UTAVUNA ULICHOPANDA.
- Mch. Gasper Madumla
- Sep 12, 2018
- 4 min read
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Kila mkulima anajua ya kwamba atavuna kile tu alichokipanda. Kipindi cha mavuno utamwona mkulima akienda shambani akiwa na mundu, na baadhi ya vitendea kazi vya shamba huku akilini mwake ni kuvuna aliyoyapanda. Ni jambo la kushangaza kuona mkulima aliyepanda zao la karanga akitarajia kuvuna mahindi, au aliyepanda mihogo akitarajia kuvuna maembe dodo. Kwa mujibu wa kanuni ya kuvuna, huwezi kuvuna usichopanda. Maisha ya kiroho yanafanana sana na maisha ya shambani katika eneo la kupanda na kuvuna, hali ni hiyo hiyo. Je unamkumbuka Yakobo aliyekuja kuitwa Israeli, unakumbuka nini unaposikia neno Yakobo? Nikukumbushe kidogo ;
Yakobo alipokuwa kijana mdogo pamoja na ndugu yake Esau, Bwana alimbariki sana. Kipindi baba yao Isaaka alipokuwa mzee sana kiasi kwamba alikuwa haoni, kipofu kwa uzee aliokuwa nao. Isaka alimwita mwanae Esau mzaliwa wa kwanza ili ambariki na alimwambia Esau aende kwanza kumwandalia chakula kitamu, kisha baada ya kula ambariki ndipo Isaka afe. Lakini muda huo Isaka anaongea na Esau, mama yao Rebeka alikuwa akisikia maongezi hayo. Na hapo ndipo alipoenda kumshauri mwanae mdogo Yakobo ili mbaraka wa Esau auchukue Yakobo “ kwa hila” Hivyo Yakobo pamoja na mama yake wakacheza mchezo wa kumdanganya baba yao Isaka kwa lengo la kupata mbaraka kwa njia ya hila tu!
Ni kweli Mungu alikwisha mbariki Yakobo tangu tumboni, na alikuwa na Neema. Hivyo kulikuwa hakuna sababu yoyote ile ya kudanganya kwa ajili ya kupata mbaraka, kwa maana ni Mungu mwenyewe angelijua huo mbaraka wa Yakobo ufike kwake kwa njia gani. Yakobo na mamae wakajitengenezea njia zao za udanganyifu katikati ya mbaraka wa Mungu. Ni kweli Yakobo kama kubarikiwa alibarikiwa lakini alikosea kujitengenezea njia mbaya za udanganyifu. Yakobo hakujua ni nini alikuwa akipanda, kwa maaana baadae itamlazimu kuvuna hicho hicho ( soma mwenyewe Mwanzo 27 yote).
Sasa angalia mavuno yake Yakobo!
Alipokuwa na familia ya watoto 12,Yusufu alikuwa mtoto wake ampendaye sana. Nduguzake Yusufu, hawakumpenda kabisa Yusufu kwa maana babaye Yakobo alimpenda kuliko wao lakini pia Yusufu alikuwa mtu wa haki akiepukana na maovu yao kaka zake. Siku moja alipoenda kuwajulia hali kaka zake waliokuwa wakichunga huko Dothani. Walipomwona walimkamata na kumvua kanzu yake nzuri na kisha wakamtumbukiza shimoni na baadae wakamwuuza kwenye mmoja wa msafara.
Ndugu zake wakachukua kanzu yake na kuiwekea damu kisha wakampelekea baba yao Yakobo aliyekuwa amekaa hemani kwake. Wale watoto wake wakamtupia kanzu mzee wao, alafu kama wakasema``mzee, ebu cheki kanzu hiyo, sio ya mwanao kweli? Sisi tumeikuta huko nyikani “ Nafikiri walisema mengi kama hayo. Neno la Mungu linasema;
“ Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi.Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba yake akamlilia.“ Mwanzo 37 :34-35
Hii inaonesha kwamba, Yakobo alimlilia sana mwanae. Ebu fikiri kili alichopanda “njia ya udanganyifu na za uongo alipomdanganya babaye Isaka kipindi cha kubarikiwa kwake, akamfanya mzee wake Isaka kuhuzunika moyo, na sasa uovu alioupanda umemrudia naye hapo ( Mwanzo 37 :34-35) analia na kuhuzunika moyo sana kwa sababu watoto wake wamemdanganya pia kwa kumwambia kwamba mwanaye ampendaye Yusufu amekufa!
Kiukweli kulikuwa hakuna sababu ya mzee huyu kulia. Lakini kwa kuwa alipanda baya, na sasa anavuna baya hilo hilo. Vile anavyosikia maumivu ya kuondokewa na Yusufu ndivyo baba yake Isaka alivyokuwa akisikia. Umeona hapo? Unaelewa lakini? Leo wewe unalia juu ya jambo hilo, lakini kumbuka ulipanda nini? Laiti kama ungelijua usingelipanda ovu ili usivune ovu. Najaribu kufikiri hapo ulipo kazini au shuleni kwako, umepanda nini kwa mwenzako maana wengine hupanda chuki, uongo ili kusudi mtu mmoja afukuzwe kazi au kuachishwa masomo kwa ila tu! Hivi hujui hata katika hilo unalolipanda litakurudiwa wewe mwenyewe? Yes litakurudia wewe mwenyewe, muulize Yakobo alidanganya naye kadanganywa!!!
Kumbuka neno hili;
“ Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.” Wagalatia 6:7
Usije ukamdhihaki Mungu, kwa kujificha kwa wanadamu juu kile unachokitenda kwa siri na kufikiri Mungu hakuoni! Mpendwa ujapofanya kwa siri ilo ulifanyalo lakini ujue Mungu anakuona hata sasa, na hicho hicho ndicho utakachokivuna. Na ndio maana andiko linakuambia “usidanganyike“. Watu wengi wanafanya mambo movu kwa siri sana, hawajui hilo ulifanyalo unalipanda na kuna siku moja utalivuna tu. Mfano wewe unaweza ukawa unatembea na mke wa mtu alafu unajifanya mjanja, ujue utalivuna pando hilo siku moja. Eidha upigwe, au u
Dawa yake ni nini?
01.Toba.
Ukweli ni kwamba, pale unapogundua kosa, huna nafasi nyingine yoyote ya kurekebisha kosa nje ya toba. Fikiri kile ulichopanda kibada kitaondolewaje bila toba? Haiwezekani ni kwa njia ya toba, tena ni toba halisi kwa kweli.
02. Jijengee mazingira ya kupenda kumfanyia mtu kitu unachopenda kufanyiwa, mwombe Roho mtakatifu akusaidie katika hili.
“Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii” Mathayo 7:12. Kama ilivyo kanuni ya kuvuna kwa kile ulichokipanda, basi ndivyo ilivyo kama utafanikiwa kupanda mema kwako na kwa wengine, na hapo utavuna mema. Ni ngumu lakini inawezekana kwa msaada wa Roho mtakatifu.
Kwa msaada zaidi pamoja na maombezi tafadhari, unipigie kwa namba yangu ya simu. Zipo hapo juu, yamkini unahitaji msaada zaidi, piga tu sasa.
Kwa mawasiliano +255 683 877 900
Mch. Gasper Madumla
What’s app ni +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments