UNYENYEKEVU KIPIMO CHA MAJIBU YA MAOMBI.
- Mch. Gasper Madumla
- Nov 8, 2019
- 3 min read
Updated: Aug 30, 2022

Kwa ufupi,
Watu wengi hatujibiwi maombi yetu kwa sababu ya kukosa unyenyekevu wakati wa maombi. Na ikiwa tunakosa kunyenyekea pale tuombapo,hii ina maana hatuna unyenyekevu hata mioyoni mwetu. Ukweli ni kwamba unyenyekevu ni siri kubwa katika maombi yako. Ni ukweli pia suala la kujibiwa maombi yako ni la Mungu mwenyewe,Yeye Mungu ndiye anayehusika hasa na kujibu au kutokujibu,na wala huwezi kwenda kushtaki au kulazimisha majibu ya kuomba kwako,hiyo ni kweli. Lakini hata hivyo kuna sababu nyingine zinatokana na mtu binafsi..
Unyenyekevu unahusika pia kwenye maombi. Kuwa mnyenyekevu katika maombi kunahusisha na utulivu,pasipo kumwamrisha Mungu atende utakavyo. Unyenyekevu wakati wa maombi hauzuii kukemea pepo,au roho yoyote ile kwa sababu umepewa mamlaka,isipokuwa baada ya yote hayo,ni vyema ukamsihi Bwana atende,kuna namna ambayo ya kujishusha mbele za Bwana. Ukisoma maombi ya Yesu, utagundua yalijengwa kwenye unyenyekevu mkubwa sana kwa maana Yeye mwenyewe ni “ mpole na mnyenyekevu wa moyo” ( Mathayo 11:29)
Wapo watu ambao wamekosa unyenyekevu, watu hawa wanaonekana hata katika kuomba kwao. Kama ni mtu makini,ukifuatilia hiki ninachokieleza utagundua mambo mawili katika eneo la maombi, mambo hayo ni “ sauti yenye mamlaka lakini pia kuna sauti yenye kiburi na kukosa mamlaka” Kuwa na sauti yenye mamlaka inaonekana wazi,kwamba yeye aombaye ana utiisho ndani yake. Na yule mwenye sauti yenye kiburi,utagundulika haraka kwa maneno yake.
Mwenye sauti ya mamlaka hupenda kumwinua Bwana ajapoomba au kuombea mtu,bali yule mwenye sauti yenye kiburi hujiinua yeye kwa kutaka kuonekana kwamba yupo na nguvu za Mungu, kwa hiyo mbwembwe kwake ni kitu cha kawaida kabisa! Sasa si rahisi kujibiwa kwa staili hii. Lakini hata hivyo Mungu bado ni mwaminifu,kwa maana Yeye wakati mwingine hujibu tu hata kama mwombaji akitafuta sifa.
Kwani hujasoma habari ya Musa?
Pale alipoambiwa auambie mwamba utoe maji,bali yeye akaupiga kama ile mara ya kwanza, alifanya tofauti na alivyoelekezwa na Bwana. Lakini hata hivyo alipata majibu yake kwa maana maji yalitoka na watu wakanywa maji,ingawa hakutenda sawa sawa. Kesi hiyo ikabakia kati yake na Bwana ( Hesabu 20:8-12).Na hali ndivyo ilivyo leo,mtu ainaweza akajinyanyua katika kuomba kwake,na uaminifu wa Bwana, Bwana akaweka majibu. Lakini kesi itabakia kati ya mwombaji na Bwana.
Unyenyekevu ni suala la moyoni,Yesu alikuwa ni mnyenyekevu na anakutaka ujifunze kwake ( Mathayo 11:29). Yesu anafundisha kwamba unyenyekevu unahitajika katika kila kitu kwenye maisha yako,yaani unyenyekevu katika kuongea kwako,kutenda kwako,lakini katika kuomba ni vyema ukajengwa katika unyenyekevu. Mtu ambaye ni mnyenyekevu katika maombi ni yule ambaye hutambua kwamba Mungu ni mkuu na mkubwa kuliko yeye hivyo,ni lazima atashuka tu katika kuomba kwake.
Sasa,tunaomba mambo mengi sana lakini kama kutakosekana na kipimo cha unyenyekevu majibu hatuwezi kupoke kikamilivu. Kwani unafikiri Yakobo alikuwa ameandikaje kwenye eneo la maombi akihusisha “ unyenyekevu ” ? Anasema;
“ Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” Yakobo 4:2-4
Moja ya kuomba vibaya ni kukosa unyenyekevu. Kwa maana aliyekosa unyenyekevu ana kiburi, mtu atakaye kupata majibu na kutumia atakavyo yeye. Biblia inasema maombi yake hayajibiwi “ hata hapati” Jifunze neno hili, kwamba unyenyekevu ni siri kubwa katika kujibiwa maombi yako. Kukosa kunyenyekea wakati uombapo uonesha kiburi, na hali ya kujiweza. Na ikiwa unajiweza kwa nini kuomba? Si uendelee na maisha yako? Unyenyekevu ni muhimu kwenye maombi yako.
Nini kifanyike ili niweze kunyenyekea wakati niombapo?
Kumbuka,unyenyekevu ni kazi ya Roho mtakatifu. Yeye ndiye haswa mwenye kuwezesha mtu kuwa mnyenyekevu. Hivyo,omba kwake akuvike unyenyekevu kama vazi ili kusudi ujue namna utakavyotumia muda wako wa maombi huku ukinyenyekea. Kuna mahali hatujibiwi kwa sababu tunajiinua mno,tumejawa na kiburi tabia ya shetani.
Ni kwa Roho mtakatifu tu,ndipo kuna hali ya kuwezeshwa. Hata hivyo jifunze sana kwa Yesu, ukiomba,uraweza kupewa unyenyekevu.
Ikiwa umebarikiwa nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja.
Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa +255 683 877 900
Na.Mch. G.Madumla
Whatsapp namba +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments