YAKUPASA UISHINDE DHAMBI!
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 22, 2019
- 3 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Zipo dhambi zitokanazo na tamaa mbaya. Kama vile uzinzi, wizi,ulevi,masengenyo,n.k. dhambi za namna hizi zinajengwa kwanza na tamaa ndani ya mtu,biblia inasema“ Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.” Yakobo 1:14-15
Kwa mujibu wa andiko hili,dhambi ni zao la tamaa. Na dhambi ikikomaa inazaa mauti. Fikiria dhambi kama ya uzinzi, katika uzinzi mtu kwanza utamani,kisha tamaa yake inamtupa kwenye tendo lenyewe ambalo ndio tunda hasa la tamaa liitwalo uzinzi, na baadae mauti ujitokeza.
Uzinzi haupo bila tamaa.
Fikiria kisa hiki cha Daudi mfalme aliyemtamani mke wa jemedeli wake Uria,hata akajikuta akizini. Na baada ya dhambi ya kuzini,mauti ikafuatia ( 2 Samweli 11:2-7). Biblia inasema Daudi alipomwona mke wa Uria anaoga,“ tamaa” ikamwingia,na hakuweza kuishughulikia tamaa hiyo,mzee akashindwa kujizuia na hatimaye akadondokea kuzini,baadae mauti ikazaliwa ( maana alimwua Uria). Kilichomwangusha Daudi ni “ tamaa” iliyokuwepo ndani ya uwezo wake.
Alipaswa kuishinda!!! Uzinzi ni dhambi ya ajabu sana,kuanza kwake hata kuisha kwake ni kwa ajabu ajabu tu,kwa maana ili uzini ni lazima mwanzie mbali,kitu ambacho unaweza ukakwepa mapema. Uzinzi hauji kwa gafula labda ubakwe! Lakini dhambi ya ajabu, dhambi hii ina mianya mingi ya kuikwepa ukilinganisha na dhambi nyingine. Uzinzi ni kama dhambi ya wizi,ambapo mwizi hawezi kwenda kuiba dukani mpaka kwanza apange njia zote kisha ndipo aibe! Na ndivyo dhambi ya uzinzi ulivyo!!!!
Kuna watu wakishazini utakuta wanasema “ shetani alinipitia…” kha! Jamani,huyo shetani kakupitiaje wakati tangu siku ya kwanza wewe mwenyewe kwa utashi wako unapanga namna gani utakwenda kuzini,tena na nyumba gani ya wageni utakwenda,tena na tshs ngapi utalipa, sasa shetani tena!!? Ni kweli ninakubali shetani yupo na ndiye chanzo kikuu,lakini wewe pia unahusika asilimia kubwa. Biblia inasemaje kwani?
“Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.“ Mwanzo 4:7
Kaini yule mwovu alipaswa aishinde dhambi ya kuua. Maana ilikuwa ndani ya uwezo wake, lakini hakutaka kwa moyo wake mbovu! Hata “tamaa ” ya ikakua na kuchukua mimba na hatimaye,dhambi ikazaliwa,na mwishoe mtoto aitwaye mauti / kifa akazaliwa,(kwa maana Kaini alimwua ndugu yake Habili)
Kwa nini ninakuambia “yapasa uishinde dhambi “? Ni kwa sababu Mungu ametupa nafasi ya upambanaji dhidi ya dhambi ya aina yoyote ile halafu ni Yeye ndiye anayetushindia kupitia Roho mtakatifu. Lakini nafasi aliyokupa huna budi kuonesha bidii,katika kuikataa na kuichukia dhambi hiyo,huku ukiwa umempa Yesu maisha yako akutawale Yeye. Na ushindi wa kila dhambi upo kwake katika Neno lake. Unapoketi vizuri katika Neno pamoja na maombi, hakuna tamaa itakayochukua mimba hata kuzaa dhambi.
Ebu fikiria hivi; ikiwa Neno la Bwana linakaa ndani ya moyo wa mtu, tamaa ikitaka kuota inajikuta inakosa nafasi ndani ya moyo,na badala yake inakosa matunda. Je mtu huyo ni lini ataweza kuangukia dhambini? Ukweli ni kwamba anaweza akafanya dhambi kwa maana ni mwanadamu,lakini zile dhambi zitokanazo na tamaa itakuwa ngumu kuzifanya. Ukiwa umeokoka,ujue Roho mtakatifu yupo ndani yako, na kuna nguvu ndani yako yakuishinda tamaa yenye kuzaa dhambi.
Bahati mbaya leo,wengine wamejikuta wakikiri kushindwa na dhambi halafu hawaoneshi jitihada yoyote ya kuchukia dhambi sana sana utakuta wakisema “ mimi nashindwa kuacha uzinzi” au “mimi sizewi kuacha dhambi hii,najitahidi lakini siwezi jamani… ” Ni kweli kuacha dhambi ni mtihani,lakini umechukua hatua gani? Je ni kweli umeichukia?
Tamaa izaayo dhambi,nyuma yake shetani yupo.
Mwangalie Adamu na Hawa watu waliopewa katazo la kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Biblia inasema “ Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.” Mwanzo 3:6
Lakini ukumbuke huo mti ulikuwepo hapo siku zote,lakini siku hiyo ambapo nyoka alipomgilibu akili Hawa,Hawa aliuona huo mti “watamanika” naye akachuma tunda kisha akala,na akampa mumewe naye akala!!! Tamaa aliyoipata gafla Hawa,ilikuwa na chanzo chake kwa maana mti huo ulikuwepo siku zote nao hakuona tamaa yoyote!!! nyoka/ibilisi alikuwa kazini kuhakikisha mwanamke anaingiwa na tamaa,na kisha tamaa izaye dhambi ya kuasi,na hatimaye mauti ipatikane kwao. Na kweli ibilisi alifahuru mpango wake Janja yake ibilisi ndio ile ile hata siku ya leo!!! Na dawa yake,ni kuzikimbia tamaa kwa kukaza kwa Bwana.Ni vyema ukajua kwamba, ikiwa kama upo kwenye tamaa ya aina yoyote, basi ujue dhambi ipo mlangoni na inakutamani,walakini wapasa uishinde.
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe. Na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900
Whatsapp namba .+255 746 446 446
Mch. G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments