ROHO YA SIMBA
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 21, 2022
- 3 min read
Updated: Aug 29, 2022

“Jivike roho ya simba”
BwanaYesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Waswahili husema paka ana roho ngumu sana, wengine husema paka ana “roho saba” hii yote ni kuonesha ugumu wa ndani wa paka. Simba naye ni jamii ya paka mkubwa wa mwituni mwenye roho ile ile ngumu kama wasemavyo waswahili.
Hivyo sifa hii ni sifa ya kiroho ambayo watu wa Mungu wanapaswa wawe na “roho ngumu ” yaani roho isiyokata tamaa kwa haraka. Ukumbuke; paka ukimpiga sana huwa inafika wakati anafanya maamuzi magumu ya kumgeukia mpigaji na kuanza kupambana naye,
tabia hii huonesha paka anaeonewa sana hukataa uonevu kwa kuanza kupambana na mtesi wake akitumia nguvu zake binafsi kwani huamini atashinda katika upambanaji
tena wataalamu wa wanyama poli husema Simba ndio wa pili kwa uzito baada ya chui / tiger.
Katika jarida la Wikipedia linalozungumzia simba linasema, ;
“ Dume anafikia urefu wa mwili pamoja na kichwa wa sentimita 170 hadi 250; kimo cha mabegani ni cm 120. Dume mkubwa anaweza kuwa na uzito wa kilogramu 225. Jike ni mdogo wake akiwa na urefu wa 140 hadi 175 cm, kimo cha mabegani cha cm 100 na uzito wa kg 150.Simba huishi kwa wastani wa miaka 10-14 mwituni, huku katika hifadhi huweza hata kufika zaidi ya miaka 20. ” (Nukuu kutoka Wikipedia)
Nukuu hiyo inaonesha namna ambavyo simba ni mnyama hatari,mwenye misuli mikubwa. Na ndio maana usiombee ukutane na simba ,Wee!!!hatarii. Lakini uwepo wa simba ni kazi ya uumbaji wa Mungu kuumba wanyama tofauti tofauti. Na kila mnyama amepewa kitu tofauti mnyama mwingine.
Ndani ya simba kuna “ roho ya simba” inayomtambulisha kuwa yeye ni simba. Na hivyo ndivyo Bwana alivyomfanya kumtofautisha na wanyama wengine. Hivyo “ roho ya simba ” inamtambulisha katika maeneo mengi,lakini nimechagua mambo 3 tu kukuonesha simba anatembea katika roho gani ambayo wewe unapaswa kutembea katika roho hizo,
1. Nguvu
Ukweli ni kwamba kuna uwezo mkubwa ndani yake simba,na uwezo huu utambulikana kama “roho ya nguvu” inayomtambulisha simba. Kwa maana ukamilifu wa simba kuwa simba ni juu ya nguvu zake. Kwa sababu hiyo simba ni ishara ya nguvu! Kumbuka hata pale Bwana alipomwambia Yoshua katika Yoshua 1:9 “uwe hodari na ushujaa..” Ilikuwa na maana Joshua ajivike roho ya nguvu,mithili ya roho ya simba.
2.Utayari wa kupigana.
Umwonapo simba msituni wakati wote yupo tayari kuzichapa! hata kama ukimstua usiku bado utamwona katika hali hiyo hiyo,Hivyo simba hudhani wakati wote ni wakati wakujilinda na kupambana,unajua hata kula kwake simba ni lazima apambane kuwinda. Hali ya namna hii hutokana na namna ya kujiamini. Hii ni roho ya kipekee kabisa ambayo hata Mungu anatazamia iumbike kwako.
Sasa leo hatupigani kwa jinsi ya mwili kwa maana sio vita yetu hiyo ( Waefeso 6 :12). Lakini tunapigana kila siku dhidi ya nguvu za giza. Mtu mwenye utayari wa kupigana katika ulimwengu wa roho ndio washindao! Waweza kujivika roho ya simba wakati wa maombi yako.
3. Sauti yenye utiisho
Fikiria simba anaponguruma,pata picha hiyo! mgurumo wake ni wa kutisha kiasi kwamba wanyama wengine hukimbia na kujificha! Utiisho huu ni kielelezo tu cha kuonesha utiisho uliopo ndani ya Kristo ambaye naye ni simba wa Yuda,mwenye utiisho na mamlaka. Na utiisho huo ni “roho halisi” ambayo unapaswa kuiomba. Kibiblia sauti yenye utiisho huambatana na sura ya kigumegume!
Ujawahi ona kuna watu ambao wakiingia katika mji,mji unataharuki hadi kamati ya wachawi wanajificha kwa sababu wamesikia mtu wa Mungu amenena au wamemwona! Hali hiyo inapaswa iwe kwako,ifike wakati hata unaporejea nyumbani kwenu,wazee wa jadi wanapokuona au kusikia sauti yako waombe poo! Ombea kuvikwa sauti yenye utiisho na mamlaka hiyo ni roho ya simba!
Kuna mengi mazuri ya kujifunza katika roho ya Simba. Lakini hayo machache yanatosha kukupa mwanga!
Ikiwa umebarikiwa nifahamishe.
Na kwa msaada zaidi pamoja na maombi,piga sasa + 255 683 877 900
What’s app number ni +255 746 446 446
Na Mch.Gasper Madumla.
UBARIKIWE
Comentarios