top of page

MUNGU ATAKUOKOA / GOD IS ABLE TO SAVE YOU.

Updated: Sep 5, 2022


Yeye Mungu ni mwenye uweza wote katika Kristo Yesu, hajawahi kushindwa na lolote lile. Kile ambacho mwanadamu ameshindwa,kwa Mungu kinawezekana,tena kile ambacho wewe mwenyewe umeshindwa ujue kwa Mungu kinawezekana. Na kwa sababu hiyo anakutaka uamini hivyo na anataka umtegemee Yeye katika yote unayopitia.


Nataka leo niangazie maisha ya imani ya vijana wanne waliokuwa utumwani huko Babeli. Hawa si wengine bali ni akina Danieli na rafiki zake watatu. Maisha yao yaliwindwa na adui / watesi ili waangamie kabisa kwa maana walikuwa ni watu waliomwamini Mungu wa kweli na kukataa kuitumikia miungu. Haikuwa rahisi kukataa kuitumikia miungu wakati watu hao wakiishi kwenye utumwa! ( Kwa maana mtumwa hufuata bwana wake atakacho).

Kuna kipindi ambacho Nebukadreza alitengeneza sanamu na kuisimamisha na kuwataka watu wote waiabudu hiyo sanamu ( maana ilikuwa ni kawaida kuabudu sanamu),lakini akina Shadraka na wenzake walikataa wazi wazi,biblia inasema;


“Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili.Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme.Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.” Danieli 3:16-18


Waliamini kwamba Mungu aweza kuwaokoka na mkono wa Nebukadreza na wala hawakuwa na shaka,lakini walikuwa tayari hata kufa ikiwa kama Mungu hatawaokoa/ angewaacha,lakini wasiabudu miungu. Simulizi hii inatuonesha jinsi gani ujasiri na imani imara iliyopo ndani ya vijana hawa. Zaidi sana tunaona mkono wa Mungu uokoao ukitenda kazi. Jambo moja kubwa la kujifunza kupitia akina Shadraka ni kwamba ;


“ Mungu hawezi kumwacha mtu yeyote anayemkimbilia,anayemwamini bali Yeye atamwokoa” Zab.30:1. Habari hii imerekodiwa katika biblia kwa makusudi kuonesha Mungu aweza kuokoa,lakini wewe huna budi kuweka imani yako yote kwake.

Katika kila hali,mkono wa Bwana upo kwa ajili ya kuokoa. Suala Ni jinsi gani umekaa naye? Ni jinsi gani unamwamini?


Kama amewaokoa akina Danieli na wenzake kutoka kwenye kifo,Je hawezi kukuokoa katika ugonjwa huo? Je hawezi kuokoka katika janga unalopitia? Bila shaka anaweza. Changamoto iliyopo ni kwamba, imani yako ni haba kiasi cha kujiwekea mipaka ya kuokolewa! Hiyo ndio shida kubwa iliyopo. Mara nyingi umekata tamaa,na kuona kwamba haiwezekani kupona au kutoka katika hali hiyo,lakini ujue sivyo Mungu akutazamapo,Yeye ana mipango mema kwako.


Ujumbe huu,ni maalumu kwako kwa kubadilisha mtazamo wako juu ya Mungu anayeabudiwa. Ukweli ni kwamba hakuna la kumshinda Bwana, lakini katika matazamo mbaya usiofaa wengi tumejikuta hatuamini wokovu wa Bwana katika maeneo yote. Nikutie moyo,Yeye Bwana yupo hai kuokoa hata sasa,simama tu katika imani yako na utamwona Mungu.


Kumbuka, Musa alichowaambia Israeli walipokuwa wakitoka utumwani,alisema;“ Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.“ Kutoka 14:13-14 .Maneno hayo ndio Bwana asemayo kwako pia. Wokovu umeachiliwa tayari kwako,lakini imani yako pia inahitajika. “ maombi ” ni muhimu sana,katika hilo ulilonalo.


Natamani tuombe pamoja katika lile unalopitia sasa,kwa maana ninamwamini sana Mungu, kwamba atakuokoa tu,atakuponya tu,atakupigania katika hilo. Tafadhali,usisite kunipigia simu ili tuombe pamoja,na kwa ushauri wa kiroho.


Namba za MAOMBI ni +255 683 877 900

Na.Mch. G.Madumla


Whatsapp namba +255 746 446 446


UBARIKIWE.

Comentarios


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page