NITAKUTIA NGUVU.
- Mch. Gasper Madumla
- Jul 25, 2022
- 2 min read
Updated: Aug 26, 2022

“ usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”Isaya 41:10
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi,
Andiko hilo ni andiko muhimu sana kwako la kurejesha tumaini lililopotea kwa sababu yoyote ile kwa maana Bwana amehaidi mambo mazuri hapo. Moja ya jambo muhimu ndilo hilo asemalo “nitakutia nguvu “yaani nitakuimarisha,nitakusimamisha.
Ni dhahiri kabisa Bwana Mungu alikuwa akisema na mtoto wake Israeli baada ya kumwona kwamba amekosa msaada,na kwa sababu hiyo amepoteza kiasi cha nguvu ya kusonga mbele.
Kuna mazingira mengine ukipitia unajikuta huna nguvu ya kusonga mbele pamoja na kwamba unamwamini Mungu. Kupoteza nguvu ni hali ya kawaida hasa pale unapoachwa au kupitia changamoto ambazo huoni wa kukusaidia. Biblia inatuambia kuhusu Petro aliyefungwa gerezani akikusudiwa siku inayofuata atolewe na kuwekwa mbele ya watu labda kuuwawa kama alivyouwawa Yakobo. Biblia nasema Petro “alilala” katikati ya askari awili. ( Matendo 12:1-6)
Kutendo cha kulala katikati ya askari huku akijua kwamba amekusudiwa mabaya kesho yake,kinatuonesha ( labda Petro hakuwa na wasi wasi na Mungu wake,akijua Bwana atamtoa tu katika gereza) Lakini inawezekana kabisa pamoja na utumishi aliokuwa nao Petro,alipoteza tumaini na kushindwa kujua afanyeje,hatimaye kupoteza nguvu au tumaini.
Kwa maana ni vigumu kupata usingizi hali ukijua kesho unatolewa kuuwawa au kutendewa mabaya! Huo usingizi unatokea wapi!
Katika hali kama hiyo,ni rahisi kupoteza nguvu hata ya kuomba!
Hujawahi kupitia hali fulani ngumu kiasi kwamba hata hujui unaomba nini au inafika wakati unashindwa kuomba?
Ipo hali ya namna hiyo,lakini ukumbuke Neno hili,kwamba “Bwana atakutia nguvu” Kwa maana yupo pamoja na wewe,kama vile alivyokuwa na Petro ndivyo yupo na wewe. Biblia inatuambia Mungu alimwinulia Petro watu wa kumwombea nao wakaomba Kwa juhudi hatimaye Bwana akamtoa gerezani. Hata kwako itakuwa hivyo,Bwana atakuinulia waombaji ambao watakusimamisha mahali ulipo,nawe utatoka salama.
Ebu ona vile waombaji waliposimama na Petro kwenye maombi baada ya kuomba sana,Bwana akamtia nguvu Petro. Kuna watu hawatakubali upotee mikononi mwa adui,naye Bwana ataachilia nguvu kwako. Kumbuka ahadi hiyo, ( Isaya 41:10)
Hiyo ni ajenda yako ya kusimama nayo katika maombi kwa kumwambia Bwana “akutie nguvu” katika kipindi hiki kigumu unachopitia.
Naye Bwana kwa kuwa ni mwaminifu atakutia nguvu tu,na utashinda,amini tu,hili ni neno lako leo .Ni ahadi ya Bwana ya kukurejeza,kukuimarisha tena bila kujali nini kimekuangusha kwa maana wewe ni mali yake,ndio maana kamwe hawezi kukutupa. Hivyo usijikatae,kwa maana Yeye aliyekuumba hajakukataa.
Kuna kuinuka tena,na sasa ndio wakati wa kuinuka kwa upya.
Waweza kunipigia simu sasa ili tuombe pamoja,
piga kwa +255 683 877 900.
What’s app number +255 746 446 446.
Na Mch. Gasper Madumla
UBARIKIWE.
Comentários