top of page

WALINZI JUU YA KUTA ZAKO ~ 02

Yerusalem


 Bwana Yesu asifiwe…

…lakini bado wema wa Bwana umekuzunguka..

“ Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani.“ Isaya 62:6-7

Biblia inasema Bwana ameweka walinzi juu ya kuta za Yerusalemu. Na sio Yerusalemu imeweka walinzi; kwa maana kuna tofauti kati ya “Bwana mwenyewe kuweka walinzi ” na “ Yerusalemu kuweka walinzi “. Sentensi hii inatueleza kwamba wajibu wa walinzi hao upo mikononi mwa Bwana kwa sababu ndiye aliyewaweka,wala sio Yerusalemu. Kama ingelikuwa walinzi wanastahili posho,basi ni Bwana ndiye anayetakiwa kuwajibika na sio Yerusalemu. Bila shaka walinzi hawa walikuwa mali ya Bwana. Biblia haituelezi kiundani ni walinzi wa namna gani wanaozungumziwa hapo. Lakini kile tunachoweza kujua kwa haraka ni kwamba;Bwana mwenyewe alikuwa mlizi juu ya kuta za Yerusalemu kuonesha tu,ni kwa namna gani Bwana aliuangalia/ aliujali mji wake. Hivyo hilo ni kundi la kwanza la walinzi juu ya kuta zako.

Neno “Yerusalemu” lilikuwa linawakilisha “mji ” kama miji mingine ya kawaida. Na katika kipindi hicho,Yerusalemu ulikuwa mji uliokuwa ukiwa / haukuwa na maana sana. Kwa sababu tunaona kile kinachoelezwa kwenye andiko hilo hilo,anasema“… mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani.” hii ina maana ulikuwa ni mji usioimarika,uliokosa sifa duniani.

02. Mtu wa Mungu ni mlinzi.

Katika andiko hilo hilo,imeandikwa “…; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya;...” hawa wanaozungumziwa hapo kwamba “wasikae kimya” sio malaika,bali ni watu halisi wa Mungu.“ Waombaji ” ndio kundi la watu wanaozungumziwa hapo,ambao tunaona wamepewa nafasi ya kumkumbusha Bwana hata Yerusalemu ukae sawa. Kwa historia fupi tu kuhusu mji wa Yerusalemu ni kwamba; ulikuwa na maadui wengi waliouhusuru,na waliouvamia kwa nyakati tofauti tofauti ( Nehemia 1:2-3).

Katika picha hiyo,yeyote atakayesimama kuomba ulinzi wa Yerusalemu kama mji, kile atakachokuwa akifanya kina maana ya kuulinda mji kimaombi,na tafsiri ya mtu anayelinda mji,mali au fedha huitwa“ mlinzi “. Hivyo mtu wa Mungu ni mlinzi eneo alipo. Mbali na ulinzi wa kutumia panga,bali ulinzi wa kutumia panga ya Roho mtakatifu kwa njia ya maombi.

Maana ya neno “Yerusalemu ” imepanuka zaidi. Kwa maana Yerusalemu inaweza kuwakilisha “mtu binafsi,mbingu mpya na nchi mpya n.k” lakini kitu muhimu kujua ni kwamba, mtu aliyeokoka ni mlinzi juu ya mahali alipo,au juu ya watu aliopewa na Bwana. Ebu fikiria kwamba, wewe umeokoka na uko na Bwana amekupa familia. Je ni nani awe mlinzi wa kiroho wa familia hiyo? Je mchungaji wako? Je kanisa lako? Au je pesa zako? Hapana!! Ni wewe ndiye haswa mlinzi unatakiwa kuwa kwa njia ya kuomba.

03. Walinzi wa kipepo.

(Kumbuka maana hasa ya “kulinda”. ) . Kuna kundi kubwa la mapepo linalofanya kukuzuia kwa ulinzi waliouweka wao. Ni kana kwamba unawekwa kizuizini huku walinzi wa kipepo mbele na nyuma usije ukatoka. Mara nyingi kama umezuliwa utajikuta upo pale pale,na huwezi kutoka hapo mpaka washughulikiwe hao walinzi.

Si wengi wanalifahamu jambo hili,kwa maana ni siri kubwa katika ulimwengu wa kiroho. Walinzi ndio wakati mwingine huzuia waamini kuja kanisani,hasa hasa kuzuia maombi yako. Wakati mwingine unaweza kuwaza kwamba “mbona kana kwamba sipokei niombapo,bora niache tu...”

“ Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi.“ Danieli 10:12-13

Danieli anasimulia maono aliyoyapokea,na ilikuwa ni vita kubwa ya kiroho kama jinsi ilivyo leo. Danieli alikuwa na maombi mazito ya siku 21 na hapo ndipo alipofunuliwa neno na Bwana. Bwana anamwambia kwamba tangu siku ya kwanza ya kuomba kwake,Bwana alisikia maombi hayo.

Lakini yeye Danieli hakujua hiyo;kwa sababu kulikuwa na jambo lisilo la kawaida lililokuwa likiendelea katika ulimwengu wa roho. Bwana anasema “mkuu wa ufalme wa Uajemi alimpinga siku zote za maombi yake siku 21” unfikiri ni nani huyo anayeitwa mkuu wa ufalme wa Uajemi?. Je alikuwa akifanya kazi gani ? Bila shaka ni roho/ibilisi/pepo ndiye aliyekuwa akiitwa mkuu wa ufalme wa Uajemi aliyekuwa akimpinga Bwana katika kupeleka majibu ya maombi ya Danieli.

Kazi yake huyo mkuu,ilikuwa ni kupinga / kuzuia na kumkatisha tamaa Danieli alipokuwa akiomba. Biblia inapanua wigo kueleza kwamba kuna “wakuu wa anga” Waefeso 2:2 & Waefeso 6:12. Hawa na wenyewe huitwa walinzi wa kipepo.

Kama vile mambo yalivyokuwa katika siku za Danieli ndivyo yalivyo katika siku hizi. Wakuu wa giza wapo,wachawi pia wapo. Kazi yao kuharibu,kuua,kuchinja pamoja na kuzuia (Yoh.10:10)…

ITAENDELEA…

Kwa msaada zaidi,pamoja na maombi nipigie sasa kwa +255 683 877 900/

Na Mch. G.Madumla.

What’s app +255 746 446 446

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page