top of page

WITO WA MUSA.

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi:

Lengo kuu la ujumbe huu,ni kuangazia namna ambavyo Bwana alivyomtuma Musa kazi ya kurejea Misri na kuwatoa Waisraeli,akianzia kwanza kumwendea Farao. Hata hivyo haikuwa rahisi kwa Musa maana alikimbia kutoka Misri. Ujumbe huu,unafanana na maisha yako binafsi vile ambavyo Bwana anakutumia.

Kila mtumishi wa Mungu ameitwa tofauti na mtu mwingine. Ukisoma habari za wito wa Paulo utagundua ulikuwa tofauti na wa Daudi, kwa maana Daudi aliitwa kutoka katika uchungaji wa kondoo akiwa mdogo kabisa,wakati Paulo yeye aliitwa kutoka kwenye uuaji na ukatili dhidi ya watu wa Mungu naye akatumwa kwa mataifa. Utofauti wa wito upo kwenye kusudi walilobeba.

Musa naye alikuwa mtu mzima alikataa kuitwa mtoto wa binti Farao,akakimbia kutoka kwa Farao( Waebrania 11:24-25). Alimwua Mmisri akidhani ya kwamba ndugu zake watafahamu ya kuwa Mungu anawapa wokovu kwa mkono wake,yeye alifikiri hivyo ( Matendo 7:25).Akakimbilia Midiani,akiwa huko- Bwana akamtengenezea mazingira mazuri ili apate kusema naye,Bwana akamfanyia maajabu ya kichaka kuwaka pasipo kuteketea kwa lengo la kupitisha kile alichotaka Bwana ( Kutoka 3:2). Bwana akasema naye na akamtuma arudi Misri ili awatoe watu wa Mungu utumwani. Kwa kuwa Bwana alimfahamu vizuri Musa,ilimbidi amtengeneze imani yake kwanza kwa kumfanyia ishara nyingi.

Hata hivyo Musa ilifika wakati akawa haelewi somo,akamwuuliza Mungu “ …hawataniamini wala hawatanisikia sauti yangu,maana watasema Bwana hakukutokea” Kutoka 4:1. Bwana akamfanyia tena ishara,ili angalau amfanye kuamini lakini hata hivyo Musa bado alisita sita. Ukumbuke ya kwamba mwenye haki hapaswi kusita sita kwa maana akisita sita Bwana hawezi kuwa na furaha naye ( Waebrania 10:38). Biblia inasema;

“Musa akamwambia BWANA Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito.BWANA akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, BWANA? ” Kutoka 4:10-11

Ni ukweli Musa alikuwa mzito katika usemi,naye alisema kweli wala hakudanganya,Ingawa kwenye Matendo 7:22,Biblia inasema kuwa Musa alifundishwa hekima yote ya Wamisri, akawa “hodari wa maneno na matendo.” Hii ina maana kwamba alikuwa mzito kuongea labda alikuwa na kigugumizi katika usemi,lakini alikuwa hodari/mwerevu katika hekima/taratibu za kimisri. Alikuwa hodari wa maneno na matendo ya kimisri lakini sio hodari wa Neno la Mungu alilokuwa akitumwa kwalo,kwa maana neno lile hakulisomea popote ukilinganisha na ustaarabu alisomea.

  1. Kujitetea / kulalamika kwa Musa kunaweza kukatafsiriwa hivi;

01. Kutojiamini na hali ya hofu juu ya Farao./Kukosa imani.

Musa alikuwa akijua mwenendo na tabia ya Farao,ubaya na ukatili aliokuwa nao Farao Musa aliujua. ( maana amekaa na Farao muda wa miaka 40 akijifunza elimu na ustaarabu wa kimisri.),Hakika Musa anamjua Farao ni mtu wa namna gani ( ingawa Farao yule wa kwanza alikwisha kufa,lakini hata Farao aliyekuja alikuwa akifanana na Farao aliyepita ).Farao alikuwa ni mungu mtu,anapewa heshima zote . Hivyo anapomwangalia Farao kifikra na kujilinganisha uwezo aliokuwa nao,anajiona hawezi kabisa hata akatengeneza sababu za kukataa anachotumwa.

Wakati mwingine unapoyaangalia mazingira yako ya kwanza, unajikuta ukiishiwa nguvu na kujiona huwezi kurudi huko na kufanya kitu,maana hawatakuelewa. Ukiwa na hofu juu yao,juu ya chochote ni lazima utajikuta ukisema “ mimi siwezi ” kitu ambacho hutakiwi kuwa nacho,bali amini kwamba unaweza katika Kristo anayekutia nguvu.

02. Kunyenyekea

Kitendo cha Musa kubeba agizo la Mungu, na kupeleka kwa Farao kinatafsiriwa kuwa ni kitendo kikubwa sana. Musa anapojiangalia na kujiona kuwa si msemaji mzuri,anatamani hata apatikane mtu mwingine atakayesema vizuri zaidi naye awe chini ya mtu huyo. Ni kama vile leo,uambiwe wewe ni mchungaji, hali ukijijua huna uwezo huo,basi ni rahisi kukataa na kusema “ mimi bado bhana!” ukiona kwamba sio jambo jepesi hata kidogo.

Hata hivyo, kitendo hiki hakikumpendeza Bwana. Naye BWANA akamwambia, “Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, BWANA?“. Katika mstari/andiko hili,tunaona mambo mawili muhimu yakitajwa na Bwana.

01) “Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu.?”

Jibu la swali hili linatueleza kuwa ni Mungu ndiye aliyekifanya kinywa cha mwanadamu. Neno “ aliyekifanya” hueleza tendo lililokamilika kufanywa,kwa mfano tuna vinywa kwa sababu tayari vilikwisha fanywa,tuna macho kwa sababu vilikwisha fanywa,tuna masikio kwa sababu tayari vilikwisha fanywa n.k. Kile tulichonacho leo kwenye miili yetu,kimeumbwa na Mungu kwa ajili yake/kwa matumizi yake. Hivyo,mtu kama ni bubu,Mungu atukuzwe katika huo ububu wake,kama kiziwi Mungu atukuzwe na kiziwi cha mtu. N.k

Hii ina maana vile ulivyoumbwa ni matokeo ya kazi ya Bwana, naye anajivunia jinsi ulivyo akijua hivyo hivyo utamtumikia Yeye naye atatukuzwa katika wewe. Musa anapotumwa na Bwana, Bwana alikuwa akimjua vyema na alikuwa pia akiwaona wengine lakini hao wengine hawakukusudiwa. Fikiria, ukiwa ni mlemavu wa miguu,kisha Bwana Mungu anakutuma akikwambia wewe ndio utakaowaongoza watu wake. Hapo wewe hutakiwi kuwa na wasi wasi kukataa,kwa maana ni Yeye aliyekuumba hivyo,na ni Yeye ndiye anayekutuma,hivyo anajua Yeye,wewe ni kusimama na kwenda mbele.

02)“ni nani afanyaye mtu“

Neno “afanyae “ ni tofauti na neno “aliyekifanya ” kwa maana “afanyaye” hueleza kitendo endelevu katika kile kilichofanywa tayari. Mfano leo tunakinywa kilichofanywa tayari, lakini katika hicho Mungu bado anafanya kitu endelevu kwa kutuwezesha kuongea. Tunaongea leo,kwa sababu Mungu ndiye “afanyaye ” tuongee. Hii ina maana ingawa tuna vinywa lakini bado Mungu ndiye anayetuwezesha kuongea. Ikiwa ndivyo,basi hakuna cha kujivunia kwa kile tulichonacho.!!!

Musa alikuwa amepewa namna yake ya kuongea, kwa kusudi maalumu la Mungu. Na Bwana Mungu anamtaka amtumie vile vile alivyo,lakini Musa haelewi kwamba namna alivyo ndivyo Mungu hujivunia. Hata leo,anachofanya ujue umewezeshwa na Bwana si kwa uwezo wako mwenyewe. Lakini inawezekana ukawa una ulemavu fulani, usihofu hapo! Mungu anataka utumike katika ulemavu wako huo huo,ili kupitia huo umpe Mungu utukufu. Ukumbuke Mungu huvichagua vinyonge aviaibishe vyenye nguvu.

Ikiwa umebarikwa,nifahamishe. Kwa msaada zaidi na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900

Whatsapp namba .+255 746 446 446

Na Mch.G.Madumla

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page