UTII WA IBRAHIMU
- Mch. Gasper Madumla
- Jul 26, 2015
- 3 min read

Tunayo mambo mengi ya kujifunza pindi tusomapo habari za Ibrahimu baba yetu wa imani (Warumi 4:16),lakini kubwa la kujifunza ni imani kuu aliyokuwa nayo. Katika imani tunajifunza “utii ” uliompendeza Mungu.
Bwana Yesu asifiwe….
Kwa ufupi,
Kwa maana Mungu alipomwita Ibrahimu na kumwambia atoke katika nchi yake na kuelekea mahali asipopajua, biblia inasema Ibrahimu “ aliitika” kitendo cha kuitika kinaonesha hali ya utii wa sauti ya Mungu.
Kuinuliwa kwa Ibrahimu kulitegemea imani na utii aliokuwa nao. Ibrahimu alikuwa na neema ya tofauti,kwa neema hiyo alifanikiwa kutofautisha kati ya sauti ya “ sauti ya Bwana” na sauti ya shetani na ya ,mwanadamu . Hivyo wakati Bwana Mungu alipozungumza naye,alijua hakika ni Mungu. Lakini ukitafakari shida inayotusumbua leo ni kuitofautisha sauti ya Bwana na sauti ya mwanadamu au sauti ya shetani!
” Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;”Mwanzo 12:1
Ukisoma zaidi utakuta Ibrahimu akitii na kufanya yale aliyoelekezwa na Bwana wake.
▪Iko dhana potofu iliyosambaa akilini mwa watu wengi katika andiko hilo hapo juu kwamba watu hudhania kwamba Ibrahimu alipoitwa aliondoka yeye peke yake. Ukweli ni kwamba alipoondoka hakuwa peke yake bali alitoka yeye,mkewe Sara,mwanaye Lutu ( mtoto wa Harani nduguye )pamoja na watu aliowapata huko harani sawa sawa na kilichoandikwa katika Mwanzo 12:4-5
▪ Hii ikiwa na maana kwamba uendapo kwa Bwana basi usikwende peke yako bali chukua na mke/mme wako,chukua na familia yako kama vile asemavyo Yoshua ” … lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana.” ( Yoshua 24:15 ) isipokuwa kwa habari ya wito tu,ndio unapaswa uende wewe kama wewe. Yapo mambo mawili ambayo Ibrahimu aliyafanya pale alipoisikia sauti ya Bwana.
Kwanza aliitika wito wake, ambao huo ulikuwa unamuhusu yeye peke yake lakini pili alichukua watu wake wakaribu akaenda nao katika wito alioitiwa.Leo,mtu aweza kuitwa na Bwana katika huduma fulani na ukashangaa akatoka yeye peke yake pasipo mume/mke wala familia yake!!! Hii inaonesha mawili,inawezekana mtu huyo hajui tofauti ya kile alichoitiwa na huduma kwa ujumla,Au inawezekana anajua ila anakaidi.
Ibrahimu aliweza kutofautisha kati ya wito wake na huduma,maana wito ulikuwa wake mwenyewe lakini huduma ilikuwa pamoja na watu wake. Ikumbukwe kwamba,baada ya Ibrahimu kutoka katika nchi ya baba yake,ndiposa anaanza kumjengea Bwana madhabahu jambo hili likiwa na maana kwamba sasa alikuwa akitembea katika wito. Imani na utii aliokuwa nao Ibrahimu,ilimuwezesha kutoka katika nchi yake na kwenda alipoelekezwa ambapo hata yeye mwenyewe alikuwa hapajui maana imeandikwa;
” Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.” Waebrania 11:8.Jambo moja tunaloweza kujifunza siku hii ya leo ni kwamba▪ Ibrahimu alikuwa akimuabudu Mungu wa kweli ( Abram was a worshiper of a true God ) maana imeandikwa ; ” Yoshua akawaambia watu wote, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Baba zenu hapo zamani walikaa ng’ambo ya Mto, maana Tera, baba yake Ibrahimu, naye ni baba yake Nahori; wakaitumikia miungu mingine. “Yoshua 24:2.
Biblia inaweka wazi juu ya baba yake Ibrahimu na akina Nahori ndugu wa kunyonya wa Ibrahimu kwamba waliitumikia miungu mingine isipokuwa Ibrahimu ambapo neno halisemi kwamba Ibrahimu aliitumikia miungu bali yeye alimtumikia Mungu wa kweli. Kumbe miungu ya Tera na nduguze iliwazuia kusikia sauti ya Mungu wa kweli,na kwa sababu hawakuweza kusikia basi hawakuwa na imani ya kweli.
Hata wewe ~ yamkini ipo sauti ya Mungu uliyoizuia kwa sababu ya miungu unayoiabudu kama vile akina Tera walivyofanya. Wapo watu wengine kwa sababu ya kungangania mahali pa mapokeo ya kidini,wameshindwa kuisikia sauti ya Mungu wa kweli. Ikiwa unamuabudu Mungu wa kweli basi utaisikia sauti yake maana hata neno linasema walio wake anawajua.
▪ Kuachana na mapokeo ya kidini yasiyofaa sio dhambi. Wala kuiacha miungu sio dhambi hata kidogo,bali dhambi ni kungangana kuitumikia miungu na kuendelea kutembea katika sheria ya mapokeo ya dini fulani ambayo hata wewe mwenyewe hujui maana ya hayo mapokeo. Mtu wa namna hii,ni vigumu kabisa kuisikia sauti ya Bwana Mungu wake na hata akisikia bado atazani ni pepo.
Kwa mfano wa Ibrahimu jifunze mpendwa,utoke mahali ambapo kuna miungu au ibada ya miungu mfano ibada za sanamu,mfano kuwa chini ya sheria mahali ambapo hata Roho mtakatifu hayupo hapo. Haijalishi baba na mama yako wanaabudu wapi,bali angalia sana wewe unaabudu kitu gani,na wapi? Siku hii ya leo nahitaji nifanye maombi na wewe mpendwa katika Kristo Yesu.
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe. Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga sasa kwa + 255 683 877 900
What’s app number +255 746 446 446
Na Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comments