UKOMBOZI WA KIFIKRA – 01.
- Mch. Gasper Madumla
- Mar 25, 2020
- 4 min read
Updated: Aug 30, 2022

Kwa ufupi,
Maisha ya mwanadamu yanapitia katika nyanja mbali mbali za ukombozi,hii inaonesha wazi kwamba mwanadamu kwa sehemu kubwa ni hayuko huru. Hivyo “ukombozi wa kifikra” una maana kuwekwa huru katika fikra/akili. Ingawa baadhi yetu tumekombolewa ( kwa damu ya Yesu,/tumeokoka) lakini inaonesha kwamba hatuko huru. Na kama hatuko huru basi ina maana tu watumwa bado hali tumekombolewa. Kivipi?
kwanza tazama hapa “ Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru. ” Yoh.8:31-32
Hao Wayahudi waliomwamini Yesu,walimwamini kama vile leo mtu anavyomwamini Yesu,Ingawa walikuwa wanamwamini lakini bado walikuwa ni “watumwa wa dhambi”. Kumbe mtu anaweza akamwamini Yesu hata akampokea /akaokoka lakini akawa bado ni mtumwa wa dhambi. Watu hao walihitaji wakombolewe katika utumwa wao.
Kumbuka pia; Mungu aliwatoa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri baada ya miaka 430 ya utumwa wao. Kwa lengo la kuwapa nchi nzuri ya ahadi isiyokuwa na utumwa. Lakini hata hivyo bado walipotolewa walilia kurejea Misri. Walitamani bora wangefia utumwani Misri pale walipozikumbuka sufuria za nyama – Kutoka 16:2-3.
Hali inatuonesha wazi kabisa watu hawa walikombolewa lakini bado walikuwa ni watumwa wa kifikra kwa maana utumwa uliathili akili zao kiasi kwamba hawakuona mema na safari ya kule waendako bali wao waliona sufuria za nyama za wamisri.Ukombozi uliofanyika kwa wana wa Israeli unafanana kabisa na ukombozi tulionao leo wa kumwamini Kristo Yesu yaani kuokoka. Lakini hata hivyo bado fikra zetu zimefungwa,hatuoni kama Bwana aonavyo,bali tunaona utumwa tu!
Matokeo ya kufungwa fikra;
01. Kukosa mwelekeo sahihi / malengo.
Hata Israeli baada ya kutolewa utumwani hali wamefungwa katika fikra,hawakuwa na malengo yoyote. Hivyo walijiendea / waliishi bila kuona wapi wanapoelekea isipokuwa Musa aliwahimiza sana waifuate njia. Hata hivyo ilikuwa ni shida kubwa mno kumfanya yeye aliyekuwa utumwani Misri kwa miaka mingi ya 430 kusahau utumwa mara moja. Ilihitajika kazi ya ziada ya kuwaonesha njia watakayoelekea,hata hivyo wengine waligoma na kufia jangwani kwa maana walizoea utumwa na hivyo wakakosa malengo kabisa.
Kawaida mtu aliyefungwa fikra hukosa malengo,wala hajui aelekeapo! Na ndio maana unaweza kuona mtu ( anaweza akawa ameokoka kabisa) lakini hana malengo ya maisha yake,wala hajawahi kufikiria kuhusu malengo,hivyo mtu huyo ujikuta anaishi kwa kile kitakachokuja mbele yake,kukipambazuka hufanya shughuli zake atakazozikuta,kisha anakwenda kulala pasipo kupanga chochote!!!!
“ Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida.Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake.” Mathayo 25:14-18
Biblia inatoa mifanao ya watu wanne,watumwa watatu na mmoja wao ni boss / bwana wao aliyepanga mpango wa kusafiri kwa muda mrefu atakao yeye. Kisha bwana huyo aliwapa fedha zake,kwa kila mmoja alimpa fedha kwa kadiri ya uwezo wake wa kuzalisha. Bila shaka huyu bwana alikuwa ni mfanyabiashara mwenye kutafuta faida kwa watumwa wake. Yule aliyepewa talanta tano,alikuwa na uwezo wa kuzalisha talanta tano zaidi,
hivyo kama angezalisha talanta nne,basi angekuwa chini ya kiwango chake cha uzalishaji. Na yule wa pili naye alikuwa na nguvu ya kuzalisha talanta mbili zaidi. Na hatimaye yule wa moja alipaswa azalishe moja zaidi sawa sawa na nguvu/kiwango chake cha uzalishaji. Hivyo utagundua kwanza,viwango vya uzalishaji vilitofautiana kwa kila mmoja. Lakini hiyo sio ishu kubwa,bali mfanya biashara huyu aliporudi alimshangaa yule aliyepewa talanta moja,ambaye hakuweza kuzalisha kabisa!
Unafikiria kwa nini hakuweza kuzalisha?
Kupitia majibu yake yule mwenye moja aliyeshindwa,tunaweza kuziona sababu zilizomkwamisha. Moja ya sababu kubwa,ni “ kukosekana kwa malengo ya kuzalisha” kwa maana aliogopa kujaribu biashara,naye alisema alimjua yule mfanya biashara kwamba ni mtu mgumu avunaye asipopanda! Kwa mtazamo huu tu,unatuonesha kwamba alikuwa akitofautiana na mitazamo ya wale wawili waliofanikiwa.
Hakuona kama wengine walivyoona,na kw sababu hiyo hakuwa na malengo yoyote ya kuzalisha bali lengo alilokuwa nalo ni kwenda kuificha chini talanta aliyopewa,ili baadae akirudi bwana wake airudishe kama ilivyo. Bila shaka,alifungwa fikra zake. Hakujua nini cha kufanya kilichohitajika kwa wakati ule. Kipindi bwana wao alipowapa aliwaeleza kabisa kwamba atarudi kukagua hesabu zao,kwa hiyo kila mmoja alijua kwamba anatakiwa aende kuifanyia biashara talanta aliyopewa,
lakini wakati wenzake wanahangaika kutafuta faidi yeye aliona ni bora aifiche,kwa kuwa hakuwa na malengo ya uzalishaji.
Bila shaka huyu ndugu mwenye talanta moja,aliishi katika kipindi kigumu sana kwa maana hakuwa na faida yoyote ya kujikimu kimaisha kwa sababu yule bwana wao alikaa kwa muda mrefu katika safari yake maana biblia inasema “baada ya siku nyingi akaja bwana wao” kuonesha kwamba kulikuwa na kipindi kirefu cha muda cha safari ya bwana wao.
Katika kipindi chote hicho,yule mwenye talanta moja alikuwa akila nini?alikuwa akiishi vipi?
kwa maana aliificha talanta yake,na wakati huo wenzake wanatanua na kufanya biashara kwa muda na wote walikuwa wanajua kwamba kuna siku bwana wao atarejea. Hivyo ufahamu wa huyu mwenye moja ulikuwa umefungwa kiasi kwamba hakuwa na malengo yoyote.Lakini ndivyo watu wengi leo wanaishi hivyo bila malengo,na miaka inasogea lakini wao hawasogei popote wapo pale pale kama huyu ndugu aliyeificha talanta yake. Kumbuka;Kuishi bila malengo ni kupotea huku unajiona!!!
ITAENDELEA…
Ikiwa umebarikiwa na ujumbe huu,basi nifahamishe tupate kumtukuza Mungu pamoja. Lakini inawezekana labda unahitaji MAOMBI kwa maana nawe unapitia changamoto hii,
Basi kwa yote nipigie sasa kwa + 255 683 877 900.
What’s app namba ni +255 746 446 446
Na Mch.G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments