JIFUNZE KUTIA MOYO./ UNDERSTAND HOW TO ENCOURAGE ONE ANOTHER.👨👨👧👦👫💃
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 11, 2019
- 4 min read
Updated: Sep 5, 2022

“ Wakasaidiana, kila mtu na mwenzake, kila mtu akamwambia ndugu yake; Uwe na moyo mkuu.Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike.“ Isaya 41:6-7
Katika maandiko haya tunaona aina tofauti ya mafundi kama vile Seremala, mfua dhahabu, fundi wa kulainisha kwa kutumia nyundo, na fundi mtaalamu wa kuunganisha . Watu wote hawa walikuwa na taaluma tofauti tofauti. Biblia inasema“ Wakasaidiana kila mtu na mwenzake “. Ingawa taaluma zao zilikuwa tofauti lakini waliweza kusaidiana kila mmoja.
Kumbe, tofauti tulizonazo za taaluma sio tatizo la kutokusaidiana, tunaweza tukasaidiana kila mmoja.
Tatizo lililopo leo lipo hapo hapo kwenye “kusaidiana” utakuta mwalimu hawezi kumsaidia mkulima kwa maana anadhani akimsaidia mkulima, huyo mkulima atampita. Au fundi Seremala hawezi kumsaidia fundi ujenzi akidhania fundi ujenzi atamzidi kete kujua akifanyacho.
Lakini biblia inatuambia kitu tofauti kabisa, kwamba inawezekana watu wenye taaluma mbali mbali wakasaidiana. Najaribu kufikiria jambo hili kwenye maisha ya utumishi wa Mungu. Lakini bado naona kuna shida ya kile kinachoitwa “kusaidiana” leo ni vigumu mchungaji wa kanisa fulani kuondoka na kwenda kumsaidia mchungaji mwenzake wa kanisa jingine. Nikajaribu kutafuta kujua kwa nini kuna hali kama hiyo? Nikagundua “ubinafsi, na kujiona bora zaidi” ndio sababu kubwa inayosumbua. Lakini cha ajabu hata mtumishi wa Mungu wa kanisani hanashindwa kumsaidia mtumishi mwenzake wa kanisa moja, madhabahu moja,!!! 😭😭😭
Sielewi tatizo lipo wapi sasa, ikiwa mtumishi mwenzako wa kanisa moja na huwezi kumsaidia kiroho kwa kigezo atajua zaidi yako wewe!!! Hii ni mbaya sana. Sasa ikiwa mtumishi mwenzako mwenye kufanya huduma moja na wewe, huwezi kumsaidia, Vipi Je itakuwaje kwa mtu mwingine mwenye taaluma tofauti na wewe, utaweza kumsaidia? Maana jepesi ni lipi? Kumsaidia mwenye taaluma sawa na yako, au kumsaidia mwenye taaluma tofauti na yako? Bila shaka;rahisi kumsaidia yule mwenye taaluma sawa na yako. Lakini mbona hakuna masaidiano ya namna hiyo? Je huu ndio ukristo anaoutaka BWANA? Biblia imetueleza kwa makusudi uwezekano wa kusaidiana hali tukiwa tofauti kihuduma, kitaaluma, kiuwezo n. K
Ikiwa mtu mmoja ana karama ya unabii naye hana karama ya ualimu basi na aje kwa nabii, wasaidiane kila mmoja. Ikiwa mtu mmoja ana karama ya maongozi naye hana karama ya ualimu basi na aje kwa mwalimu wasaidiane kila mmoja. Lakini ikifika wakati wa kila mmoja kujiona yeye ni bora, au kukataa kumfuata yule mwenye nacho, basi hiyo sio tabia tunayofundishwa katika Neno la Mungu. Leo, kazi ya Mungu tumeifanya kuwa ngumu kwa kuwa tumekataa kusaidiana bali kila mmoja anajifanya anajua zaidi. Mimi huwa sielewi kabisa!!! Kwa nini ujifanye unajua hali ujui kitu? Kwa nini usikubali kusaidiwa? Ili na wewe ukawasaidie wengine.
Lakini tunaona jambo jingine lililopo kwa hao mafundi “Seremala akamtia moyo mfua dhahabu “. Unajua kazi ya Seremala ni tofauti na kazi ya kufua dhahabu, lakini hali kuna utofauti mkubwa bado Seremala akamtia moyo mfua dhahabu. Hii ina maana kwamba Seremala anaikubali kazi ya mfua dhahabu ndio maana alimtia moyo. Lakini hii ina maana pia kazi ya mfua dhahabu ilionekana na Seremala akaitambua.
Ni rahisi kabisa kwa Seremala kuikataa kazi ya mfua dhahabu kwa sababu Seremala anataaluma yake binafsi. Lakini Seremala huyu hakuona kitu kushikilia useremala wake hali akijua Kazi ni zaidi ya useremala. Hivi unanielewa lakini 😎?
fikiria jambo hili; wewe unafanya kazi gani? Kisha kazi uifanyayo unashirikiana na mtu mwingine kabisa mwenye kufanya kazi nyingine tofauti na yako. Je upo tayari kumtia moyo kwa maneno au matendo? Ukweli ni kwamba watu hatuishi hivyo!!! Lakini kama huwezi kumtia moyo mtu mwingine basi ujue kwanza “huoni kazi yake, ” pili “huikubali ” tatu “una kiburi cha kawaida kabisa”
Biblia inasema “ Seremala akiisifu kazi ya kuunga, akisema ni kazi njema” Oooh my God! Jesus help us. Imefika wakati Seremala akaisifu kazi ya fundi mwenzake tena mwenye taaluma tofauti na yake; tena akazidi na kusema “ni Kazi njema ” ni wangapi leo wapo tayari kuikubali kazi ya mtu mwingine,mbali na kanisa lake. Kisha akasema kwenye halaiki “kazi ya mchungaji mfulani ni kazi njema sana“. Au ni nani leo asimame na kuisifia kazi ya mtu mwingine? Ukweli ni kwamba wapo watu wa namna hiyo, lakini ni wachache sana tena ni wakutafuta kwa kweli. Lakini je ndivyo tunavyofundishwa? Lah hasha!!
Anza leo, kuikubali kazi ya mwenzako. Tena ifike wakati ambapo uisifu kazi aifanyayo hata kama ni kazi ndogo, lakini ukumbuke kwamba katika udogo huo huo kuna kitu kinafanyika. Ukiweza kuikubali kazi ya watu wengine, ujue na kazi yako itakubalika tena zaidi ya hapo kutakuwa na kibali zaidi. Wapo wachungaji ambao hakubali kabisa kazi za watu wengine.
Yaani ukifika na kujitambulisha
“ mimi nimeokoka nampenda Yesu” ujue watakuuliza “unaabudu kanisa gani” kwa kigezo cha kutaka kujua kanisa, ukiwaambia kanisa fulani ambalo wao kwanza hawalitaki, hapo tayari watakujaji, “mhhh huyu hajaokoka bhana kama anaabudu kule” Hali / tabia hii ni mbaya!!! Jifunze kwa mafundi hawa. Kwa maana kila mmoja alimkubali mwenzake na kukubali kushirikiana naye tena kila mmoja akamtia moyo mwenzake na kuisifu kazi ya mwenzake.
Kutia moyo kuna maana kubwa sana,kwa maana kutia moyo kunaonesha kukubali kile mwenzako anachofanya. Ni kweli kunawezekana kukawa na makosa fulani lakini nakwambia hakuna kwenye makosa mazuri yakakosekanika bhana!
Ikiwa kama umejifunza kitu hapa, nifahamishe.
Kwa huduma ya maombi pia piga kwa namba hizi ; +255 683 877 900
What’s app namba ni+255 746 446 446 .
Na Mch. G. Madumla
UBARIKIWE.
Comments