top of page

WALINZI JUU YA KUTA ZAKO ~ 03.

Bwana Yesu asifiwe…

Isaya 62:6-8…. Moja ya sifa ya mlinzi ni kutokunyamaza usiku wala mchana;yaani kutokutulia hata mambo yawe sawa. Neno hili “ walinzi juu ya kuta zako” linatoa picha ya mji uliozungukwa kwa uzio pamoja na walinzi waliojipanga juu ya huo uzio. “ mji” unaweza kuwakilisha familia, ukoo,au mji kama kama mji. Lakini kumbe mji unapaswa kuwa na walinzi ambao kazi yao ni kulinda mali pamoja na kuulinda mji dhidi ya uvamizi wa aina yoyote. Hivyo aina nyingine ya ulinzi ni, damu ya Yesu. Ambayo inafanya kazi kubwa sana ya kulinda dhidi ya roho za giza. “Neno la Mungu” kama chanzo cha maarifa ya Mungu ni silaha, na ni ulinzi mkubwa sana kwako.

  1. Mambo muhimu kujua.

Kila kinacholindwa kina thamani ndio maana kinalindwa. Ikiwa kama wewe unalindwa na nguvu ya Mungu, basi wewe u wa thamani. Lakini hata hivyo shetani amepofusha akili za watu wengi ( 2 Wakorintho 4:4); ambao hudhani kuwa wanalindwa na dawa za waganga. Ukweli ni kwamba mganga wa jadi hana uwezo wa kukulinda wewe, ila ana uwezo wa kukudanganya tu!

01. Hila za shetani.

Ebu fikiria upo barabarani unaendesha kurudi nyumbani. Na unafika sehemu fulani na unakutana na mtu usiyemfahamu na gafla anakusimamisha na kukuomba lifti. Ile kumwangalia ni nani huyo, unamwona mdada wa kawaida kabisa anakwambia “naomba lifti ” kwa kuwa ni binti, unamwonea huruma kwa mazingira aliyopo na labda ni usiku. Kisha unamwuuliza una kwenda wapi muda huu? Kisha baada ya kukwambia anakoenda,basi unamchukua na safari inaendelea. Katikati ya safari unahisi hali tofauti, jini si jini, pepo si pepo, yaani uelewi elewi!! 😎😎😎

Kisha anakwambia “niache pale mbele” na kwa sababu ya kupata wasiwasi unaombea rohoni kumwacha popote pale. Alafu gafla unajikuta ukisema “kwa jina la Yesu tokaaa” ( maaana unaogopa kusema shetani toka kwenye gari yangu, angekuuliza nani shetani!) na gafla unacheki nyuma ya siti aliyokaa, na huoni mtu yeyote tena wala hujamshusha maana bado mlikuwa katika mwendo kasi. Alafu kuangalia vizuri unaona kikaratasi kilichoandikwa jina lako kamili, na vitu vya ajabu ajabu kwenye kifuko.

Na hapo unaanza kutafakari, hivi ingelikuwaje kama ungemfikisha kule atakako? Mbona mwanzo wa kuomba lifti alikuwa mkarimu, mcheshi na kuonesha kweli anahitaji msaada? Na hapo ndipo unapoona kwamba ilikuwa ni hila. Kulikuwa na mpango mbaya juu yako, lakini Bwana amekusaidia. Mfano huu unaonesha jinsi gani hila inavyofanana, kwa maana si rahisi kutambua hila. Wakati mwingine unaweza kuona jambo kana kwamba ni jema lakini kumbe si hivyo uonavyo, kuna hila ya kukuua.

Hili ni jambo la kwanza kujua kwamba kuna shetani na hila zake. “Hila” ni njama za udanganyifu, uhalibifu.Kawaida mtu anayefikiri kutafuta walinzi ni yule aliyeona hasara inayoweza kumpata, au kuja. Mtu atakapogundua kwamba anaweza kupata hasara basi kitakachofuata ni kufanya mikakati ya kuikabili hiyo hasara. Njama za shetani ni moja ya mpango wa kuleta hasara kwenye maisha yako! Hivyo ni vyema ukatambua hila za shetani, ili ujipange kuzikabili/kuzipinga.

Kama hautatambua hila za shetani, basi ni dhahili hautamaanisha kuwa na mikakati ya kuzipinga. Kama mlinzi ambaye kazi yake sio kulinda tu, bali na kushambulia pia nawe unapaswa kujifunza kujua kulinda na kushumbulia hila za adui. Mfano wa mambo ambayo shetani ujaribu kushambulia ni kama vile “maono, malengo yako, huduma, afya, mafanikio kwa ujumla, masomo, kazi n. K.

Ni vyema utambue kama utakuwa umetegwa kwenye eneo lolote ili uanguke,. Hapo si rahisi kugundua mtengo wa adui yako kwa kutumia akili zako binafsi. Utaweza kugundua mitengo / hila kwa msaada tu wa Roho mtakatifu. Katika Yeye hakuna jambo litakalojificha likafichika, kila kitu kipo wazi kwake. ( utahitaji kujifunza kiundani namna ya kumtumia Roho mtakatifu kupitia hapa hapa) Lakini kwa habari ya mipango ya shetani

Biblia imeweka wazi jambo hili, maana inasema; “ Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.“ Waefeso 6:10-11 Kile kinachoelezwa hapa ni “mtu kukaza kwa Bwana “ na Katika uweza wa nguvu zake. Hii ina maana unapokuwa na bidii bila kuchoka katika Bwana, Bwana atapigana badala yako. Lakini lengo mama hapa ni kukuonesha kwamba ziko hila, sasa ili ufanikiwe kuzitambua unahitaji jambo moja ambalo ni“uwe hodari katika Bwana “

Kumbuka ; mlinzi ili awe mlinzi anahitaji mambo mawili makubwa“ujuzi au maarifa na silaha”. Katika mstari huu, mambo hayo yanatajwa kwamba uwe hodari katika Bwana ( eneo la kuwa na maarifa ya kiungu) pamoja na kuvaa silaha zote za Mungu. Kazi kubwa za silaha za Mungu ni kuzipinga hila za shetani, kumbuka hilo. Katika mstari huu, utagundua kwamba bila silaha zote za Mungu huwezi kuzipinga hila za shetani. Neno “ silaha zote za Mungu ” linakutazamisha kuwa zipo silaha za Mungu,ambazo wewe unatakiwa uzivae kwa maelekezo stahiki.

Ningelikuwa ninaongea na mtu ambaye ni mwanajeshi au mtu aliyewahi japo kwenda jeshini, nadhani angenielewa zaidi. Tunapozungumzia suala la silaha, tunazungumzia aina mbili za silaha “ silaha za kujiami/ kujilinda na silaha za kushambulia”. Makundi yote ya silaha haya yameelezwa kwenye Waefeso 6:10 na kuendelea. Lakini ni kwa ajili ya kupambana na hila za shetani katika ulimwengu wa roho…

ITAENDELEA…

Ikiwa unahitaji kuzungumza nami juu ya kile unachopitia kwa mfano wa hila nipigie tu. Kwa msaada zaidi pamoja na maombezi, piga sasa +255 683 877 900

What’s namba+255 746 446 446 .

Mch. G. Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page