YESU YU HAI
- Mch. Gasper Madumla
- Jul 5, 2022
- 3 min read
Updated: Sep 5, 2022

Nimekusudia kukuletea matukio 8 Kwa ufupi, kama yalivyoandikwa katika biblia, matukio ambayo yanayomtambulisha Yesu Kristo kwamba ni hai na halisi. Biblia inasema katika 1 Wakorintho 15:3-4 (KJV)
“…, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko;”
Kamatia hayo “ alikufa,alizikwa na alifufuka katika wafu” hayo ni maneno muhimu sana ambayo unapaswa kuyashika katika imani yako ili kusudi unapomfuata Yesu ujue hakika Yesu alikufa,alizikwa na hatimaye akafufuka katika wafu, kuonesha Yesu Kristo sio wa kawaida kwa maana amepita wote. Matukio hayo ni kama ifuatavyo;
01. Kaburi kuwa wazi.
Kwa namna yoyote ile kulikuwa hakuna uwezekano wa kibinadamu kwa kaburi la Yesu kuwa wazi kwa sababu kwanza Wayahudi waliomsulubisha waliweka ulinzi mkubwa kwenye kaburi lake,kisha wakaweka na jiwe kubwa sana kwa hofu kwamba wanafunzi wake Yesu wasije wakamwiba.
Lakini pamoja na ulinzi wote huo,walikuta kaburi li wazi,mwanaume Yesu ametoka! Tukio hili lilifanyika“ Yerusalemu ” kaburini na lilitukia “Jumapili ya ufufuo” – Mathayo 28:1-8,Marko 16::1-8,Luka 24:1-12,Yoh.20:1-10
2. Yesu amtokea Mariamu Magdalene
Huyu ndio mwanamke wa kwanza mwenye sifa ya kumwona Yesu mara tu baada ya kukufuka. Tena Mariamu Magdalene alikuwa wa kwanza “kuhubiri injili ya ufufuo wa Yesu ” ulimwenguni kwa maana Yesu Kristo mwenyewe alimtuma,naye akatii. Kutii kwake ndio tunaona hata leo injili ya ufufuo wa Yesu Kristo inahubiriwa kote kote ( lakini hata kama asingetii bado injili ya ufufuo wa Yesu ingehubiriwa tu) Tukio hili pia lilikuwa hapo hapo Yerusalemu,siku ya Jumapili – Marko 16:9-11,Yoh.20:11-18
3. Yesu akiwatokea baadhi ya wanawake.
Kulikuwa na kusudi kubwa la Yesu kuanza kuwatokea wanawake kuliko wanaume. Kwanza alikuwa akiwatambulisha wanawake kama vyombo viteule vya Bwana,na kuonesha kwamba ni watu muhimu sana katika huduma (alijua nguvu ya mwanamke katika huduma). Lakini pili kuna kitu cha utofauti kilichopo ndani ya mwanamke,aliona “moyo wa kujitoa” ambao kwa moyo huo wanawake walijitolea kwenda kaburini mapema kulitizama kaburi.
Mazingira ya kipindi kile hayakuwa mazingira rahisi kwa mtu yeyote ambaye ni mfuasi wa Yesu kujitokeza hadharani, lakini wanawake walithubuti kujitokeza hadharani na kwenda moja kwa moja hadi kaburini,kisha Yesu alipouona moyo huo,alijidhihilisha kwao – Mathayo 28:9-10
4. Yesu ajidhihilisha kwa Kleopa na rafiki yake waliokuwa wakitenda Emau
Hili lilikuwa ni tukio la nne la Yesu kuuthibitishia ulimwengu kwamba yu hai. Hawa majamaa wawili walikuwa wamefumbwa macho wasimtambue Yesu jemedali,mwamba aliyewatoka walinzi wa kaburi! Inaonekana Kleopa na mwenzake walikuwa ni miongoni mwa wafuasi wa Yesu maana walikuwa wanaamini. Tukio hili lilikuwa njiani kuelekea kijiji cha karibu kutoka Yerusalemu kiitwacho Emau,siku ya Jumapili- Marko 16:12-13 , Luka 24:13-35.
5.Yesu Kwa Petro
Petro mtume mtu aliuekuja kuwa na usongo sana wa injili baada ya Yesu Kristo kufufuka,naye alipata neema ya kipekee kutokewa na Yesu mwenyewe. Bado wakiwa wote Yerusalemu, Yesu ajidhihilisha kwa Petro. Luka 24:34,1 Wakorintho 15:5
6. Kuvuviwa kwa wanafunzi 10
Wanafunzi wakiwa katika hali ya hofu mara tu baada ya mateso ya Yesu hadi kifo chake,walikuwa pamoja katika chumba cha juu huko Yerusalemu. Ingawa Yesu alikwisha waambia kwamba atafufuka siku ya tatu, lakini hofu ya wabaya wao iliwasumbua.
Hapo walipokuwa wamefunga na milango wakiwa gholofani,Yesu akawatokea. Tukio hili lilikuwa na lengo la kuwafanya upya wanafunzi wapokee uzima / Roho mtakatifu lakini ( lakini si ubatizo katika Roho mtakatifu) ilikuwa ni sawa na Yesu kuwapa wokovu wanafunzi wake au kuokoka Kwa wanafunzi. – Yoh. 20:19-23,Luka 24: 36-43
7. Thenashara/ Wanafunzi 11 wakiwa wanakula pamoja.
Mioyo ya wanafunzi wake Yesu ilipoteza imani,hawakusadiki. Yesu akajidhihilisha kwao kwa kuwafanya waamini kwamba Kila alichosema ni lazima kitimie. Walipokuwa Yerusalemu hapo hapo wakiwa 11 aliwatokea – Marko16:14,Yoh.20:26-31 na 1 Wakorintho 15:5
8. Yesu akijidhihilisha kwa Petro,Tomaso/Pacha, Nathanieli, Watoto wawili wa Zebedayo,na wanafunzi wawili ( Jumla Wanafunzi 7)
Tukio hili lilikuwa kipindi ambacho wanafunzi wake hawa walirejea katika kazi zao za uvuvi. Wakati wakivua samaki ndipo Yesu naye akawatokea hapo hapo. Walikuwa wakivua katika bahari ya Galilaya au ziwa Galilaya,mahali ambapo hata leo lipo halisi nchini Israeli. Haijulikani hasa ni siku gani alipowatokea,lakini aliwatokea katika kazi yao ya uvuvi – Yoh. 21:1-25
Pamoja na matukio hayo manane(8), pia yapo matukio mengine matano ambayo yanathibitisha ya kwamba Yesu amefufuka kweli kweli,yu hai. Mfano; moja ya hayo matukio matano,ni tukio la Yesu Kristo “kujidhihilisha kwa Paulo” – Matendo 9:1-19.
Hayo yote ni kwa mujibu wa biblia yaliyopata kuandikwa. Pia kuna matukio mengine ambayo Yesu mwenyewe akiwatokea watakatifu wake hata zama za leo ambayo hayapo katika maandiko hii yote ni kuonesha ya kwamba tupo pamoja naye Yesu Kristo.
Ikiwa umebarikiwa nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja.
Na Kwa msaada zaidi unipigie simu Kwa+255 683 877 900
What’s app number +255 746 446 446
Na Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE
Comments