top of page

MTU MPOLE ZAIDI YA WANADAMU WOTE.

Updated: Aug 30, 2022


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi,


Pamoja na kuwa na watumishi wa Mungu wengi waliopita na watumishi mbali mbali wa kizazi kipya, lakini kuna Mtumishi mmoja amepewa sifa ya kipekee ya kuwa mtu mpole zaidi ya wanadamu wote. Kwa mujibu wa biblia,inamtaja kuwa “ Musa” ndiye haswa alikuwa ni mtu mpole zaidi ya wote. Imeandikwa;


Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi.” Hesabu 12:3


Najaribu kufikiria tu, hivi huyu Musa alikuwa ni mtu wa namna gani katika nyumba ya Mungu kwa maana hata mpango wake wa wokovu katika nyumba ya Israeli kipindi cha agano la kale unafananishwa na mpango wa wokovu wa Yesu Kristo katika agano jipya. Maana torati ilitolewa kwa mkono wa Musa,Neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo ( You.1:17).


  • Lakini Yesu naye alikuwa ni mpole na mnyenyekevu wa moyo ( Mathayo 11:29) Hii inaonesha wazi kabisa kulikuwa na kushabiana kitabia kati ya Musa na Yesu Kristo. Pamoja na hayo Yesu alikuwa Bora ya Musa maana alikuwepo kabla ya Musa kuwepo. 


Upole wa Musa ndiyo ulikuwa nguvu


 Tukimzungumzia Musa tunaona upole wake ndio ilikuwa nguvu yake kuu ya kutembea katika kusudi. Kwa maana upole wake ndiyo “unyenyekevu mbele za Mungu ” He was a very humble man, na Kwa sababu hiyo tu,ilimfanya awe na ukaribu/ ushirika na Mungu kiasi kwamba Bwana alikuwa akinena naye mdomo kwa mdomo yaani waziwazi bila mafumbo. Tana ndiye alikuwa mtu mwaminifu sana katika nyumba ya Mungu yote ( Hesabu 12:7-8)

Pamoja na kwamba yeye Musa alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, lakini alikuwa na kitu tofauti cha unyenyekevu uliotafsiriwa kama upole zaidi ya wanadamu wote. Mungu alionekana sana Kwa Musa katika upole wake,na hapo ndipo nguvu zake Musa zinaonekana.


Laiti kama tungeliweza kuondoa kipengele cha upole wake,basi Musa angelikuwa wa kawaida. Tunaweza kujifunza kitu hapo, kwamba Kumbe Kila mtumishi aliyeitwa na Bwana kuna sehemu ya nguvu zake zinazomsogeza katika kusudi la wito huo.


Na kawaida ya nguvu inayoweza kukusimamisha ni lazima ijaribiwe katika moto,ili kupima uwezo wake wa kustahimili kusudi ulilobeba. Ukicheki namna ambavyo Musa akijaribiwa, utagundua kwamba kilichokuwa kinajaribiwa ni kimoja tu,“ upole na unyenyekevu wake

Kwa maana mara nyingi watu aliokuwa akiwaongoza walikuwa wakitenda dhambi,kiasi kwamba yeye hushuka na kupomoka mbele za Bwana Kwa kuwaombea rehema hata ilifika wakati aliona bora afutwe yeye kwenye kitabu cha uzima  lakini Mungu asiwaangamize na kuwafuta Israeli ( Kutoka 32:32) .


Hii ni tabia ya upole uliochanganyikana na huruma ya namna ambayo hakuna mtumishi alivyokuwa nayo isipokuwa Yesu pekee yake.


Kumbuka!


Upole ni kinyume cha kiburi,hivyo kama Musa alikuwa mpole basi ni sawa na kusema alikuwa hana kiburi ndani yake. Na tunaweza kuthibitisha hili pale tunapomwona Musa akitumwa na Bwana akajioneshe kwa Farao,wakati wote alisema “ Bwana,Mungu wa Israeli asema hivi...” Mtu mwenye kiburi atasema “ Mimi nasema hivi…

Tofauti hapo ni moja,Musa alijua Neno alilopewa ni la Bwana sio la kwake,hivyo hata katika uwasilishaji alimtanguliza Bwana kwamba ndiye mwenye hilo Neno. Hakutaka kujionesha kwamba Neno ni la kwake, tabia hii inaonesha hali ya upole wake na unyenyekevu mkubwa sana.


Ukweli ni kwamba “unyenyekevu” ni nguvu ya utumishi. Kwa maana ikiwa unahitaji kuwa na ushirika mkubwa na Bwana kiasi cha kisikia sauti yake kama ilivyokuwa kwa Musa huna budi kunyenyekea zaidi,na hapo Bwana atakuinua. Kama utafuatilizia maisha ya Musa utagundua kwamba alikuwa aliyeinuliwa kwa kusudi kubwa.


Mtu aliyetoka katika familia ya kawaida sana tena familia isiyokuwa na utajiri wala Mali,maana hatuoni popote kwamba mzee wake alikuwa na mifugo,au fedha,au dhahabu isipokuwa kile ambacho mzee wake alichokuwa nacho ni kutoka katika kabila la Lawi.

Ikiwa kama ni kabila la Lawi basi tunapata picha ya mambo ya ibada yalikuwa kipaumbelee chao na Mungu akaichagua familia ambayo ilimpa nafasi ya kwanza,Kwa hiyo akamwinua Musa kutoka huko. Na bila shaka hata kabla ya Musa kuwa Musa Mungu aliuona moyo wake na akaona upole na unyenyekevu,tena akapendezwa nao.


Inawezekana kabisa kulikuwa na mbegu ya upole na unyenyekevu iliyokuwa ndani yake angali alipokuwa katoto kachanga,na mbegu hii ikawa nguvu yake hapo baadae.


Kumbuka ;


Upole wa Musa unaelezea pia ile namna ya kutegemea Mungu katika hali zote. Na hali hiyo inatafsiriwa kama Imani thabiti alivyokuwa nayo Musa. Tena Bwana huwainua watu wapole na wanyenyekevu hivyo,jifunze kuwa na upole na unyenyekevu,na hapo utaziona nguvu za Mungu kwa kiasi kikubwa mno.


Ikiwa umebarikiwa nifahamishe, pia Kwa msaada zaidi piga + 255 683 877 900.


What’s app number ni +255 746 446 446.


Na Mch. G. Madumla.


UBARIKIWE

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page