TOSHEKA NA MSHAHARA WAKO.
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 23, 2020
- 3 min read
Updated: Sep 30, 2022

Wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa,Neno la Mungu lilimfikia Yohana mwana wa Zakaria,akiwa jangwani. Naye Yohana tangu wakati huo,akaanza kuhubiri juu ya ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi. Yohana alifahamika kwa kazi yake,naye huitwa Yohana mbatizaji,mtu shupavu,aliyejazwa Roho mtakatifu tangu tumboni mwa mamaye,mtengeneza njia ya Bwana.
Yohana, aliulizwa maswali mengi na kuyatolea majibu yote wakati akiwa kwenye kazi yake ya kubatiza. Moja ya swali muhimu aliloulizwa na askari ni hili “ sisi ( askari ) nasi tufanye nini?” Luka 3:14. Naye akawajibu,akawaambia;
“…Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu.” Luka 3:14
Bila shaka Yohana alijua dhuluma iliyokuwa ikifanywa na askari, tena alijua kwamba askari walikuwa wakiwaonea raia kwa kuwashtaki kwa uongo,na kisha alijua kuwa askari hawatosheki na mishahara yao,na ndio maana ilimbidi awaambie ukweli.
Kumbe suala la baadhi ya watumishi wa serikali kukosa uaminifu kwenye kazi zao halikuanzia leo,isipokuwa lilikuwepo tangu enzi za Yohana mbatizaji. Tangu enzi hizo,kulikuwepo na watumishi baadhi yao wa serikali waliokosa uaminifu hata wakawa ni “wazulumati,wapendao rushwa,wenye kupotosha kweli,wenye uchu wa mapato ya aibu”
Askari wa kipindi kile walikuwa wakilipwa kwa maana ni watenda kazi wa kiserikali ( dola tawala),
lakini hata hivyo walikosa uaminifu na maadili sahihi ya kazi zao,mbaya zaidi “hawakutosheka na mishahara yao” hii inatupa picha kwamba,askari hawa walikuwa ni watu wenye uchu,njaa ya wizi na kuzulumu raia na mali zao,lakini pia walikuwa ni wapiga “dili” .
Askari anayetajwa hapo amevaa uhusika wa mtu yeyote anayefanya kazi ya kuajiliwa ama kujiajili. Neno hili “ utosheke na mshahara wako ” linakuhusu na wewe usomaye.
Lakini ukweli ni kwamba hata kama askari/mwajiliwa akiongezewa mshahara mara mbili ya mshahara wake, hata hapo bado hawezi kutosheka. Kwa maana kadri ya fedha inapoongezeka na matumizi ya mtu huongezeka,kwa hiyo dawa ya kutosheka si tu kuongeza mshahara bali kutosheka ni jambo la moyo.
Jiulize,ni wangapi wamepandishwa mshahara lakini mbona bado ni majizi ya kupindukia? There is something else ! Ni muhimu kujua kwamba, Mungu anachukia dhuluma,na uonevu wa aina yoyote ule.
Kwa nini watu hawatosheki?
Ukweli ni kwamba mwanadamu ana tabia ya kushindwa kutosheka kwa jambo lolote lile. Mwanadamu wa asili (aliye mbali na wokovu) kamwe hawezi kutosheka kwa chochote akipatacho. Kwa sababu tamaa za mwili zi juu yake ,kutamani visivyofaa!!!
Nafsi ya mtu wa asili,haishibi hata bali tamaa inampelekesha tu siku zote. Ebu licheki jambo hili katika kazi ya mikono yako hapo ofisini,uone kama watu wa namna hii wanaweza kutulia kwa kutosheka wakipokeacho? Cheki,tena hata kwenye ngazi ya ndoa Je kuna kutosheka na uliye naye ikiwa kama ni mtu wa asili? Utagundua hakuna hali ya kutosheka kwa maana,mwili hutamani zaidi. Ikiwa mwili upo juu ya roho,kamwe huwezi kutosheka.
Hii ina maana mtu anayeongozwa na mwili,hawezi kutosheka hata iweje!!! Kwa hiyo,watu hawatosheki kwa sababu wanaongozwa na ( tamaa za) mwili.
Na ndio maana hata kama mtu akipewa mara dufu,lakini bado atatoka nje na aibe kidogo. Wengine kwenye ngazi ya ndoa,wamepewa watu sahihi,wazuri lakini bado haridhiki,kwa maana bado yupo na maongozi ya kimwili!!!
Je askari/ mtu aweza kutosheka na pato lake?
Ndio,askari anaweza akatosheka na mshahara wake,ikiwa kama atakuwa mwadilifu wa moyo. Kuwa mwadilifu wa moyo kunahitaji msaada wa kiroho zaidi,kwanza “kuokoka” ndio msaada mkubwa na wa kwanza wa kiroho. Ukiokoka na kufuata misingi ya wokovu,kamwe huongozwi na mwili tena,bali unaongozwa na Roho.
Tena, huyo Roho mtakatifu hawezi kukutia chini ya tamaa za mwili,hivyo unamwitaji sana. Kwa hiyo, Uwezekano wa kutosheka na mshahara kama mshahara upo mkubwa,ikiwa moyo wako “utatahiriwa“
Je kuna madhara ya kutokutosheka ?
Moja ya dhara kubwa la kutokutosheka ni “wizi” kwa maana wizi huja kwa sababu mtu hufikiri hajatosheka na alichonacho,Wizi,ni tabia ya shetani ( Yoh.10:10). Lakini Yohana anataja mambo mawili muhimu ambayo na yenyewe ni matokeo ya kutokutosheka,
“ kudhulumu na kushitaki kwa uongo” haya mawili ni matokeo ya mtu asiyetosheka. Kawaida ya mtu asiyetosheka,lazima atakuwa ni mtu wa dhuluma/mjanja mjanja fulani hivi,lakini huyo huyo hakosi kuwa mwongo,tena uongo wake ni wa kushtaki kwa mabosi,kwa maana moyo wake unawaka uovu unaotokana na hali ya kutotosheka na mshahara wake. Tena dhara jingine ni “wivu wa kijinga jinga” kwa maana akiona cha mtu,basi moyo wake unaumia lakini kumbe mwenzake amejitoshekea!
Ukumbuke;
Kuna watu hawapati hicho unachopata wewe sasa,hivyo ukipoteza hicho utajuta sana.
Adui,ibilisi ndiye aujazaye moyo wa mtu hata kuona anachopata ni kidogo,na sasa aende kutafuta kingine.
Anayekupa wewe,aweza kukunyima akiona tabia ya kutoridhika. Itamuumiza ( hata kwenye ngazi ya ndoa, ikiwa mwenzako anajitahidi akupe,lakini wewe unaona si kitu akupacho,ujue utamvunja nguvu,kesho aweza asikupe)
Toba inahitajika na uchukue hatua ya kumpokea Bwana Yesu,akusaidie na hali hiyo.
Ikiwa kama umebarikiwa,nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja. Kwa msaada zaidi na MAOMBI piga sasa kwa + 255 683 877 900
What’s app namba + 255 746 446 446
Na. Mch.G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comments