top of page

USIWE NA TABIA YA KUPENDA FEDHA.


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi sana…

Waswahili wanasema“pata pesa tuijue tabia yako” hawajakosea kwa kauli hii. Maana tabia halisi ya mtu ( hata tabia ya aliyeokoka utaijua vizuri baada ya kuishika pesa.) Kuna watu leo ni wapole sana yaani watulivu fulani hivi,lakini kumbe utulivu wao ni kwa sababu hawana pesa,sasa ngoja wapate pesa! Wanasumbua hao,na hata upole na utulivu haupo tena😁😁😁. Sijui wewe tabia yako ikoje sasa,je ukiwezeshwa mijipesa utabaki hivyo hivyo au ndio utakuwa hautulii? Neno linasema;

“ Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.” Waebrania 13:5

Kupenda fedha ni tabia ya kila mtu kwa maana hakuna aichukiae fedha,lakini neno linakutahadharisha ya kuwa hutakiwi kuipenda fedha kwa maana ni shina moja la mabaya ya kila namna ambayo wengine hali wakiitamani fedha na wamefarakana na imani ( 1 Timotheo 6:10). Wale wote wenye kupenda fedha kupindukia mara nyingi wameigeuza na kuitumikia na wameifanya mungu kwao,na kitendo hicho basi wamefarakana na imani.

Unapaswa uridhike na vile ulivyonavyo,(haina maana usitafute fedha,hapana) nafasi ya kwanza apewe Mungu si fedha. Fedha ni adui mkubwa wa imani ikiwa utaipa nafasi ya kwanza,kumbuka lile neno alilosema Bwana juu ya kuwatumikia mabwana wawili  “ . .. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali” Mathayo 6:24. 

Leo hii huduma nyingi zimegeuzwa na kuacha njia saa ya Bwana kwa sababu ya kupenda fedha,karama hazitumiki vizuri kwa sababu mwenye karama ameangukia kwenye kupenda fedha,nabii nyingi ni za uongo kwa sababu ya kupenda fedha n.k. Kile ambacho unatakiwa kujifunza ni kuwa makini sana na kitu kinachoitwa fedha. Usikubali fedha ikutawale bali uitawale! Je hivi unajua ni watu wachache mmno ambao wana Mungu huku wakiwa na pesa? Wengi wenye pesa hakuna kumpenda Mungu na wala hawana Mungu. 

Tabia ya kupenda fedha ikikutawala basi ujue na imani utaiacha,maana muda wa ibada wewe utakuwa ukikimbizana na kutafuta fedha. Na hili tumelishuhudia kwa watu wengi tu. Huwezi kuwa salama kwenye eneo lolote lile ikiwa una tabia ya kupenda fedha,iwe ni mtumishi wa Mungu au mtumishi wa serikali au mfanyakazi. Ebu cheki maisha ya mtu mwenye tabia ya kupenda fedha inakuaje,alafu niambia,utagundua kwamba mtu wa namna hiyo hana utulivu na ni mdhambi wa kawaida,maana uongo hakosi,hakosi kujiinua,uzinzi utakuwepo au la utakuwa ukimnyemelea,nakadhalika!

Dawa ya tabia hii ni kujitahidi kuridhika na pato au mshahara wako,unaridhika na mavazi uliyonayo,malazi na makazi uliyonayo. Usipende vitu vikubwa hali huna pesa bali ridhika na ulichonacho.Kumbuka; Maovu mengi kama si yote husababishwa na tabia ya kupenda fedha. Ukiweza kujizuia kupenda fedha basi ujue Mungu atakujazi kwa uaminifu wako…

Kwa msaada zaidi na maombezi,

Piga sasa kwa +255 683 877 900

Namba ya what’s app ni .+255 746 446 446

Mchungaji Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page