UKOO WA YESU KRISTO
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 22, 2022
- 3 min read
Updated: Aug 29, 2022

“Ukoo wa Yesu/ The Genealogy of Jesus “
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Pamoja na kwamba Kristo alikuwepo hata kabla ya uumbaji wa ulimwengu ( Yoh.1:1,17:5. Tena alikuwepo kabla hata ya Abrahimu ( Yoh.8:58). Yeye hana mwanzo wala mwisho. Lakini kwa kuwa alivaa mwili na kukaa kwetu,basi ni dhahiri alikuwa na jamaa ili kuunganisha “nasaba”
Kwa maana “ Kristo” ni mtiwa mafuta ni masihi wa Mungu. Maandiko mengi yanaeleza juu ya uwepo wake kabla kuwekwa misingi ya ulimwengu. Na Kristo ni Yesu.
Mwinjilisti Mathayo anaanza kwa kuutaja ukoo wa Yesu kwa sababu yeye mwenyewe aliyashuhudia maisha ya Yesu kwa kuyaona,kwa lengo kubwa la kumweleza Yesu kuwa ndiye masihi pekee na Mwana wa Mungu. Mwanga huu alioutoa Mathayo unatupa wepesi wa kuelewa hasa maisha ya masihi wa Mungu.
Kwa maana Mathayo amefuatilia mababu wa Yesu kupitia kwa Yusufu baba wa kufikia wa Yesu. Ukoo wa Yesu unajengwa imara na nguzo mbili za mwazo nazo ni “Ibrahimu na Daudi” ambao wanatajwa mwanzo kabisa ( Mathayo 1:1). Hivyo Yesu ni mwana wa Daudi,mwana wa Ibrahimu.
Ilikuwa ni desturi ya kiyahudi kumtambulisha mtu kwa kutaja mababa,na mababu wa mtu ( Hesabu 13:4-13, 1 Samweli 1:1 n.k). Ukoo wa Yesu ulifuata unabii uliotolewa hapo mwanzo kabisa kwamba katika Ibrahimu atatokea masihi wake – Mwanzo 12:3
Kumbuka;
Yesu alikuwa ni uzao wa Daudi kufuatia ukoo wa Yusufu baba wa kufikia. Kuzaliwa kwake Yesu ni Kwa uweza wa Roho mtakatifu kupitia tumbo la Mariamu – Mathayo 1:18-23. Lakini kisheria aliandikishwa kama mtoto wa Yusufu. Mama yeke Mariamu naye alikuwa wa ukoo wa Daudi.
Kwa kuwa Yesu baba yake alikuwa Mungu hivyo damu yake haikuwa damu ya kawaida yenye vinasaba na Yusufu bali vinasaba vyake vilikuwa ni vya Mungu mwenyewe ndio maana damu yake Ina nguvu mpaka leo. Hivyo Kwa habari ya Yusufu baba mlezi wa Yesu ni sawa na kusema Yusufu alimchukua Yesu na kuishi naye kisheria,
Tendo ambalo hata leo linafanyika la kumchukua mtoto ambaye si wako kwa kuzaa,labda waweza kumchukua katika ngazi ya kiserikali ( kama vile ustawi wa jamii) na kumlea kama mwanao kisheria.
Kama Yusufu alifanya hivyo,basi hata wewe unaweza kufanya hivyo,na ni baraka sana maana utakuwa umewasaidia watoto wanaozaliwa na kutelekezwa. Lakini Yesu hakutelekezwa,kumbuka hilo.
Mpangilio wa ukoo wa Yesu
Laiti kama mpangilio huu ungelipangwa na mwanadamu basi ni dhahiri kuna watu wasingelipangwa katika ukoo huo. Au watu wengine wangelisahaulika. Mtu kama “ Rahabu yule aliyekuwa kahaba”- Mathayo 1:4, Yoshua 2:1. Hata kama baadae Rahabu aliokoka lakini kitendo tu cha kuwa kahaba kingewafanya watu kumsahau kumfuta katika ukoo wa Yesu, masihi.
Kuna kitu nataka ujifinze hapo, kwamba Mungu haangalii kama mwanadamu aangaliavyo. Yeye mpangilio wake ni wa ajabu sana. Hivyo ukifuatilia ukoo wa Yesu, Bwana Mungu alikusudia kumfanya Yesu azaliwe kwa watu wa kawaida kabisa ili ukombozi wake ukamilike.
Kumbe inawezekana ukazaliwa na kahaba na baadae wewe ndio ukabeba kusudi la Mungu katika ukoo wako. Kama ni hivyo,basi si kitu kuwa na kina Rahabu kwenye ukoo kwa mtu aweza kuwa kahaba kama Rahabu Lakini baadae akaokolewa ikabaki historia kitu muhimu ni kujitenga Sasa na ukahaba na kuokoka.
Pamoja na hayo,historia ya ukoo wa Yesu unaonesha wazi kabisa kwamba Yesu alikuwa wa nasaba ya kiyahudi mahali ambapo masihi wa Mungu alikusudiwa azaliwe. Ukoo wa Yesu ni mpana sana,hauesabiki Kwa maana yeye ni uzao wa Ibrahimu,uzao mwingi kama mchanga wa pwani.
Kwa maana wakristo wote ulimwenguni wanahesabika kuwa sehemu ya ukoo wa Yesu na hata wale ambao bado wangali katika viuno na matumbo ya wakristo watakao kuja kupokea Neema ya wokovu nao ni sehemu ya ukoo wa Yesu. Kwa kuwa lango la kujiungamanisha na ukoo wa Yesu bado liko wazi,ni vyema kukata shauri kwa kupokea neema ya wokovu,
kumkiri Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako na kukubali kuongozwa na yeye,hapo utakuwa nawe sehemu ya ukoo wa Yesu Kristo.
Ikiwa kama umebarikiwa, nifahamishe Kwa + 255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Na Mch. Gasper Madumla
UBARIKIWE
Comments