USISHINDWE NA UBAYA
- Mch. Gasper Madumla
- Apr 26, 2017
- 2 min read
Updated: Sep 5, 2022

Ni jambo jema tena lakupendeza kwamba usilipe baya kwa ubaya bali uushinde ubaya kwa kulipa jambo jema. Ujumbe huu ni kwa ajili yako wewe uliyetendewa ubaya! Tazama kisasi ni kazi ya Bwana Yeye Bwana atalipa kwa maana ndivyo ilivyoandikwa (Warumi 12:19).
Kumbuka ya kwamba “ubaya” ni roho ya shetani, hivyo kwa kuwa umetendewa na ubaya,wewe usilipe kwa ubaya ukitambua ya kwamba ubaya ni tabia na ni roho ya shetani.
Roho wa Bwana akusaidie usijilipize kisasi katika kila jambo baya unalotendewa,ujue ya kwamba ikiwa watakutendea au wamekutendea wewe basi wamemtendea pia na Mungu aliyekuumba jinsi ulivyo. Hivyo rudisha moyo nyumba usiwatendee mabaya,bali mema ili kusudi Mungu wako atukuzwe kwa hayo mema.
Tabia kubwa ya shetani ni kutenda ubaya siku zote. shetani hana wema hata kidogo,sasa ukimuona huyo anayekutendea mabaya basi ujue si yeye haswa! bali shetani yupo ndani yake ndiye atendaye,kwa maana mtu huyo hajui atendalo. Bali tabia ya Mungu ni kutenda wema,nawe ukiwa mtoto wa Mungu huna budi kutenda mema kama Baba yako wa mbinguni atendavyo. Jifunze kwa watumishi wa Mungu waliotendewa mabaya bali wao hawakulipa baya kwa baya bali baya kwa wema. Biblia inawaelezea watumishi waliofanikiwa kusamehe kwa kulipa jema.
Mfano; Jifunze kwa habari ya Stefano alipopigwa kwa mapigo mengi,lakini angalia asemavyo
;“ Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu.Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.” Matendo 7:59-60
Andiko hilo linatufundisha tusilipe baya kwa baya bali baya kwa wema. Kwa sababu Stefano hakulipa baya kwa baya bali kwa wema,kwa maana alipopigwa kwa mawe katika hali hiyo ya maumivu mengi na kuumia sana ndiposa hakutaka kuwaombea adui zake mabaya kwamba labda waangamizwe wote kwa moto utokao mbinguni bali tunamuona akisema “…Bwana, usiwahesabie dhambi hii...” Matendo 7 :59.
Stefano aligundua kwamba watu waliompiga walitenda dhambi ya kustahili kuhukumiwa kifo,lakini hakudiriki kuomba hukumu hiyo iwashukie bali akawaombea wasamehewe. Angalia jambo alilolifanya Stefano,hakulipa baya bali wema. Je ungelikuwa wewe ndio Stefano ungeliweza kumuomba Mungu awasamehe adui zako wanaokupiga? Au utatuma moto na kuwaangamiza? Utajijibu wewe mwenyewe!
Ni kweli umetendewa ubaya,tena ubaya mkubwa kiasi kwamba wamekuumiza moyo wako lakini kumbuka kurudisha moyo nyuma kwa kutokutenda baya. Unajua siku zote ukitendewa ubaya kisha nawe ukalipa ubaya basi nawe unahesabika ni mbaya! Ni sawa sawa na msemo wa kiswahili usemao ukimkimbiza chizi nawe utaonekana ni chizi! Ukweli ni kwamba huwezi kuishi bila kutendewa mabaya,sasa ishu sio kutendewa bali ishu ni namna gani wewe unatenda.
Thamani ya imani yako itakamilika kwa kutokulipa ubaya kwa adui zako.
Mimi naomba Mungu akupe moyo wa msamaha kusudi uwasamehe waliokukosa. Kwa sababu ukishindwa kuwasamehe/kumsamehe basi utaangukia katika kulipa kisasi tena utaangukia katika mateso ya chungu na ghadhabu.
Usilipe baya kwa ndugu huyo,bali wewe muhesabu tu kama mkosa wa kawaida kisha msamehe na endelea kumuombea mema kusudi Mungu amrekebishe huyo. Hivi unajua kama unataka kulipa baya,huwezi kuwa na kipimo cha kulipa? Mwenye kipimo hicho ni Mungu tu. Mpende vivyo hivyo huyo anayekuudhi ( Warumi 12:20)
Inawezekana ukawa umeshindwa kabisa kuwasamehe,basi naomba unipigie kwa namba zangu hizo hapo chini,ili tuombe pamoja na uweze kuwaachilia na kutowalipa baya,
piga sasa kwa +255 683 877 900
What’s app number ni+255 746 446 446
Mch.Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comentarios