UTIMILIFU WA UNABII – 3
- Mch. Gasper Madumla
- Mar 14, 2018
- 2 min read
Updated: Sep 5, 2022

Na Mch Gasper Madumla.
“Utimilifu wa unabii wa Isaya uliotimizwa katika Kristo ‘‘
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi.
Kumbuka,nabii Isaya ni mmoja kati ya manabii wakubwa wanaoelezwa kwenye biblia. Ukiulizwa leo utaje vitabu vitatu vya manabii wakubwa,basi ujue kimojawapo ni Isaya kutokana na sehemu kubwa ya unabii alioutoa Isaya. Hivyo utagundua kwamba zipo nabii nyingi alizozitoa nabii Isaya nazo zimetimia,lakini leo nataka nikutazamishe nabii kubwa tatu miongoni mwa nabii nyingi zilizotimia. ( Haina maana kwamba nabii nyingine ni ndogo,hapana! Lakini katika nabii hizo nimechukua tatu tu kwa kujifunza )
01. Bikira kuchukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume,mtoto ataitwa Imanueli. ( Isaya 7:14)
Miaka mingi ilikwisha tabiriwa kwamba bikira atachukua mimba kwa (uweza wa Roho mtakatifu) naye mtoto atakaye zaliwa ataitwa Imanueli . Unabii huu tunauona utimilifu wake ( Mathayo 1:18-23,24-25). Mungu alimchagua Mariamu mwanamke wa kawaida kabisa kwenye familia ya chini,tena msichana mdogo bikira,lakini uzuri wa Mariamu alikuwa mwanamke aliyejitunza katika usafi wa kiroho,mtakatifu kwa ajili ya kumbeba mkombozi Yesu. Unabii wa Isaya ulikuwa ukingojwa lakini umetimia,mwokozi amezaliwa.
Kuzaliwa kwa Yesu kumefanyika mara moja tu,na hakuna kuzaliwa tena kwa mwokozi. Leo hii ni wewe unapaswa uzaliwe upya kwa roho ndani yake na uendelee kumuishia ili uwe mbali na hukumu ya jehanamu ya moto. Bwana Mungu alifanya kazi kubwa sana na nabii Isaya kuhakikisha kwamba unabii huu mkubwa unatimia. Haikuwa rahisi kwa unabii kama huu,lakini kwa sababu Mungu alikuwa na mpango na watu wake,akamtuma mwanaye ili kila mtu atakaye muamini na kumpokea Yesu awe na uzima wa milele ( Yohana 3:16)
02. Yesu atafanya huduma yake haswa Galilaya ( Isaya 9:1-2)
Kumbuka ; katika kipindi cha agano la kale,Galilaya ilikuwa nchi (ardhi) ya kabila la Naftali ( Joshua 20:7) na mengine mengi. Lakini kwenye agano jipya Galilaya ilikuwa ni wilaya iliyoongozwa na Herode. Ndani ya Galilaya kama wilaya ilikuwa na miji muhimu minne kama vile Nazareth,Kapernaumu,Kana ya galilaya,na Bethsaida.
Hivyo Isaya alitoa unabii kwenye agano la kale,kwamba Yesu ataanzisha huduma akitoa nuru,Nuru imewaangazia. Isaya alikuwa akizungumza Yesu kuwa ni Nuru itakayowazukia galilaya na sehemu nyingine. Na ndio maana Yesu alifanya huduma yake sana ndani ya Galilaya ( hususani Kapernaumu). Huduma kubwa ya Yesu ilikuwa huko. Yesu mwenyewe anaitwa Yesu Kristo wa Nazareth.
03. Yesu kubeba magonjwa yetu/ kutuponya ( Isaya 53:3-5)
Isaya alitoa unabii juu ya Yesu kwamba,atachubuliwa,atadhauriwa kwa ajili yetu, Yesu atachukua masikitiko yetu,atapigwa na damu yake itamtoka kwa ajili yetu,kwa kupigwa kwake wewe na mimi tumepona. Kipindi Isaya anayasema haya kilikuwa ni kipindi cha agano la kale,( ingawa Yesu alikuwepo kabla ya kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu kwa jina la Neno.) Unabii huu umetimia maana ndiye Yesu aliyeshughulikia magonjwa yetu yote pale msalabani.
Kumbe,kila kitu alichokifanya Yesu kilikuwa kwenye mpangilio na mpango wa Mungu na ndio maana Mungu aliandaa njia mapema katika utaratibu mzuri unaofaa. Ili wewe na mimi tuweze kuamini kwamba Yesu hakujifanyia mambo yake bali yale aliyotumwa na Baba maana uungu wote wa Baba upo ndani yake.
Hata leo Je tunaishi kwenye nabii hizo?
Jibu,ni ndio. Leo tunapaswa kuweka imani zetu kwake Yesu,maana ikiwa tutakuwa nje yake au kinyume ujue tutaangamia na kutembea kwenye laana kwa sababu neno lake li halisi halijaabadilika wala kamwe hakitabadilika. Jambo moja muhimu unalopaswa kujua leo,ni kwamba “ kila kilichoandikwa ni lazima kitimie“…
Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900
Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments