top of page

UTASHINDA KWA MAOMBI.~01


Bwana Yesu asifiwe..

Kwa ufupi,

Kuna mambo mengine huwezi kushinda kwa nguvu zako za kawaida,isipokuwa kwa njia ya kuomba tu. Kawaida maombi yanatusaidia sana,hasa pale tunapokuwa tumefikia mwisho wa kupambana kwa akili zetu binafsi. Ni vyema ukatambua kwamba,kuna mengi usiyoyajua kwa maana yamefichwa mbali na upeo wa macho yako,lakini katika hayo yote,huna budi kuyajua sasa,na njia moja kubwa ya kuyajua yale yaliyo mbali na upeo wa macho na masikio yako ya kawaida ni “ kuomba”. Binafsi sijawahi kusikia popote pale kwamba kuna mtu alipata hasara ya kuomba! Kwa sababu hakuna hasara kabisa katika kuomba. Lakini ni vyema tukajifunza kwamba ushindi unapatikana kwa njia ya kuomba tu. Unajua kwa kuomba kwako kutakufanya uishinde vita unayopitia sasa. Ingawa tunapenda kushinda katika yote tunayopitia lakini bahati mbaya,wengi wetu hatupendi kujikitita katika kuomba.

Hata hivyo Biblia inatupa habari ya waombaji,na inasema kwamba wapo waombaji lakini baadhi yao ni watu wenye kuomba vibaya ili kusudi watumie kwa tamaa zao.  Katika Yakobo 4:3. Ukweli ni kwamba tunajichanganya sana katika uombaji wetu kwa maana mara nyingi hatujui kuomba ipasavyo isipokuwa Roho hutusaidia katika udhaifu wetu. Katika kitabu cha Yakobo 4:3,tunajifunza mambo yafuatayo,ambayo anatukwamisha katika ushindi wetu;

01. Kusukumwa na tamaa mbaya!

Wengi wetu tunaomba nje ya mapenzi ya Mungu kwa sababu tunasukumwa/ongozwa na tamaa zisizofaa. Hivyo “tamaa” zimekuwa ni kichocheo kikubwa katika kuomba,na si Roho mtakatifu anayepaswa kusukuma maombi. Siku zote tamaa zikichukua nafasi,basi hapo zitamtoa mwombaji katika kusudi mama la kuomba kwake. Tunapozungumzia tamaa mbaya,ni hali ya mihemuko/hisia/uchu wa kimwili wa kutamani kuwa kama fulani au kupata kama fulani. Hali hiyo haisukumwi na Roho mtakatifu,bali tamaa binafsi na wakati mwingine shetani.

~Je ni kanuni au taratibu gani nzuri za maombi?

JIBU:Kanuni au taratibu za uombaji mzuri ni kama ifuatavyo;

01. MWOMBAJI AWE NA HOJA KAMILI.

Mwombaji yeyote anapaswa apeleke hoja yenye nguvu mbele za Bwana Mungu wake. Imeandikwa“ Haya, leteni maneno yenu, asema Bwana; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo. “ Isaya 41:21

Ikiwa Bwana anasema tumpelekee hoja zetu zenye nguvu,basi ujue kuna wakati hoja hizo zilikuwa zikipelekwa zisizokuwa na nguvu. Maana ukiona pametajwa hoja zenye nguvu,basi ujue zipo zisizo na nguvu.

▪ Hoja ambazo hazina nguvu,ni zile ambazo mwombaji huomba mambo mengi ndani ya dakika chache pasipo kupangiliwa na kuongozwa na Roho mtakatifu.

Wapo watu wenye kumpelekea Bwana hoja zisizo na nguvu,mfano utamkuta mtu akiomba mambo mengi kama thelathini hivi kwa wakati mmoja pasipo mpangilio wa kuongozwa na Roho mtakatifu. Sababu ikiwa Roho wa Bwana akikuongoza kuyaomba hayo yote ndani ya dakika chache basi hapo utakuwa umepeleka hoja kamili mbele za Bwana.

Lakini ukiona umeomba mambo mengi pasipo mpangilio wa Roho mtakatifu kwamba katika maombi yako hakuna mambo ya kipaumbele ya kuyaomba basi ujue hujapeleka hoja kamili.

Mfano umeomba uolewe/kuoa gafla hujamaliza ukaomba ujenge,kisha ukaongeza kupata safari za ulaya~gafla tena ukaomba wadeni wako wasahau madeni yao wanaokudai hali ukijua dawa ya deni ni kulipa na kwamba hakuna maombi ya namna hiyo! Tena ukaongeza kuomba kibali kazini kwako, hapo hapo ukakumbuka kwamba hujala,ukaomba upate chakula cha mchana,na ikatokea wakati wa kuomba kwako akaingia jirani yako uliyekuwa una ugomvi naye katika miaka ya nyuma,ukaanza kumvunja na kumbomoa katika maombi,yaani!! N.K Hapo utakuwa hujapeleka hoja kamili,na utakuwa umepayuka-payuka ( Mathayo 6:7 ).

Kwa sababu maana kamili ya neno kupayuka~payuka sio kuomba kwa sauti kubwa,bali ni kuomba pasipokuwa na mpangilio maalumu kama mfano niliyokupa hapo juu,hivyo basi kumbe mwombaji hata kama akiomba kimya kimya anaweza akawa anapayuka payuka mbele za Bwana ikiwa kama hana mpangilio maalumu wenye kuongozwa na Roho mtakatifu.

Ikumbukwe ya kwamba yeye mwenye mpangilio maalumu hata kama akiomba kwa sauti kubwa ya namna gani hapayuki~payuki,maana mpangilio maalum wa maombi huongozwa na Roho mtakatifu ambaye Yeye hufanya mambo yote katika uzuri na utaratibu 1 Wakorintho 14:40.

Bwana Yesu Kristo,mara nyingi aliwaambia wale wenye mahitaji kwamba  “wataka nikutendee ni nini? ” hali akijua shida zake zote mtu yule aliyemuendea. Swali la namna hili, Yesu Kristo alikuwa akitaka kujua ni kipi haswa chenye nguvu kinachomsumbua mtu. Mfano tazama Bartimayo yule aliyekuwa kipofu,jinsi ambavyo Yesu Kristo alivyomuuliza kwamba “ Wataka nikufanyie nini?” Kisha Bartimayo akamjibu “ Nataka nipate kuona” Marko 10:51-52

Ombi la Bartimayo la kutaka kuona lilikuwa ni ombi lake lenye nguvu sana. Sababu kumbuka ya kwamba Bartimayo alikuwa ni muhitaji wa pesa,muhitaji wa vitu N.K~ ndio maana alikuwa akiomba watu wamsaidie pale njiani alipokuwa ameketi. Mtu huyu angeliweza amuombe Bwana Yesu pesa,lakini alipogundua siri hii ya kwamba anapaswa apeleke hoja yenye nguvu,ndiposa akaomba apate kuona.

Wewe je!! Pindi uombapo unapeleka hoja kamili yenye nguvu? Maana ukiweza kuwa na hoja ya msingi basi ujue vingine vitafuata juu ya jibu katika ombi lako lenye nguvu. Mtazame mfalme Sulemani,alipoambiwa aombe atakalo~ Sulemani akampelekea Bwana ombi moja tu lenye nguvu,akasema apewe moyo wa adili ili awahukumu watu wa Mungu na kuweza kupambanua mema na mabaya,aliomba moyo wa hekima (  1 Wafalme 3:4-9 )

Kisha BWANA akampa,na akampa na utajiri ambao hakuuomba. Utajiri ulifuata baada hoja kamili kutolewa. Mungu wetu anatujua vyema,anachotaka tumuambie yale mambo ya msingi kwanza,ambapo mengine hufuata badaye. Sijajua wewe una hoja gani kamili ambayo wataka leo kumuambia BWANA. Basi sasa waweza kuomba pamoja nami kwa kunipigia simu yangu hapo chini…

ITAENDELEA…

Ikiwa umebarikiwa na ujumbe huu,basi nifahamishe tupate kumtukuza Mungu pamoja. Lakini inawezekana labda unahitaji MAOMBI kwa maana nawe unapitia changamoto hii,Basi kwa yote nipigie sasa kwa + 255 683 877 900

What’s app namba ni +255 746 446 446

Na Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page