USIWE KWAZO.
- Mch. Gasper Madumla
- Aug 27, 2019
- 3 min read
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa kifupi,
Usiwe kwazo / Never be a stumbling block !
“Kwazo” ni mfano wa jiwe au kitu fulani kinachosababisha mtu aanguke au azuiliwe katika kitendo cha makusudi yake. Lakini pia “ Kwazo” ni pingamizi au kizuizi,kigingi cha kumwangusha mtu asisonge mbele. Mtu anaweza akawa kwazo kwa mwingine katika maneno, ishara au matendo yake. Mfano;
a) “ Kwazo kwa njia ya maneno ” mtu anaweza akawa anazungumza maneno ambayo kwa kweli yanaumiza moyo, kiasi kwamba yeye asikiaye hujikuta akibeba uchungu,na hatimaye kuangukia dhambini,Lakini chanzo chake ni maneno tu ya mtu mmoja.Ujawahi kuona mtu anayetumia kinywa chake vibaya. “Badala ya kujenga yeye hubomoa” na bahati mbaya hadi watumishi wa Mungu wa siku za leo,wamewakwamisha waamini wengi kwa maneno ya vinywa vyao! Ukumbuke;Kutumia kinywa vibaya,ni kufanyika “kwanzo” kwa watu wengine. Ukichunguza matumizi ya kinywa chako kwa undani,waweza kugundua kwamba kuna mahali labda umewakwaza watu wengine kwa kujua au wakati mwingine pasipo kujijua. Ni bora uwe unajua kwamba umemkwaza mtu ili umwendee kutengeneza naye,lakini ni mbaya pale ambapo unamkwaza mtu halafu wala hujui kama unakwaza mtu kwa sababu hawezi kutengeneza naye!!!
b)“Kwazo kwa njia ya ishara” Watu wengine hawana maneno maneno bali ni watu wanatumia sana lugha za picha kama vile kung’onga,kuzomea,kusodoa,kukonyeza,kufyonza,kukunja uso,kuigiza kwa ishara n.k hayo yote yanapofanywa dhidi ya mtu,mtu huyo akiona au kusikia ujue atakwazika tu,na kujiuliza “ kwa nini ananingonga? Kwa nini ananidharau kiasi cha kunifyonza? ” Wewe fikiria mtu anapotumia ishara moja wapo ya hizo juu yako,utajisikiaje? Hivyo kwazo linaweza kufanywa kwa njia hizo za ishara mbaya dhidi ya mtu au watu. Kuna watu ndio zao kufyonza,yaani kitu kidogo tu yeye ni kufyonza mwanzo mwisho!!! Ni tabia mbaya ya kumkwanza mtu.
c) “ Kwazo kwa njia matendo ” Wapo watu wanaoongea kidogo lakini wanatenda sana, wanajulikana kama watu wa vitendo / men of action. Ili akukwaze,basi anakutafutia tendo fulani baya,na hapo unakwazika! Fikiria tendo kama la “usaliti” jinsi linavyoumiza moyo,usaliti ni tendo linaloweza kumkwaza mtu kiasi cha kuchukua maamuzi mabaya!!! Lakini kuna watu wanakwaza wengine kwa matendo tu pasipo kuongea wala kuwa ishara. Fikiria namna mtu anavyoweza kukwazwa katika usafili wa uma kama huku kwetu Dar Tanzania. Pale daladala linapojaza watu wengi kupitiliza kiasi cha abiria kukanyagana na kushikana sehemu nyeti. Halafu hapo ndipo mmoja utakuta akisema “ kwa nini unanibaishia?!! Ukome,nasema ukome!!!!” sasa mtu wa watu hata hujafikiria kufanya ujinga huo,lakini utafanyeje ikiwa ndio usafili wenyewe? Kwa hiyo kuna matendo mengi yenye kukwaza sana!!!
Moja ya jambo kubwa ambalo Yesu alilifundisha lilikuwa juu ya makwazo,ambayo hatutakiwi kuwa sehemu yake. Na amelipa uzito mkubwa sana kuonesha mkristo hapaswi kuwa kwazo kwa namna yoyote ile. Kwenye Luka 17:1-2,Yesu amefunua adhabu itakayompata mtu yule atakayekuwa kwazo,biblia kwanza inasema;“… Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa.“
Hii ni sawa na kusema,mtu yeyote atakayemkosesha mwamini mpya katika wokovu,mtu huyo ni bora afe ( Kwa maana kitendo cha kumfungia jiwe la kusagia shingoni na kutupwa baharini ni sawa na kufa,kwa maana hakuna adhabu kubwa kama hiyo,isipokuwa ni kifo tu)
Biblia inasema tena;“ Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe;” 2 Wakorintho 6:3 Hii ni kwako mtumishi wa Mungu, Je utumishi wako ukoje? Je unawakwaza watu? Ukumbuke kwamba; wakiwepo watu ambao kweli kabisa wanaolalamika juu yako kwamba unawakwaza,basi ujue utachapwa na Bwana vikali! Chunguza utumishi wako ukoje!!!
Tokeo la kwazo;
Uchungu – uchungu ni moja ya tokeo baya la kwazo linapoachiliwa kwa mtu. Wengi wanapokwazika ujikuta wakianza kubeba uchungu kwa kuwashikilia watu. Ukumbuke; uchungu ni mlango wa magonjwa mengi kwa maana ni mlango wa mapepo!
Hasira – ni zao la kwazo,mtu ayekwaza hupanda hasira sana!
Kisasi – ni mtoto wa hasira!
N.K
Maswali ya kujiuliza;
Watu wengine hawafahamu kwamba wamekuwa makwazo makubwa kwa watu wengine. Wakidhani kuwa wao wapo salama,lakini ni vyema wakajiuliza maswali ya msingi kujua nafasi zao zipoje. Hata wewe ni vyema ukajichunguza kwa kujiuliza maswali yafuatayo kucheki kama u kwazo au la?
Je wewe ni mwongeaji sana pasipo sababu ya maana kiasi cha kumfanya mwingine ajisikie vibaya hata kulia na kumwingiza dhambini ( mfano wa wana ndoa ambao hawawezi kunyamaza bali kitu kidogo yeye ni kuongea usiku kucha!)
Je maisha yako yamewazuia watu kuokoka? ( Je imefika wakati ambapo wasio okoka wakiona maisha yako wewe uliyeokoka,basi wao hawawezi kuokoka na hatimaye husema “ hakuna wokovu kama ndio maisha haya“)
Je umewahi mara ngapi kutumia lugha ya picha/ishara hata ukafikia wakati mtu akaamua kupatwa na uchungu?
N.K
Dawa ya kwazo;
Pendo – Tunda la Roho “ pendo” ndio dawa haswa la kwazo,kwa maana katika pendo kwanzo halina sehemu. Biblia inasema “ Wana amani nyingi waipendao sheria yako,Wala hawana la kuwakwaza.“ Zab.119:165. Watu waipendao sheria ya Bwana, ni wale hasa walio ndani ya pendo,hao hakuna la kuwakwaza wala wao hawawezi kuwa kwazo!
Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe. Na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa+255 683 877 900
Whatsapp namba +255 746 446 446
Mch. G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments