WOKOVU NI TENDO LA KISHUJAA
- Mch. Gasper Madumla
- Apr 11, 2017
- 5 min read

Mch. Ezekiel Paul Bundala
Bwana Yesu asifiwe…
KWELI KUU: Wokovu ni kwa neema kwa njia ya imani katika Yesu Kristo Bwana na inahusisha hesabu kwa kuyahesabu yaliyofaida kwetu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo Yesu.
Wafilipi 3:8; Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;
UTANGULIZI: Wokovu ni tendo la kishujaa linalobadili mtindo wote wa maisha yako yote ikiwa ni pamoja na tabia na mwenendo wako. Kwa hiyo basi, maisha ya wokovu ni tendo la kishujaa linalohusisha kufa kwa nafsi yako na mwili wako ili roho yako (pamoja na nafsi yako) iishi kwa ajili ya Kristo, roho yako imuishi Kristo huku mwili wako ukiteketea juu ya madhabahu (ya mapenzi ya Mungu) kama dhabihu iliyo hai takatifu ya kumpendeza Mungu; na mwenye kuutoa mwili huo madhabahuni ili uwe dhabihu ni wewe kwa njia ya kujikana nafsi yako.
Katika kuishi maisha ya wokovu, mwili na roho huhusika kwa asilimia zote huku msukumo wa kila tendo ikiwa ni upendo wa Kristo ndani yetu ambao kiini chake ni Roho Mtakatifu ndani yetu tuaminio. Mambo yote yanayofanywa na mtu huyu aliyeookoka huanzia katika utu wake wa ndani (ambao ni roho yake moyoni mwake) na kumalizikia katika utu wake wa nje (ambao ni mwili wake). Kwa maana hii, wokovu hauishii ndani tu katika roho ya mtu, lakini pia unahusisha mwili wa mtu katika kutimiza mapenzi ya Mungu ambayo roho ya mtu imeyapokea kutoka kwa Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, katika swala la wokovu, ni lazima mwili na roho vikubaliane, viwe na nia moja, na mara zote lazima mwili ukubali kuacha mapenzi yake na kufuata mapenzi ya roho. Kwa moyo mtu huamini hata kuhesabiwa haki, na kwa kinywa mtu hukiri hata kupata wokovu.
MWILI NI NINI NA ROHO NI NINI: Ili tuweze kuelewana nitakapofikia katika kiini cha somo hili, ni muhimu tukaelewa dhana ya mwili na dhana ya roho katika maswala ya wokovu ambao tunaupata kwa neema kwa njia ya imani katika Kristo Yesu ambaye katika yeye huyo tunao ukombozi kamili.
Mwili ni utu wa nje wa mtu wakati roho ni utu wa ndani wa mtu na ndio mtu halisi. Mwili unaukomo katika ulimwengu wa mwili na wa roho pia, wakati roho haina ukomo inaishi milele. Mwili unayo nia na roho pia inayo nia; nia ya mwili hupingana na nia ya roho. Ili mwanadamu aishi maisha ya rohoni (ya kumpendeza Mungu) kwa sababu Mungu ni Roho na hao wamwabuduo imewapasa kumwabudu katika roho na kweli, ni sharti nia ya mwili ife ambayo ndio ndio utu wa kale, utu wa nje ili nia ya roho iwe na nguvu ya kutekeleza matakwa yake ambayo wakati wote (kwa mtu aliyeookoka) huzaliwa na mapenzi ya Mungu ambaye ni Roho.
Nia ya mwili na Nia ya roho: Kwanza ni lazima tutambue kuwa mwili ni wa dunia hii wakati roho si ya dunia hii, ni ya mbinguni. Kwa kuwa mwili ni wa dunia hii una nguvu zaidi ukiwa duniani na kwa sababu hiyo wakati wote (usipokufa) hutafuta kuyatenda mapenzi ya dunia hii. Kama vile samaki au nyangumi au mamba anapokuwa na nguvu zaidi awapo majini isipokuwa amekufa, ndivyo ulivyo mwili katika dunia hii, una nguvu isipokuwa umekufa. Kwa kuwa roho si ya dunia hii, daima yenyewe hutafuta kuyatenda mapenzi ya Mungu (ambaye ni Baba yetu wa mbinguni). Lakini, kwa kuwa mwili na roho ya mtu aliye hai viko duniani, kama nia ya mwili (ambayo ni uadui juu ya Mungu) haitakufa ili kuipa nafasi roho iishi katika mapenzi ya Mungu, mwili utaiponza roho kwa kusababisha mauti ya roho ya milele ambayo ni mauti ya pili (Jehanamu ya milele). Kwa hiyo ni sharti nia ya mwili ambayo siku zote hutenda mapenzi ya dunia hii, ambayo ni mapenzi ya mwili ife ili roho iishi katika kutekeleza na kutenda mapenzi ya Mungu.
Nia ya mwili ni mauti; mambo ya dunia hii yaletayo mauti ambayo wakati wote hayatokani na Mungu. Na chochote kisichotokana na Mungu ni kinyume na Mungu, kinapingana na Mungu. Nia ya mwili (mawazo yanayotokana na matamanio ya mwili katika mambo yale mwili unataka kutekeleza au kutekelezewa, kufanya au kufanyiwa) hupelekea msukumo wa mwili kutenda matendo ya mwili badala ya matendo ya Roho. Matendo ya mwili ambayo huzaliwa na nia ya mwili huonekana kwa watu ambao hawaongozwi na Roho Mtakatifu, ambao hawajatawaliwa na Roho Mtakatifu na ambao hawaenendi kwa Roho, kwa kufuata na kutii maongzi ya Roho wa Mungu.
Warumi 8:5 – 11; Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho. Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na aamani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kutii (sio tu haitii, bali haina uwezo wa kutii, haiwezi kabisa kutii). Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ikiwa Roho wa Mungu, anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali Roho yenu i hai, kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa Roho wake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.
Wagalatia 5:16 – 21; “Basi nasema, enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili, kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati uchafu ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.”
Nia ya mwili huua mapenzi ya Mungu, lakini pia huua ushirika wa mtu na Mungu kwa kuitenga roho ya mtu na Mungu. Kwa hiyo, kama mtu anataka kuishi maisha ya wokovu, ni lazima afanye tendo la kishujaa la kukubali kuua mwili wake kwa habari ya mambo ya dunia hii ili roho na mwili wake viishi kwa ajili ya Kristo Yesu.
Wakolosai 3:5 Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu.
Katika somo lijalo, tutaangalia gharama ya kuishi maisha ya wokovu kwa kila mwamini katika kujitenga na dunia ili kuishi kwa ajili ya Kristo. Ikumbukwe kuwa maisha ya wokovu ni maisha ya gharama, ijapokuwa tunapokea kwa neema na tunawezesha kwa neema kwa njia ya imani katika Kristo Yesu bado kuna kipengele cha sisi wenyewe kuchukua hatua madhubuti za kujikana na kuhesabu yaliyo faida kwetu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo, na hili mimi nimeliita ni tendo la kishujaa. Mtume Paulo akiwaandikia watakatifu wote pamoja na maaskofu na mashemasi wa kanisa la Filipi, anasema, “Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake” (Wafilipi 1:29). Wokovu ni imani katika Yesu Kristo, lakini pia ni mateso kwa ajili ya Yesu Kristo. Mtu anapoamua wokovu wa kweli maana yake ameamua kutenda tendo la kishujaa kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
Mungu akubariki,
Na, Mch. Ezekiel Paul Bundala 0693 212 044
Comments