BIDII KATIKA MAOMBI💪
- Mch. Gasper Madumla
- Feb 10, 2019
- 3 min read

Kwa ufupi;
Hivi bidii ya maombi hupelekea nini?
Kumbuka;
Maombi yakifanywa kwa bidii,yanakuwa na matokeo mazuri kwa maana Mungu hupendezwa na bidii ya mwombaji. Unajua ,Yeye Bwana hujibu maombi yetu,ila wakati mwingine sisi tunachelewesha majibu yetu kwa kukosa bidii wakati wa maombi. Bidii ya kuomba ni jambo muhimu sana kwa maana mwenye bidii huona mengi tofauti na mwombaji mlegevu.
Bidii ya maombi ni hali ya kurudia rudia kuomba bila kukata tamaa pamoja na kushukuru. Tendo hili la kurudia rudia kuomba wakati wote husababisha Mungu kuingilia kati katika yale magumu uyaombayo. Mfano mzuri tunajifunza kwa Eliya mtumishi wa Bwana aliyeomba kwa bidii kuizuia mvua isinyeshe kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita. Kwa upako wake na kuchanganya bidii aliyokuwa nayo,tunaona majibu ya maombi yake.
• Bidii ya maombi husababisha miujiza mikubwa.
“Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.” Yakobo 5:17
Ebu tazama kwa umakini neno hilo,kisha ona vile tabia ya Eliya ilivyokuwa. Kwanza Biblia inatuambia kuwa Eliya alikuwa ni mwanadamu kama sisi.Hakuwa malaika,bali mwanadamu ambaye alikuwa na namna yote ya ubinadamu. Pamoja na ubinadamu wake aliokuwanao mtu huyu alikuwa ni mwombaji mwenye bidii kubwa,kiasi kwamba miujiza ilikuwa ikimfuata yeye. Unajua kitendo cha kusimamisha mvua hakikuwa ni kitendo cha kitoto toto/cha kawaida,bali ni mujiiza mkubwa. Bila shaka Eliya alikuwa pamoja na Bwana. Lakini si hivyo tu,Eliya alitenda mengi kwa bidii. Angalia pia katika 1 Wafalme 18:1-20
Ukisoma hilo andiko,utaona Bwana anamrudisha Eliya kwa mtesi wake Ahabu ili Bwana alete mvua. Eliya kurudi kwa Ahabu kulihitaji ujasiri,imani pamoja na ibidii katika maombi. Lakini hatimaye tunamwona Eliya akifaulu mtihani huo wa imani. Na hapa tunaweza kujifunza kwamba,Mungu anaweza kukurejeza kwa mtesi / adui wako ili yeye akaonekane huko,isipokuwa unapokuwa mbele ya mtesi wako usijipambanie mwenyewe,mwache Bwana akupiganie.
Eliya mbele ya Ahabu. ( 1 Wafalme 18:41-45)
Ukisoma hayo maandiko kwa utulivu, utajifunza kitu kikubwa sana ninachofundisha hapa. Angalia hili ; Baada ya Eliya kumwambia Ahabu aende nje kuna mvua kubwa, Ahabu kweli alikwenda lakini hapakuwa na mvua yoyote. Eliya akachukua hatua ya “kupanda mlimani” kuomba, naye akaomba huko. Mara ya kwanza alipoomba, akamtuma mtumishi wake akacheki kama mvua imekwishaanza, naye mtumishi wake akakwea juu, kuchungulia huku na huku hakuona kitu chochote. Akarudi na kumwambia Eliya “ hakuna kitu” dah!
Akafanya hivyo mara kadhaa lakini hakuna majibu na ukumbuke hapo ameambiwa ya kwamba akijionesha kwa Ahabu, mvua itanyesha ( 1 Wafalme 18:1). Je Mungu alimdanganya? Mbona amejionesha na mvua hakunyesha? Lakini, Kumbuka Mungu si mtu, aseme uongo;Wala si mwanadamu ajute. Akisema amesema ( Hesabu 23:19). Ikiwa ndivyo, shida ilikuwa wapi? Bila shaka Mungu alikuwa akiangalia bidii ya Eliya aliyokuwa nayo katika kuomba. Kwa maana alipoenda mara ya saba, Bwana alifungua mvua nao ikanyesha. Ebu fikiria kama Eliya angeliomba kilegevu legevu kama uombavyo wewe leo, hiyo mvua ingelinyesha? “Bidii, bidii, bidii, bidii tena narudia bidii ni kitu muhimu sana kwako… “
Ebu jiulize, ni mara ngapi umekuwa ukiomba kilegevu na kukata tamaa? Tena umeomba kidogo tu, kisha ulipoona hakuna badiliko lolote ukaacha! Wewe unafikiri mambo mazuri unayoyataka yatakuja kwa mteremko kama utakavyo bila kutoka jasho? Jasho lako linahitajika katika kuomba hili hilo ulipokee.
Mjane na mzee aliyekaza kwa bidii katika kuomba, auona utukufu wa Bwana. ( Luka 2:36-38).
Mara nyingi nikisomaga biblia yangu,napenda kujifunza kitu kwa huyu mzee nabii mke ambaye kwa kweli uzee wake ulikuwa kwenye mwili tu lakini hakuzeeka rohoni, kwa maana alikaza sana katika kufunga na kuomba, tena alikuwa akiomba hekaluni “haondoki hekaluni“. Huyu alikuwa na miaka 84, na amekaza kwenye kufunga na kuomba, vipi wewe ambaye hata miaka 60 hujafika huwezi kufunga wala kuomba.
Ukiambiwa kanisani kwako kwamba kuna mfungo na maombi basi hapo ndipo wamekutibua na kuzila unazila kanisa!!! 🏃🏃🏃. Sasa, utafanikiwaje mpendwa? Ebu mtazame huyu ambaye ni mjane na mzee lakini kafanya maamuzi ya kukaza kweli kweli, sasa unashindwa na mtu mzima kama huyu? Weka bidii sasa katika maombi na utauona utukufu wa Bwana.
Bidii katika maombi inatoka wapi?
Bidii ya kuomba hutokana na kiwango kizuri cha mazoezi ya kiimani ( kujizoeza kuomba,kusoma na kutafakari Neno n.k) Katika kila zoezi la kiroho,unapaswa kumwomba Roho mtakatifu kwa maana Yeye ndiye mwezeshaji. Anza leo kujiwekea ratiba ya maombi kila siku na uzingatie kuyatimiza uliyojipangia. Na gafla utaanza kuona bidii ya maombi ikiongezeka.
Ikiwa kama umebarikiwa nifahamishe, pia Kwa maombi na msaada zaidi , piga +255 683 877 900.
What’sapp namba+255 746 446 446 .
Mch. G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comentarios