USITENDE NENO LOLOTE KWA KUSHINDANA WALA KWA MAJIVUNO.
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 12, 2018
- 3 min read

Na mch. Gasper Madumla
Bwana Yesu asifiwe….
Kwa ufupi…
Kuna watu ambao wana tabia za kurithi(Hulka),au za makuzi yao. Ambapo katika tabia hizo ni mbaya sana kwa sababu hazitokani na Mungu bali shetani. Wapo watu ambao ni wabishi kupindukia yaani utakuta hata ukimuonesha rangi nyekundu bado atakubishia akikuambia sio nyekundu bali ina mchanganyiko na nyeusi! Yaani basi tu ili mradi abishe bishe hivi,ndipo asukie furaha. Sasa bora watu wa namna hiyo,kuliko watu wa mashindano na majivuno hao ndio hatari.
Kwa sababu watu wa namna hiyo wapo tayari hata kukubali kupoteza muda au pesa katika kushindana kwa vitu ambavyo havina mbele wala nyuma tena havina Mungu ndani yake! Paulo mtume alipoona hasara ipatikanayo katika mazungumzo mabaya ya mabishano alimuandikia mapema mwanaye wa kiroho Timotheo akimtaka akatae mambo yasiyokuwa na Mungu ( 1 Timotheo 4:7)
“Kushindana na majivuno” ni moja ya mambo ya kuyakimbia,kuyakwepa. Mambo hayo hayo anayoambiwa Timotheo ndiyo unayoambiwa wewe leo. Lakini cha ajabu badala ya kuyakimbia, eti ndio unayoyakimbilia!!! Au badala ya mtu kukimbia dhambi lakini utakuta ndio anayeikimbilia.
Mojawapo ya tabia mbaya ni tabia ya kushindana pamoja na tabia ya majivuno. Ni tabia pandikizi za shetani ndani ya mioyo ya watu,kwa maana hatukuumbiwa kushindana shindana wala hatukuumbiwa majivuno. Tabia ya kushindana ni tabia ya kutaka mambo yako tu ndio yasikilizwe,ubinafsi,ubishi hivi,kutokukubali ushauri au mambo ya mwengine. Mtu anayeshindana ana shida kwa kweli na ni kero kwa wengi kwa sababu chochote kinachotolewa na wengine hukataa na kutaka ya kwake tu ndio yakubaliwe au ya sawa. Ebu jichunguze ndugu yangu uone kama una tabia ya kushindana.
Mpendwa,Neno hili ni lako! Unapotenda neno lolote jaribu kumtanguliza mwenzako kwanza. Na umuone mwenzako ni bora,tena umuone ni wa thamani,umuone kwamba anafaa. Hivyo ukimuona mwenzako namna hiyo basi ni dhahiri hutaweza kushindana naye katika neno au jambo lolote lile. Biblia inasemaje katika jambo hili;
“ Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.” Wafilipi 2:3
Biblia haikunyamaza katika hili kwa sababu mambo ya kushindana na kujiona bora ni mambo ya kishetani. Lakini leo cha ajabu watu wapendwa ndio watu wa kushindana,utakuta kanisa fulani likishindana na kanisa fulani,mchungaji fulani akishindana na mchungaji fulani,mpendwa fulani akishindana na mpendwa fulani. Yaani badala ya mkristo akishindana na ibilisi sasa imekuwa mkristo kwa mkristo!!! Ni aibu.
Majivuno yameingia kwa kasi makanisani kwa namna ya ajabu kiasi kwamba wengi wamejikuta wakijivunia vipawa vyao,wakijivunia utajiri wao. Hii ni mbaya sana!!Ukiweza kumuhesabu mwenzako kama ndugu,basi hapo ni dhahiri kabisa hutaweza kushindana naye wala majivuno hatakuwa kwako katika Jina la Yesu Kristo.
Mara nyingi watu wanaopenda kushindana ni wale either hawana kazi maalumu ya kufanya au shetani amewatawala. Kwa sababu mwenye kazi maalumu hakubali kupoteza muda. Unajua kushindana na majivuno si tabia tena bali roho inayowatesa wengi sana.
Mungu anapendezwa sana na unyenyekevu,ndio maana imeandikwa “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.” Wafilipi 2:3. Daraja zuri la kuinuliwa ni kuwa na unyenyekevu wa moyo.
Je sasa ninawezaje kuacha tabia ya kushindana?
Omba toba,akimsihi Mungu akusamehe makosa yako yote.
Ni lazima uombewe yamkini kama kuna vifungo,vifunguliwe.
Hakikisha unakubali mambo ya wengine na yaheshimu mawazo ya wengine.
Kubali kushuka na uwahesabu wengine kuwa bora,ili uweze kuwasikiliza na kuwajali.
Somo hili ni pana sana kwa mujibu wa biblia,lakini kwa ufupi tu ni hayo. Waweza kunipigia simu zangu zilizopo hapo chini ili ujifunze zaidi. Na kwa maombezi piga sasa
Piga sasa kwa +255 683 877 900
Namba ya what’s app ni +255 746 446 446
Mchungaji Gasper Madumla.
UBARIKIWE
Comments