top of page

USIACHE KUOMBA,YAPO MAJIBU.

Usiache kuomba / A constant prayers /Praying until something happens

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi,

Kuna kuomba katika kiwango cha chini pia kuna kuaomba katika kiwango cha juu. Kuomba kwenye kiwango cha chini ni pale mwombaji anapoomba kilegevu,na baadae kuacha kuomba.Lakini kuomba kwenye viwango vya juu ni pale mwombaji anapoomba mpaka kitu fulani kitokee. Hii ni sawa na kusema “kuwa kinganganizi wa maombi”. Ukweli ni kwamba kuna mambo hayawezi kutoka katika uombaji wa kawaida kawaida tu,ndio maana Yesu aliwaambia wanafunzi wake kwamba “ Ila namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga” Mathayo 17:21. Mkazo wa Yesu ni kutufundisha kwamba kuna mambo yasiyotoka mpaka umaanishe zaidi katika kuomba na kufunga. Bado nia ipo pale pale ya kufundisha watu wenye kutamani kuona mambo makubwa hawana budi kukaza kuomba,wala wasiache!

  1. Kipindi cha Eliya.

Eliya ni mmoja wa watu waliokuwa na imani thabiti kwa Mungu. Ni mfano mzuri wa mwombaji kinganganizi,mtu mwenye kuomba mpaka kitu fulani kitokee. Naye alikuwa ni mwanadamu mwenye tabia ya uanadamu kama wewe,lakini hakuacha kuomba,na hatimaye mengi yalitokea kwa kuomba kwake (Yakobo 5 :17). Habari zake zimeandikwa kwa makusudi kabisa,ili kukufundisha kwamba katika maombi kuna majibu,lakini majibu hayo hayawezi kuja kwa wepesi,bali kwa kupambana! Eliya alifanikiwa kusimamisha mvua kwa muda wa miaka mitatu na nusu! Je unafikiri maombi yake yalikuwa ni maombi ya kitoto toto? La! Aliomba akimaanisha!

  1. Usiache kuomba,yapo majibu

Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele. Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini. Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba.’‘ 1 Wafalme 18:41-43 Biblia inasema Eliya alimwambia Ahabu “inuka kwani panasauti ya mvua tele” Ukweli ni kwamba hapakuwa na mvua yoyote,lakini katika kipindi kikavu,Eliya anaiona mvua ( Eliya anayaona majibu ya maombi yake kabla ya kuyapata majibu hayo). Si wengi wenye kuweza kuona majibu yao kabla ya kuomba,lakini mwombaji halisi anapaswa kuona majibu yake kabla ya majibu hayo kudhihilika katika ulimwengu wa mwili / damu na nyama.

Lakini si tu hivyo,biblia inatuambia hapo,Eliya alipopanda mlimani kuomba,aliomba mara ya kwanza lakini hakukuwa na majibu,na huku ndani yake anayaona majibu yake. Yaani ndani yake anaiona mvua kubwa,lakini mazingira ya nje yanakataa yakisema hakuna mvu. Hata hivyo akaomba tena mara ya pili na kumtuma tena mtumishi wake acheki kama kuna dalili yoyote ya kile anachokiona rohoni,lakini hata hivyo mtumishi wake anamletea majibu ya kwamba “hakuna mvua hata kidogo” Eliya anapanda tena kwenye maombi kwa mara ya tatu,kisha hakuna majibu.

Anafanya hivyo mpaka mara ya saba.Katika mara ya saba ndipo anaona kiwingu kidogo kama mkono wa mtoto! lakini bado Eliya anaiona mvua! Haikuwa rahisi kwamba unatoa majibu lakini hayaonekani,kisha unaomba ukitegemea Bwana akujibu mapema lakini Bwana hakujibu hapo. Ni rahisi sana kukata tamaa na kusema “nimechoka maana sioni hata dalili ya hiki nikiombacho!” Lakini haikuwa hivyo kwa Eliya,mtu ambaye aliomba mpaka kitu kikatokea. Kama Eliya amefanya hivi,ujue basi na wewe unaweza,kwa sababu Mungu ni yule yule.

  1. Je Mungu alikuwa hasikii maombi ya mwanzo ya Eliya?

Unaweza ukajiuliza hivyo,lakini majibu yake ni kwamba Mungu alikuwa akisikia tangu Eliya alipotia nia ya kuomba,alimsikia. Lakini Bwana alimtaka Eliya akaze kuomba kwa maana kile akiombacho ni kikubwa,na kwa kusudi akufundishe kwamba kuna mambo ambayo yanakuhitaji kuomba na kuomba nakuomba na kuomba,bila kuchoka kwa maana yapo majibu yako tu. Tatizo lake unapoomba na kuona majibu yamechelewa,basi unakata tamaa na kuona kwamba haiwezekani,Nani kakwambia kwamba Mungu anashindwa na hilo unaloliomba? Jifunze kwa Eliya ambaye kabla ya kuomba aliamini kupokea tayari,kisha akakiri kwa kinywa yale anayoyaamini,kisha akaomba kwa juhudi zote,bila kuangalia atajibiwa saa ngapi;

ama lini lakini neno moja alilokuwa akilijua ni kwamba “yapo majibu yangu / ipo mvua tayari”. Ebu jiulize mwaswali haya; Je uombapo unakiri kupokea kabla ya kupokea yenyewe? Je una kasi gani katika kuomba? Je upo tayari kwenda mlimani / kufunga ? Je upo tayari kuvumilia na kuendelea kuomba? N.K Kumbuka usiache kuomba,kuna majibu yako tayari,kaza kuomba! Jifunze kwa Eliya,kwamba kuna majibu yanayochelewa hata kama utaomba. Lakini usiache kuomba kwa maana yajapochelewa,ujue yapo na yanakuja.

Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja. Kwa msaada zaidi na MAOMBI piga +255 683 877 900

What’s namba + 255 746 446 446

Na Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page