top of page

YAPASA UISHINDE DHAMBI.

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi.

Neno hilo “yapasa uishinde dhambi ” ni sawa nq kusema “lazima uishinde dhambi ” ( You must master sin).Bila shaka unaweza ukajiuliza kwamba “mtu anaweza kuishinda dhambi? ….Hivi inawezekana mtu akashinda uovu?..” n.k ni vyema kujiuliza hivyo. Lakini mimi leo nakwambia kwamba,inawezekana kuishinda dhambi ukiwa ndani ya Kristo. Kwa maana hakuna nguvu ya dhambi kwake aliye ndani ya Kristo,kwa sababu nguvu ya dhambi ilikwisha shughulikiwa pale msalabani,na wewe ikiwa umeokoka basi ujue hutakiwi tena kushindwa na dhambi ya aina yoyote ile. Na hiyo ndiyo kweli yenyewe.

  1. Kila mwanadamu aliyeumbwa na Mungu amepewa nafasi ya kufanya maamuzi.

Kitendo cha kuamua kipi ufanye na kipi usifanye kipo ndani ya uwezo wako. Na ndio maana unaweza ukachagua kufanya uovu au kutenda haki,au ukachagua mauti au uzima. Au unaweza ukachagua baraka,au ukachagua laana. Lakini kwa sababu akili za mwanadamu zinawazaga kuchagua mabaya tu siku zote,kwa sababu hiyo Mungu anakushauri uchague uzima ili uwe hai. ( Kumb.30:19).

Ikiona mpaka Mungu anakuelekeza uchague jambo jema basi ujue ameona ndani yako ya kwamba huwezi kuchagua lililojema,hivyo kwa kulijua hilo,amekushauri uchague uzima, uchague baraka ili uwe hai ukiwa na nguvu ya kufanikiwa. Ukweli ni kwamba wengi huchagua kufanya dhambi kama sehemu ya machaguo yao. Ebu fikiria mtu anayepanga kuzini,Je hajachagua kweli kumkosa Mungu?

Kwa maana mpaka uzini ni lazima upange na huyo unayekwenda kuzini naye,kisha utoke nyumbani kwako mbali,upande daladala au gari yako,tena ufike mahali na kumsubili,anachelewa na unamngoja kwa kiu,kisha unakwenda kutafuta nyumba ya wageni mkakamilishe uzinzi. Ukifika nyumba ya wageni utaanzia mapokezi ili ulipe kwanza chumba,kisha mhudumu akupe funguo na hatimaye uzini. Ebu cheki hatua hizo zote kama ulikuwa hujapanga kufanya dhambi ni nini hasa? Yaani kuanzia kwenye mawasiliano ya kuchati mpaka mfikie kwenye nyumba ya wageni, hapo umeamua kabisa kutenda dhambi kama sehemu ya maamuzi yako!

Mtazame Kaini ambaye anasimama akiwakilisha watu wote walioamua kufanya dhambi. Tena anawakilisha watu wote walioamua kwenda kinyume na utaratibu wa Mungu. Lakini yupo Habili yeye mtu wa haki,aliyeamua kwenda na Mungu. Kusimama kwenye kweli naye huwakilisha watu wote waliosimama kwenye kweli wakitafuta kuyafanya mapenzi ya Mungu.

Hawa wote wawili bila shaka walifundishwa jinsi ya kumwendea Mungu katika utoaji / sadaka. Mungu alikwisha weka utaratibh unaofaa wa kutoa dhabihu,na utaratibu huo akawafundisha Adam na Hawa ( Mwanzo 3:21) . Mungu alichinja mnyama badala ya kufa kwa Adamu na Hawa kwa sababu walitenda dhambi. Hili lilikuwa fundisho kwa akina Kaini na Habili kwamba sadaka ni ya wanyama ndiyo inapaswa kutolewa,nao walifundishwa tena na wazazi wao.

Lakini tunamwona Kaini mtu aliyeshupaza shingo yake kwa kuleta mazao ya ardhi kinyume kabisa na utaratibu uliowekwa. Bila shaka Kaini aliamua kwenda katika njia yake mwenyewe,kwa sababu aliamua kufanya dhambi tu. Isipokuwa Habili akabakia kwenye utaratibu uliowekwa. Maandiko yanatueleza Bwana akazipokea sadaka za Habili aliyekaa kwenye utaratibu uliowekwa ( Mwanzo 4:3-4). Hata hivyo,Mungu akasema na Kaini jambo la ajabu sana;

“Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.” Mwanzo 4:7

Bwana anamwambia Kaini hivi,wewe Kaini kwani ukitenda vizuri au ukikaa kwenye utaratibu unaotakiwa,hautakubalika? Kaini tazama dhambi sasa ipo hapo na inakunyemelea,lakini bado ipo nafasi kwa ya kuishinda. Jitahidi uishinde hiyo dhambi. Hii ni sawa na kusema Bwana alimpa Kaini nafasi nyingine ya kutubu na kugeuka.

Lakini tunaona Kaini hakuona haja ya kutubu,bali alifanya chaguo la kufanya dhambi! Na hatimaye akaua mdogo wake. Hata leo,Bwana anasema nawe kwamba; “kama ukikaa katika utaratibu wake vyema,hutakubalika? La umekosea basi geuka leo. Na kama hautageuka kwa toba leo,tazama dhambi itakuvaa kama ilivyomvaa Kaini “

Jiulize,ni mara ngapi unakaa nje ya utaratibu wa Mungu? Ni mara ngapi unamkosa,kisha wala huna haja ya kugeuka kwa njia ya toba? Sivyo hivyo Bwana atakavyo mpendwa,kwa maana ukiamua kukaa hivyo basi huna tofauti na Kaini, au huna tofauti na mtu aliyechagua kutenda dhambi. Jifunze kuishinda dhambi leo hii.

Ukichunguza maisha yako utagundua kwamba mara nyingi mwenyewe huwa unaamua kufanya dhambi fulani hivi ijapokuwa unajua kwamba ni dhambi lakini unafanya tena wakati mwingine unahaha / unaiangaikia kuitafuta dhambi yaani unafunga safari kutoka mtaa wa kwanza hadi huko kwenye mtaa wa saba,kwa ajili ya kukamilisha dhambi fulani. Lakini ukitambua neema ya Mungu kwako usingelifanya hivyo.

Ukiwa ndani ya Kristo, umekuwa kiumbe kipya,ya kale yamepita ( 2 Wakorintho 5:7). Lakini kwa nini bado unatenda dhambi mpaka sasa? Huku ukifurahia?

Nimetafuta sababu,namk nikaona kuna mambo muhimu sana ambayo bado yanatusumbua hata sasa ingawa tumeokoka tayari. Baadhi ya mambo hayo ni ;

01. Yesu bado hajafanyika kuwa Bwana na mwokozi.

Ukweli ni kwamba kuna tofauti kati ya kuokoka kwa maneno maneno tu,na ile namna ya Yesu kuwa Bwana. Hapo zamani mtu akiwa bwana,ina maana ya kwamba mtu huyo ndiye msemaji wa mwisho na mpangaji wa mambo yoyote. Mtu akiws bwana,akisema kwa mtumwa wake njoo huja,akisema nenda,huenda bila shuruti kwa sababu yeye ni bwana wa watumwa wake.

Hivyo hivyo,Yesu akiwa Bwana, maana yake ni Yeye ndiye msemaji na mpangaji wa matumizi ya mwili wako. Hii ikiwa na maana kila ulitakalo kufanya ni lazima upate kibali kutoka kwake,huna maamuzi ya kutumia mwili wako nje yake. Lakini ebu jiulize,ni kweli Yesu amekuwa Bwana kwako? Unanielewa lakini?

02. Ofa za waovu ( Mithali 1:10,15),( kuambatana na watu waovu)

Tabia za marafiki waovu,watu wenye njia mbaya. Watu wengi ingawa wameokoka lakini bado hawajatoka kwa watu wa dunia hii,hivyo hujikuta wakiendelea kutenda dhambi hata kama hawataki lakini kule kushiriki pamoja na wasioamini ni tanzi kubwa la kuangukia pabaya. Hujawahi ona mtu ambaye ni mpendwa lakini kampani yake ni ya watu wasiookoka? Halafu ikiwa wakikaa pamoja badala ya yeye kuwabadilisha ni wao wanaombadilisha na kumtumbukiza shimoni. Hata kama uko na ndugu zako wasiookoka ni lazima uishi nao kwa akili wasije wakakuzidi kete.

03. Kuishi mwilini kupitiliza.

Mtazame mfalme Daudi mtu aliyeupendeza moyo wa Mungu ( Matendo 13:22). Lakini biblia inasema alijikuta akitembea na mke wa mtu,( mke wa Uria jemedari wake kisha na kumuu huyo Uria – 2 Samweli 11 yote). Daudi alijisahau kama mtumishi wa Mungu, alipokuwa hana kazi maalumu,yupo mwilini tu,tamaa za mwili zilimshinda hatimaye akaangukia uzinzi. Ukiwa mwilini ni shida,kwa maana unaweza ukaenda kanisani lakini shetani dk yoyote anaweza kukupiga mweleka !! Jikague,wewe ni mtu wa namna gani,rohoni au mwilini? Kumbuka ; Watu wa mwilini ni chakula cha shetani. ( sababu hii ni kubwa kuliko zote)

Hata hivyo dawa ya kutokutenda dhambi ipo. Hata kama ikitokea umetenda kwa kutokukusudia dawa ipo na kusimama tena kisha kufunga hiyo hali ya kuanguka dhambini.

  1. Kuokoka kama bado ( 2 Wakorintho 5:17)

  2. Toba

  3. Omba kwa Roho mtakatifu akusaidie.

  4. Hakikisha unalijaza neno la Kristo kwa wingi ( Zab.119:11)

  5. Jitahidi sana kuwa mwombaji – omba mara kwa mara.

  6. Fanya mazoezi ya kukataa mabaya hata kama utachekwa na watu, au kudhalaulika,potelea mbali wakudharau,lakini wewe jitenge nao.

Ikiwa umebarikiwa na fundisho hili nifahamishe pia. Kwa maombezipia nipigie kwa namba hizi hizi + 255 683 877 900 

WhatsApp ni .+255 746 446 446

Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comentários


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page