MTUME PAULO CHINI YA GAMALIELI
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 28, 2022
- 3 min read
Updated: Aug 29, 2022

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Mtume Paulo ni mtume wa namna yake katika mitume waliowahi kuishi hapa duniani ingawa hakuwa miongoni mwa wale mitume/ thenashara 12 wa Yesu. Lakini alama yake aliyoiweka kamwe haiwezi kufutika kwa sababu alama yake ni kazi ya Yesu mwenyewe.
Kumbuka ;
Kuna mambo mengi mno ya kuandika kuhusu mtume Paulo, lakini kwa sehemu ndogo sana najaribu kuyaangazia maisha yake ya “umishonari” hasa hasa katika “ elimu yake” aliyoipata ili kusudi iwe somo kwako.Utume aliopewa na Bwana Mungu hakutokana na mapenzi ya mwanadamu yeyote bali Mungu ni kutokana na mapenzi ya Mungu – Wagalatia 1:15-16
Pamoja na kukirimiwa kipawa cha ufunuo na hekima,mtu aliyenyakuliwa mpaka mbingu ya tatu,na kusikia maneno yasiyotamkika ambayo haijuzu mwanadamu ayanene ( 2 Wakorintho 12:1-4),mtu huyo aliyekuwa na uwezo wa kipekee wa kunena katika Roho zaidi ya watu wote ( 1 Wakorintho 14:18)
mtu huyo ni Paulo mtume. Lakini alikuwa na mwanzo wake wa haya yote, katika huo mwanzo tunaweza kujifunza mambo mengi mno. Najaribu kuchukua jambo moja tu. Nalo ni “ Paulo kuwa chini ya Gamalieli “
“ Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi;” Matendo 22:3
Paulo anaanza na utambulisho wake kwamba yeye ni nani hasa,anasema ;
1.Yeye ni myahudi – Kuhusu familia
Ilikuwa ni vyema kwa Paulo kujitetea kwa kueleza kuhusu familia yake,ili wenye kumshtaki wajue wanamshtaki mtu wa namna gani. Na kwa kuwa ni myahudi pia ni Mfarisayo ( Matendo 23:6). Tena raia wa kirumi (Matendo 22:25-28). Ingawa mama yake hafahamiki lakini biblia inawataja ndugu zake wachache kama vile dada yake aliyekuwa akiishi Yerusalemu,Pia inamtaja binamu wake -Matendo 23:16
2.Alilelewa na kujifunza chini ya Gamalieli.
Paulo alifundishwa ya baba zake kwa usahihi sana kuliko ndugu zake. Tendo hili linaonesha kwamba Paulo alikuwa ni mtu wa jitihada sana katika “elimu“,hivyo ni sawa na kusema alikuwa ni “msomi” mzuri na ndio maana wanazuoni husema kwamba Paulo alikuwa ni mbobevu wa sheria na nyaraka zake zina mafunuo.
Ile namna ya kuwa chini ya mwalimu Gamalieli kumlimsaidia sana kujifunza sheria vyema kiasi kwamba hata Wayahudi hawakuweza kumkamata katika sheria. Pamoja na kwamba inawezekana hapo mwanzo alikuwa hajui kama ataokoka na kuwa mtume wa mataifa.
Roho mtakatifu alikuwa na sehemu yake muhimu sana kumwongoza lakini na “ elimu ” ilikuwa na sehemu yake ambapo elimu ilikuja kumsaidia hapo baadae.
Kitendo cha Paulo kuketi chini ya miguu ya mkufunzi kilimwongezea hatua ya ufanisi katika kazi yake. Hatua hii ya Paulo aliyoipitia ya “kujifunza” ni muhimu sana kwako kwa maana bado kuna mengi hujui.
Paulo kuwa chini ya Gamalieli ilikuwa inatoa picha ya unyenyekevu ambao Paulo alianza kufundishwa mapema hata kabla ya kupokea neema ya wokovu na huduma. Ambapo baadae alikuwa si chini tena ya Gamalieli bali chini ya Yesu ambaye ni mwalimu wa walimu. Lakini unyenyekevu huo wa kuwa chini ya mtu,ulimweleza vile ambavyo baadae hatakuwa hana budi kushuka zaidi mbele za Bwana. Ili Bwana abakie Bwana.
Kumbuka;
Kuna siri ya kukaa chini ya Gamalieli. Ikiwa Bwana anakutuma kazi kwa watu fulani wa jamii fulani basi uwe na ukahika atakuinulia Gamalieli ili kusudi ujifinze vyema kabla hujatoka na kwenda. Lakini ukimkataa Gamalieli,umekataa maarifa na ufanisi wa huduma yako. Ni dhahiri Paulo alikemewa na kuonywa juu ya sheria alizokuwa akijifunza chini ya Gamalieli, lakini hatuoni popote kwenye biblia kwamba Paulo alimkimbia au kumdhalau Gamalieli mkufunzi wake Kwa sababu ya maonyo
Je wewe upo chini ya miguu ya nani? Gamalieli wako yupo? Waweza kustahimili kukemewa na kuonywa na Gamalieli? Lakini vipi leo,hali ikoje? Unajiongoza?
Tumekuwa na mitume wengi leo ambao hawana akina Gamalieli au wamewakimbia akina Gamalieli yaani ni mitume ambao hawataki kuwa chini ya Gamalieli/ mkufunzi.
Paulo alikuwa msomi
Paulo alipenda kujifunza kwa waliomtangulia katika huduma,kazi na maisha kwa ujumla wake. Kwa maana tunaona hata alipokutana na Akila na Prisila bado alitafuta sana maarifa ya elimu ya ufundi wa mahema,na hatimaye Akila na Paulo wakafanya kazi pamoja ( Matendo 18:1-3)
Kama hiyo haolitoshi,tunaona tena pale Paulo alipokuwa yupo kifungoni kwa ajili ya Kristo, aliona kifungo si kitu zaidi ya kusoma / kuendelea kupata maarifa kupitia vitabu vya ngozi. Ukisoma 2 Timotheo 4:13 utaona akiagiza vitabu aletewe huko kifungoni.
Jambo la kushangaza wakati huu,ni pale unapoona baadhi ya watumishi wakikataa maarifa na kuikimbia shule na kuona shule itawapotezea upako.
Au pale kuona Mtumishi kukataa kuwa chini ya miguu ya mkufunzi akijidhania upako alionao unamtosha !!! Jifunze sana kuhusu kutafuta maarifa . Na rudi shule,bado kuna safari ndefu ya kujifunza. Lakini pia ni vyema uwe chini ya Gamalieli.
Ikiwa kama umebarikiwa, nifahamishe. Pia Kwa msaada zaidi pamoja na maombezi tumia namba hii. +255 683 877 900
What’s app number +255 746 446 446
Na Mch. Gasper Madumla
UBARIKIWE.
Comments