YESU ALIBEBA DHAMBI ZAKO
- Mch. Gasper Madumla
- Feb 6, 2018
- 3 min read

Na. Mch Gasper Madumla
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi..
“ Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.” 2 Wakorintho 5:21
“alimfanya kuwa dhambi” hii ina maana Yesu yeye alifanywa dhambi kwa ajili yetu na sio tu alifanyika kuwa dhambi badala yetu. Yaani Yesu alijiweka kuwa dhambi,yaani dhabihu ya dhambi kwa akibeba ghadhabu ya Mungu. Naomba uelewe hivyo. Kumbuka;huyo ni mtu aliyekuwa haijui dhambi yaani hakuwa na dhambi,lakini kwa sababu ya pendo lake Yeye alikubali kuwa dhabihu ya dhambi.
Ghadhabu ya Mungu ilipanda sana kwake kiasi cha kuiangamiza ulimwengu,lakini mwanadamu mmoja mkamilifu akakubali kubeba ghadhabu yote ya Mungu. Si jambo dogo hilo,ebu tafakari juu ya ghadhabu ya Mungu. ~ neno “ ghadhabu” ni hasira kali iliyopitiliza yenye kuambatana na adhabu kubwa,tena Mungu ndiye awezaye kuadhibu vikali,ingawa Yeye si mwepesi wa hasira. Ilikuwa tuangamie sote kwa sababu ya dhambi na maovu yetu,maana mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23)
Lakini Yesu akafanyika dhambi,kitendo cha Yesu kukubali kufanyika dhambi ni kitendo cha “upatanisho” kati yetu sisi (ambao kwa kweli tulikwisha hukumiwa mauti) na Mungu. Ebu tafakari jambo hili,na utagundua kwamba ikiwa wewe ni mtenda dhambi umekwisha hukumiwa,ukisubiri mauti kama mshahara wako,lakini yupo Yesu Kristo sasa ambaye ni dhabihu ya dhambi, amekuja kulipa gharama yako,hivyo huna budi kumpokea Yesu Kristo awe Bwana na mwokozi wa maisha yako.
Hapo katika agano la kale,mtu alipotenda dhambi ilimpasa hukumu mara moja. Lakini kwa sababu ya pendo la Mungu akawahurumia kwa kuwawekea sheria kwamba,mtenda dhambi apeleke dhabihu ya dhambi kwa ajili ya dhambi zake. YESU alikubali kuwa dhabihu ya dhambi zetu,ili wewe usife utakapo muamini na kumpokea,tena upate kuhesabiwa haki bure.Neno hili“haki ya Mungu katika Yesu” maana yake ni hali ya kuwa na uhusiano mwema na Mungu ndani ya Yesu.
Kumbuka hili;mateso yaliyofanyika pale msalabani Kalvari hayakuwa ya kuigiza kama filamu,yalikuwa ni mateso halisi yaliyomuumiza sana Yesu. Mungu alikuwa amekasirishwa na dhambi za walimwengu,hivyo hasira yote ilimuangukia Yesu ambaye amebeba ghadhabu ya Mungu,hata Yesu akaona kuachwa na Baba yake. Haikuwa kawaida kawaida!!! Leo unapotenda dhambi,unajua gharama aliyolipa Yesu pale msalabani? Unapokataa kuokoka,unajua gharama aliyolipa Yesu pale msalabani kwa ajili yako wewe? Mi sijui kama unaelewa hiki nikisemacho kwako!
Kifo cha Yesu pale Kalvari kilikuwa kifo cha kubeba dhambi ya kila mtu atakayeweka imani yake kwa Yesu,( kwa kumpokea Yeye). Mungu hana upendeleo kwa mtu au taifa lolote( Matendo 10:34-35). Ingawa kulikuwa na ghadhabu ya Mungu juu yako,lakini Mungu alikuwa na mpango nawe kukuokoa kwa kifo na kufufuka kwa Yesu. Kumbuka,Yesu alikuwa mpatanishi wetu maana hatukufaa mbele za Mungu,
“ kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa;” Warumi 3:23-25
Sisi sote hatukufaa mbele za Mungu,tulipungukiwa na utukufu wa Mungu. Lakini sasa tumehesabiwa haki bure kwa upendeleo wa Kiungu tu,katika njia ya ukombozi katika Kristo Yesu. Hii ina maana kila amekusudiwa asiangamizwe kwa kujitoa kwake Yesu kuwa dhambi,sasa ukipokea ukombozi katika Yeye,hapo ndipo utakapohesabiwa haki bure kwa neema ya Mungu. Unaona hapo umuhimu wa kuweka imani yako kwa Yesu,na kumpokea Yeye.
Nikitafakari pendo la Mungu kunihurumia mimi niliyekuwa ninastahili nilipwe adhabu kubwa ya mauti kwa sababu ya dhambi zangu na makosa yangu yote,hapo ndipo natamani kulia si kwa sababu ya uchungu bali kwa sababu ya furaha hata kukosa cha kusema mbele za Mungu. Na nikibakia kumtukuza Mungu tu kwa matendo hayo makuu na yote anayoyatenda.
Hivi unajua Mungu hana upendo bali Yeye wenyewe ndio pendo,lazima ujue Yeye anakupenda sana kiasi cha kukubali mwanawe wa pekee asiyeijua dhambi kuwa dhambi. Hivyo;Jambo moja la kujifunza leo hii ni kwamba Yesu amekwisha kukulipia gharama ya dhambi zako pale Kalvari msalabani kazi imebaki kwako ya kujiunganisha na msamaha huku kwanza kwa Kusudi la Mungu ni kukuhesabie haki bure katika Yesu. Sijui kama unanipata vyema.
Ingawa, yamkini ni mtu mwenye dhambi mpaka sasa,lakini nataka nikupe habari njema kwamba bado hujachelewa,ukweli ni kwamba waweza kumpokea huyu Yesu sasa popote pale ulipo. Unachotakiwa kufanya ; unipigie simu au mpigie mtumishi yeyote iliye karibu nawe kisha kwa imani tuombe pamoja sasa.
Kumbuka; haki ya Mungu inapatikana Katika Kristo tu. Ukihitaji kuwa mwenye haki huna budi kumpokea Yesu Kristo kwanza ili uanze kutengeneza mahusiano yako na Mungu.
Kwa msaada zaidi,na maombezi nipigie kwa simu+255 683 877 900
Namba ya what’s app ni .+255 746 446 446
Mchungaji Gasper Madumla.
UBARIKIWE
Comentários