angeliamua kwenda mchana? Au je Musa angelimwendea Farao mchana, angelimwona?
Utagundua kwamba Mungu alikuwa akiheshimu sana “muda” hata miujiza yake aliifungamanisha na muda. Kwa maana hata sasa muda wa kukutanika,ibada muhimu sana.Musa alipomfikia Farao katika muda uliokusudiwa na hapo ndipo tunaziona ishara,ajabu na miujiza mikubwa ikitendeka kwa mkono wa Musa. Jaribu kufikiria kama Musa angelipuuzia muda aliopewa
Hali ya leo ikoje?
Watu wengi wamepishana na uwepo wa Mungu haswa wawapo ibadani kwa sababu ya kutokujali muda uliopangwa. Kwa mfano; kiongozi wa ibada ametangaza kuwa “ ibada itaanza saa tatu kamili asubuhi “ Kisha watu wote wakasema “ameeen“. Sasa,kwa sababu Bwana wetu anaheshimu sana muda, basi ujue saa tatu atashuka hapo kwa ajili ya kuhudumia watu wake waliokubaliana kukutana saa tatu. Lakini lahaulaa!!! Hiyo saa tatu kamili asubuhi, ndio kwanza kila mmoja anajiandaa nyumbani mwake,mwingine utakuta muda huo huo ndio anakunywa chai nyumbani mwake!!!
Kwa hiyo kila mmoja atafika kwa muda wake,na mbaya zaidi hadi kiongozi aliyetangaza kuhusu ibada utakuta akiingia kwa kuchelewa sana. Sasa hapo kile kilichopangwa na Bwana kiachiliwe sawa sawa na makubaliano yenu wenyewe,kinazuiliwa kabisa! Na hatimaye kusanyiko linakosa uwepo wa Mungu,kumbe tatizo sio Bwana Mungu bali ni ninyi kwa kutokuzingatia Muda.
Ebu fikiria inauma kiasi gani pale unapowekeana ahadi na mtu,ahadi ya kuonana saa fulani halafu unajitahidi kweli kuwahi katika muda ule ule na huku ukiwa umebeba zawadi yake mtu huyo. Lakini baada ya kufika,unagundua huyo mtu hajafika,kwa hiyo wewe uliyezingatia muda itakupasa umsubiri labda kachelewa na foleni za leo…. Unasubiri weee,nusu saa inapita…..lisaa linapita….hatimaye masaa mawili… Hivi katika hali ya kawaida utafanyeje hapo ? Kama si kuondoka tu!!! Sasa unaamua kuondoka na zawadi yake mtu huyo ambaye ni mswahili katika kuzingatia muda na ndivyo tufanyavyo mbele za Bwana.
Jifunze hapo kwa Musa,Bwana anampa muda maalumu anaotakiwa Musa kumwendea Farao ili Bwana apate kushuka ndani ya muda huo huo,naye Musa akafanya vivyo hivyo sawa sawa na alivyoagizwa.
Leo kuna shida sana ya namna ya kuzingatia muda wa kuonana na Bwana kwa visingizio vingi visivyo na maana yoyote ile. Watu wengi wanachelewa ibadani,katika muda ambao Bwana Mungu amewakusudia kuwaponya,wao huja baadae kinyume na utaratibu.Mambo mengi yangelitokea kwako,ikiwa kama ungeliweza kuzingatia muda hasa wakati tu wa ibada. Lakini cha ajabu kwa waamini wa leo! Ni kwamba;
Watu wapo tayari kuamka usiku wa saa tisa,na kuanza safari ya kwenda kazini. Kwa kusudi waweze kuwahi na wamfurahishe boss,lakini watu hao hao,ndio wachelewaji wa kutupa! Kwenye mambo ya ibada,ambapo ibada inaanza saa tatu asubuhi,lakini bado hawawezi kuwahi na ndio hao hao wa kwanza kuondokaga katikati ya ibada!!!
Hawaumii wanapochelewa ibadani mahali ambapo walipokuwa hawana kazi walikuwa wakimlilia Mungu awape kazi,lakini ndio watu hao hao,waliokuwa tayari kuumia wachelewapo kazini!!!
Bwana anatufundisha ( Kutoka 7:14-17). kwamba,Yeye ni Mungu wa muda,anajali sana muda.Anza leo,kutimiza maagano yako unayoyaweka mbele za Bwana katika muda. Ikiwa ulimwomba Bwana Mungu ya kwamba, kesho saa fulani utaomba,basi hakikisha muda huo huo unaingia kweli kwenye maombi bila kupoteza muda hata kidogo. Na ikiwa kama ulimwomba Bwana Mungu na kusema “kesho saa fulani nitasoma neno lako… ” basi jitahidi kutimiza hilo. Jifunze kwa Musa.
Ikiwa kama umebarikiwa,nifahamishe. Na kwa MAOMBI na ziada piga sasa +255 683 877 900
Whatsapp namba +255 746 446 446
Na Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comentarios