NAMNA YA KUMREJEZA ALIYEKOSA.
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 29, 2019
- 5 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi.
Hakuna mtu asiyekosa katika duniani hii. Hata yule unayemwona mzuri ujue anamakosa mengi tu. Hivyo si jambo la kushangaza kumwona mkosaji bali ni jambo la kawaida. Swala la muhimu ni kujiuliza Je aliyekosa anarejezwaje? Mungu anajua tabia ya mwanadamu jinsi ilivyo, kwamba ni tabia ya kukosa. Ukitafakari jambo hili kwa kumwangalia Adamu kama kiongozi wa familia,utagundua kwamba na Yeye alikosea,. Kukosea kwa Adamu kunaonesha tabia halisi ya mwanadamu, ;
lakini pia kunaonesha viongozi na wenyewe wanakoseaga. Ebu chunguza kwa ukaribu pale Adamu alipokosea, Mungu alimpa nafasi ya“ kutubu ” kama mlango mkubwa na wa maana ili kupitia toba Adamu aweze kurejea upya. Lakini hata hivyo Adamu hakutubu chochote badala yake akaanza kumlaumu mwanamke aliyeshirikiana kukosea. Mungu anamsubiria Adamu aseme “nimekosea Ee Mungu, kwa maana nimekula tunda la mti uliotuagiza tusile, nisamehe” lakini hakutubu na hatimaye adhabu ikawa ni sehemu yake.
Na ndio shida kubwa tuliyonayo wengi, tunashindwa kurejea kwa kuwa hatuombi msamaha wakati tuliyemkosea amekaa akisubiri tuombe msamaha kwake, na hatimaye tunajikuta kwenye madhara makubwa. Katika fundisho hili la leo, tunaangazia haswa namna ya kumrejeza mtu aliyekosa katika dhambi au kosa lolote akiwa katika kundi.
Panapo kusanyiko la watu zaidi ya watatu basi makosa yapo pia kwa kuwa hamfanani kila mmoja. Wakiwepo walokole 5 tu, ujue mmoja anaweza akawa mkosaji kati yao, au wakakosana wenyewe kwa wenyewe kwa jambo dogo sana. Hii inatuonesha makosa hayana budi kuwepo lakini je unayashughulikia vipi? Biblia inasema nini katika hili; “ Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.“ Wagalatia 6:1
Watu walioitwa “ndugu” katika andiko hili, ni wale waaminio;(yaani kaka na dada katika Kristo). Unapookoka u ndugu na mwenzako aliyeokoka, undugu wenu si wa damu na nyama/mwili bali ni wa roho ndani ya Kristo. Sasa, neno linaitaka jamii ya waaminio ( labda kanisa, au kikundi cha ibada / fellowship), kujua namna ya kumrejeza mkosaji na mtenda dhambi mmoja ambaye naye ni ndugu katika Bwana.( Kumbe mkosaji ni lazima atakuwepo ndani ya kanisa au jamii ya waaminio.)
Utaratibu stahiki unaelezwa vyema namna ya kushughulikia suala hili la kumrejeza mkosaji. Lengo kubwa si kumpoteza mkosaji bali kumrejeza! Ikiwa “kumrejeza mkosaji ” ndio lengo mama katika kundi, basi lazima tukubaliane ya kwamba kutakuwa na kazi ya ziada kutekeleza zoezi hilo. Kwa maana yeyote anayefanya kazi ya kurejeza mkosaji, ni sharti akubali kushuka hata kudharauliwa ili ampate mkosaji. Biblia inatuambia wewe wa rohoni unapaswa kumrejeza mtenda dhambi “kwa roho ya upole” kumbe!
Kulikuwa na kijana mmoja alitenda dhambi ya uzinzi na binti mmoja. Na matokeo ya dhambi hiyo, binti akapata mimba. Sasa, jamii ya waaminio wakamsukumia mbali huyu binti na kumwona mhuni, wakamwita na majina mabaya. Yule kijana akaamua kujitenga na ushirika huo. Binti alipoona masimango yanazidi akaamua aende kutoa mimba😭😭😭🏃🏃🏃🏃
Kwa neema ya Mungu, mchungaji mmoja alitokea na kukutana na huyu kijana. Wakaanza mazungumzo, mchungaji alimsihi sana kwamba wasije wakatoa mimba. Kijana akawa amechanganyikiwa kwa maana hakutaraji kuwa baba hali yeye anasoma, na yule binti naye anasoma. Hivyo alivyotoka kwa mchungaji akawa akienda kunywa pombe, akawa na stress!!!
Mchungaji akamtafuta na kuhakikisha anakuwa naye karibu, mchungaji alipoona huyu kijana amekosa ukaribu wa rafiki zake akamfanya rafiki na kumchukulia taratibu ili aweze kueleweka sana. Na hatimaye alimpata vyema, wakasimamisha mpango wa kutoa mimba. Mtoto wakazaa, na mchungaji alifanikiwa kumrejeza kijana na binti kwenye kundi, nao wakaanza na moja na Bwana.
Haikuwa rahisi kabisa, mchungaji kuacha baadhi ya ratiba nyingine na kushughulika na kijana tena wakati mwingine alijifanya naye kama kijana ili apate kueleweka vyema. Hii ndio gharama ya kumrejeza mtenda dhambi, huu ni mfano tu wa kujifunza. Si lazima uwe mchungaji ndio umrejeze mkosaji bali hivyo hivyo ulivyo sasa, waweza.
Katika andiko letu Wagalatia 6:1 tunaona kundi maalumu la watu walioelekezwa katika kazi ya kumrejeza aliyetenda dhambi na makosa. Kundi hili la watu wanaitwa “watu wa Roho”. Neno hili linalotaja watu ni msamiati kwa maana nini hasa maana ya “ninyi mlio wa Roho” lina maana gani? Au “wewe uliye wa Roho ” ina maana gani?
Neno “ mtu wa Roho” humanisha mtu anayeishi akiongozwa na Roho mtakatifu. Au ni yeyote yule aliyeokoka mwenye hofu na Mungu. Mtu wa namna hii anapaswa kujua namna ya kumtafuta mkosaji na kumrudisha kwenye kundi kwa roho ya upole. Hivyo katika kundi, pale mmoja anapotenda dhambi au kukosea kwa jambo lolote, wewe uliyeokoka unatakiwa umrejeshe mtu huyo sio na wewe unamtokomeza azidi kupotea. Kwa maana wapo wapendwa ambao wenyewe kazi yao ni kumsukumia mbali mkosaji, hawaelewi ya kuwa ni wao wanaotakiwa wamlete karibu mkosaji.
Si vyema kumkemea mkosaji isipokuwa inapobidi. Biblia inakutaka kama kiongozi kutumia hekima ili ufanikiwe kumrejeza mwenye makosa. Ikiwa kama kiongozi akishindwa kumrejeza mkosaji, basi ni dhahiri hana sifa ya kuwa kiongozi kwa maana moja kati ya sifa kubwa ya kiongozi ni kukumbatia akiwarejeza waliokosa. Mambo yafuatayo yanaweza yakawa ni msaada mkubwa wa kumrejeza huyo mkosaji;
01. Maombi.
Mtu wa Roho anapaswa kumwombea yule mkosaji kabla ya kuongea naye kwa sababu maombi yakitangulia yatalainisha maongezi yenu mtakayoyafanya. Maombi ya awali juu ya mtenda dhambi yanagusa moyo hata kuleta amani kabla ya mazungumzo yenu. Hivyo maombi ni mlango mkubwa wa kumrejesha mkosaji. Wakati mwingine unaweza ukawa hujui namna gani utakayoitumia ili kumrejeza aliyepotea.
Lakini ukiomba kikamilifu utaiona njia sahihi utakayoitumia. Wakati mwingine mkosaji ni mkali na anajitetea sana kiasi kwamba haoni kosa lolote ingawa amekosa sana. Sasa mtu kama huyu huwezi kumwendea bila kuomba, unahitaji kuomba na kumwombea kabla ya kuonana ili kibali kiachiliwe wakati mtakapoonana kwa mazungumzo.( Lakini uombe mtakapokutana pia) N. K
02. Mwone kana kwamba hajakosea. /chukuliana naye.
Hii ni tabia ya Mungu na ndio tabia ya Yesu. Wakati mimi na wewe tulipokuwa dhambini, wakosaji wakubwa hapo ndipo Mungu hakuhesabu makosa yetu na aliweza kutuchukulia jinsi yulivyo. Yesu aliwaona wenye dhambi kana kwamba hawana dhambi ili apate kuwarejesha. Kama Yesu angeliweza kuwahukumu, au angewaona watu wenye dhambi ni wabaya na wamekosa sana.
Basi wokovu usingelikuwepo. Kwa hiyo hata wewe ungeliangamia. Lakini aliweza kuvhukuliana nasi, na ndivyo nawe umwone huyo kana kwamba hajakosea. Ninajua ni ngumu jambo hili, lakini linawezekana na unapaswa kufanya hivyo sasa. Ukiweza kumwona mkosaji katika mtazamo huu, basi utampenda, na utaweza kuchukuliana naye.
03. Zungumza naye kwa upole, ukijua na wewe siku moja ulikuwa mkosaji.
Ili umrejeze mtu kundini unahitaji hekima ya juu sana. Ndio maana ni lazima uombe kwa Roho mtakatifu akusaidie. Kabla ya kuzungumza naye, jiulize ; Namna gani utaanza na namna gani utamalizia? Akikataa kukubaliana na wewe utachukua hatua gani? Je utafanya nini ili upate kueleweka vizuri? N. K mwenye hekima mara nyingi katika mazungumzo uanza na simulizi, au kujielezea yeye kuwa alikosea zaidi ya hayo. Mwenye hekima humpa nafasi ya kutosha mkosaji /aliyegafirika ajieleze. Kumbuka hili; kadri mkosaji anavyoendelea kuzungumza ndivyo anavyotua mizigo yake na ndivyo inavyokuwa rahisi kumsaidia. Kumbuka lengo ni kumrejeza kundini.
Kumbuka;
Kila kiongozi kwenye kundi au kila mtu kwenye kusanyiko hana budi kumfikiria yule aliyegafirika katika kosa lolote. Ukitumia upole kushughulika na aliyegafirika, basi ujue utampata tu. Hata kama itachukua muda kumpata aliyepotea dhambini, lakini utafanikiwa.
Tatizo lililopo leo;watu wa Roho ni wakali sana kiasi kwamba wengi hifikiria ukali kama kigezo cha kurejeza watu ingawa huwezi kutumia ukali kwa kumrekebisha mtu. Laiti kama utajua kwamba huduma ni mali ya Kristo basi utajifunza kuwa kama Kristo mtu aliyeona si kitu kuchukua nafasi ya Mungu akanyenyekea akawa mtii ( Wafilipi 2:9-11)
Si vyema ikiwa mtu amekosea, basi kumwanika na kulifanya kanisa lote lijue kwamba amekosea. Si vyema ikiwa mwanakwaya amekosea basi ndio uifanye kwanya yote itambue kosa lake. Ni vyema kama kiongozi kutumia hekima na kufuata njia zilizoanishwa hapo juu ili umpate huyo aliyekosea. Biblia inasema ikiwa kama kuna watu “wanaodumu kutenda dhambi”, basi watu hao wakemewe mbele ya wote ili wengine waogope na kujifunza kupitia kwao ( 1 Timotheo 5:20)
Kwa msaada zaidi +255 683 877 900.
Whastapp+255 746 446 446 .
Mch G. Madumla
UBARIKIWE.
Comments