KUOMBA KWA MAMLAKA.
- Mch. Gasper Madumla
- Apr 13, 2018
- 5 min read

Na Mch Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe….
Kwa ufupi..
Kuna utofauti mkubwa sana katika eneo la maombi,na ni vigumu kujua undani wa utofauti huu ni mpaka pale utakapokuwa muombaji haswa na Bwana akufunulie siri hizi. Kuna kuomba nje ya mamlaka na kuna kuomba ndani ya mamlaka ingawa kila aombaye yu ndani ya mamlaka ya Kristo Yesu. Jambo hili ni siri,na ndio maana inawezekana ikakuchukua muda kuelewa. Ukweli ni kwamba kila aliyeokoka amepewa mamlaka lakini shida ipo kwenye matumizi ya hizo mamlaka,na hapo ndipo pana utofauti mkubwa.
Mfano utofauti wa kuomba nje ya mamlaka; mchungaji anaweza akamuombea mtu vizuri kabisa,akamuombea kwamba mtu huyo abarikiwe “ Baba katika Jina la Yesu Kristo,ninaomba umbariki mwanangu huyu,nguvu yako umpe akastawi…n.k” kisha angalia tena hapa “ Baba katika Jina la Yesu Kristo, ninambariki mwanangu huyu,ninaachilia nguvu yako na akastawi ” utofauti uliopo hapo ni kwamba mmoja anaomba pasipo kutumia mamlaka aliyopewa na mwingine anaomba akitumia mamlaka aliyopewa. Mchungaji amepewa mamlaka ya kubariki,hivyo hana sababu ya kutoitumia mamlaka hiyo moja kwa moja katika Jina la Yesu Kristo – “ Yakobo akawaita wanawe, akasema, Kusanyikeni, ili niwaambie yatakayowapata siku za mwisho.” Mwanzo 49:1
Katika andiko hili ( Yakobo 49:1) ukisoma na kuendelea, tunaona mzee Yakobo akiwaita wanawe na kuwabariki wote lakini anaanza kumbariki mmoja mmoja. Kama mzazi amepewa nguvu ya kubariki na nguvu ya kulaani pia,hivyo Yakobo anatumia vyema nguvu ya kubariki na anabariki ipasavyo. Huu ni mfano tu,ukionesha kwamba ikiwa umepewa mamlaka fulani ndani ya Bwana,basi itumie vizuri. Unayo nguvu hii katika Bwana,ya kubariki au kuomba kimamlaka na mambo yakawa. Fahamu ya kwamba Mungu amekumilikisha kazi ufanye pamoja naye,si wewe ufanyaye peke yako bali pamoja na Bwana.
Maombi kwa mamlaka ni yale maombi yaombwayo katika ufahamu halisi sawa sawa na nguvu uliyopewa. Mfano Bwana amekupa nguvu ya kuamuru katika Jina la Yesu Kristo,hatimaye mambo yakaenda. Badala ya kuomba mtoto wako afunikwe na damu ya Yesu,unaweza ukatumia mamlaka hiyo kuomba katika Jina la Yesu,na kuachilia damu ya Yesu. Badala ya kuomba ulinzi kutoka kwa Bwana,unaweza ukaachilia ulinzi Jina la Yesu. Maombi ya namna hii yanafanywa na wale wenye mamlaka waliojitambua.
Kuomba bila mamlaka uliyopewa ni sawa na askari aliyepewa silaha yenye uwezo wa kumpiga adui,kisha akaomba aliyempa silaha hiyo aje na kuitumia badala yake huku akiwa ni yeye aliyepewa ndiye kaishika! Kumbe angeliweza kuifyetua pale pale mkononi mwake maana amepewa tayari aitume. Fikiria upo ndani na una silaha ambayo aliyekupa amekupa uitumie,alafu wakati wa kutaka kuitumia unaanza kumuita aliyekupa ambaye yupo nje au chumba kingine kwamba aje kwako kisha achukue silaha hiyo hiyo aitumie kisha akupe tena. Maombi ni silaha kubwa sana dhidi ya nguvu za giza katika ulimwengu wa roho. Kuna wakati mwingine inakulazimu utumie mamlaka ya kukemea,kufukuza,kuharibu,kungoa,kuangamiza kisha na kupanda ( Yeremia 1:10)
Ni kweli kuna wakati unabidi uombe ukimsihi Bwana atende,na huwezi kuomba kwa mamlaka ukimsihi Mungu. Lakini utaomba kwa mamlaka dhidi ya mambo mengine. Sasa si wengi wanaotumia maombi ya namna hii,maana wengi tunajua maombi ya kumsihi Mungu tu bila kujua kwamba Bwana ametupa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi ( Luka 9:1). Unajua kushindwa kutumia mamlaka katika maombi yako kunapelekea kuonewa na ibilisi,au kutokupata majibu wakati mwingine;maana ikiwa Mungu anakusubiri uombe kwa Jina lake utamke mambo na yawe,lakini na wewe umekaa unamsubiri Yeye Mungu atende.
Siku moja tukiwa katika maombi ya jioni kwenye fellowship huko kwangu. Gafla popo akaingia ndani pale sebuleni tulipokuwa tumesimama sote tukiomba. Tukiwa kwenye maombi,ndipo popo nae akaonekana kwenye dari / paa la nyumba hiyo. Sasa kilichotokea wengine wakamuona yule popo aliyekuwa akiruka ruka juu na wakati mwingine akihama kochi hili na kochi hili,waliomuona kwanza wakapunguza nguvu ya kuomba. Mimi sikumuona haraka hivyo nikashtuka kuona mbona sauti za waombaji wenzangu zimekata gafla hivi na wengine wamepunguza kasi ya kuomba. Nilipoangalia huku na kule nakagindua kumbe popo aliyeingia ndie katibua hali ya hewa!
Sasa cha ajabu ni kwamba badala ya kupata nguvu zaidi ya kuomba kwenye eneo kama hilo badala yake wakakosa nguvu na umakini wa kuomba,nikawaambia“hakuna chochote kitakacho wadhuru,kama kulikuwa na mpango mbaya basi ungelikwisha wadhuru,lakini mpaka naona hivi,maana yake ni ushindi huo” . Hivyo walivyokuwa na hofu kana kwamba ni mimi ndie ninatakiwa kumfukuza,kilichotakiwa ni kuomba kwa mamlaka kwa kumuamuru na kumfukuza huyo popo na chochote kilichopangwa katika ulimwengu wa roho. Ni hivyo tu,kuna wakati wa kutumia mamlaka tu.Kuomba kwa mamlaka ni moja ya omba ya Yesu,Yesu alikuwa akiamuru mambo kadha wa kadha na mambo yakawa.
Lakini ikiwa kama mtumishi wa Mungu haompi kwa mamlaka aliyopewa basi tunaweza kujiuliza kwa nini? Na lazima kutakuwa na sababu fulani tu,sababu Bwana anataka kila muombaji awe na nguvu ya kuamuru mambo,au kutamka juu ya mambo na kuwa. Huna sababu kuwa mchungaji ndipo uweze kufanya haya yote,bali unachohitaji ni kukaa uweponi. Na kumbuka ndani yako kuna nguvu ya ajabu sana ila inawezekana bado hujaitumia lakini ukianza kutumia utaona vile Mungu atakavyofanya kazi na wewe.
Kumbuka,“kuomba kwa mamlaka” haina maana ujitegemee wewe mwenyewe kwenye maombi au uwe unafanya vitu kwa akili zako mwenyewe! Hapana!!!’ Bali maana yake ni kumtegemea Roho mtakatifu huku ukitumia uweza wake wote. Unajua,ebu fikiria pale ulipokuwa duniani ni mara ngapi ulikuwa ukitamka mambo ambayo kwa kweli ni mabaya na ulitamka kwa nguvu zote,alafu yakafanyika mfano,wengine waliwaambia watoto wao “ mbwa wewe!…hautafanikiwa kabisa!!! ” Sasa wakati huu ukiwa umeokoka (kama umeokoka lakini) unashindwa nini kutamka baraka kimamlaka mfano “ ninakubariki…wewe ni mshindi…” unapomuomba Mungu afanye ni vyema sana na ndivyo inavyotakiwa,lakini ikiwa Mungu amekupa mamlaka unasema “ Katika Jina la Yesu Kristo,ninakubariki….” na huku ndiko kutumia mamlaka vizuri.
Nifanyeje ili niombe kwa mamlaka?
Hakikisha unaongeza kiwango che Neno.
Yeyote mwenye mamlaka katika maombi yake ni yule mwenye utiisho mkubwa wa neno. Neno la Kristo ndilo likupalo mamlaka iliyokuu katika maombi yako. Maombi yasiyoambatana na neno ni kana kwamba yanapea,hayana nguvu. Unapotamka neno lako huku ndani yako kuna kiwango cha juu cha Neno utashangaa mambo yatakavyojibiwa. Ukisema “ninakubariki sawa sawa na ilivyoandikwa kwenye biblia…” uwe na uhakika Mungu ataliangalia neno lake apate kulitimiliza ( Zab 107:20)
Hii ni kanuni kubwa sana itakayokupa uhakika wa kile unachoomba,maana Neno la Kristo likijaa kwa wingi ndani yako,utajua wakati gani ulio sahihi wa kuomba na uombe nini haswa kwa ufunuo maana Roho mtakatifu ndiye atakayekusaidia ( sababu Roho mtakatifu huketi kwenye neno) . Ufahamu huu ninaokufundisha leo kuhusu “ vile Neno linavyokusaidia hata uweze kuomba kwa mamlaka” ni ufahamu adimu sana maana si wengi wenye kujua mambo haya.
Fahamu leo kwamba si kila anayeomba anaomba kwa mamlaka ingawa wote wanaomba katika Jina la Yesu Kristo lenye mamlaka. Najifunza kwa mzazi anayetaka kumtamkia mwanaye kitu,utagundua mzazi hutamka moja kwa moja kwa sababu ndani yake kuna nguvu hiyo,na vivyo hivyo ndani ya Kristo umepewa mamlaka ya kuratibu mambo moja kwa moja katika Jina la Yesu Kristo
Kwa huduma ya maombezi na msaada zaidi nipigie kwa ;+255 683 877 900
Namba ya What’sapp ni +255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comments