USISHINDWE NA UBAYA,BALI UUSHINDE UBAYA KWA WEMA.
- Mch. Gasper Madumla
- Oct 31, 2018
- 3 min read
Bwana Yesu asifiwe…
“Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema. ” Warumi 12:21
Watu wengi hufikiri kwamba ubaya unalipwa kwa ubaya wakidhani wako sahihi na kumbe ubaya haulipwi kwa ubaya bali ubaya unalipwa kwa wema. Ikiwa umeumizwa basi huna sababu yakuumiza pia,bali jitahidi kulipa jema,na wema wako utakuwa jibu sahihi kwa ubaya wao. Je unafikiri kitendo cha kulipiza ubaya kitakuweka leo kwenye sehemu gani?
Na hapa yupo mtu aitwae Yusufu mtoto wa Yakobo,aliyetendewa mambo ya hiyana / ubaya. Ndugu zake walimkusudia kumwua na kuziangamiza ndoto zake bali Mungu alimkusudia mema. Fikiria mtu kama Yusufu aliyetendewa hila na udanganyifu mkubwa lakini bado hakuwalipa ubaya kwa ubaya. Ni kweli ndugu zake walimwuuza,akawa mtumwa huko Misri,akafungwa.
Na hatimaye Bwana akampandisha kutoka gerezani hadi kwenye ngazi ya uwaziri mkuu wa Misri. Alikiwa kiongozi baada ya farao,ebu cheki kwenye ile miaka saba ya njaa iliyowalazimu ndugu zake kutoka Kanaani hadi Misri kutafuta chakula; Yusufu hali akiwatambua ndugu zake lakini tunaona akiwafanyia ukarimu kama sehemu ya kuwalipa mema kwa mabaya waliomfanyia.
Biblia inasema Yusufu aliwaandalia ndugu zake karamu naye akaketi pamoja nao ( Mwanzo 43:24 – 34) akala chakula pamoja nao.( Kumbuka ni watu hao hao waliotaka kumwua ). Haikuwa rahisi lakini Yusufu ameonesha mfano kwamba usilipe baya kwa sababu umetendewa baya,bali ulipe jema ili wengine wajifunze Mungu wako uliye naye.
Usichoke kutenda ukarimu kwa wabaya wako.
Unamwitaji Mungu akusaidie ili uweze kuishinda hasira na uchungu uliopo ndani yako kwa maana sasa unatakiwa usilipe baya hata moja. Bado nakutazamisha kwa Yusufu huyo huyo ambaye kabla ya kujifunua kwa ndugu zake,hakuwatendea mabaya kitu ambacho kilikuwa ndani ya uwezo wake. Yusufu angeliweza kuwaangamiza kaka zake wote kipindi kaka zake walipoingia Misri kununua chakula. Lakini Yusufu aliwatendea mema tu. Fikiria mazingira magumu kama hayo aliyopitia Yusufu, bila kurudisha ubaya kwa kaka zake. Vipi wewe,Je unaweza kustahimili ubaya wa ndugu zako bila kurudisha cheche za ubaya? Jihoji,!!! Wengi wameshindwa.
Leo,yafaa ujifunze kusamehe na kuachilia kisha uwatendee wale wabaya wako mema kama kwa Bwana. Ni vigumu kutenda jema ikiwa umetendewa ubaya lakini inawezekana bado kutorudisha chochote kibaya kwao. Siku zote ubaya haukosekani,kwa maana kama kuudhiwa utaudhiwa tu. Au kama kutendwa vibaya kutakuwepo tu. Lakini unafanya nini unapotendewa vibaya? Je unashindwa kujizuia kiasi kwamba ni lazima urudishe ubaya?
Ili kuonesha kuwa ni lazima utaudhiwa au kutendwa,ebu fikiria unapopanda daladala,utakuta mtu akikukanyaga wakati mwingine aliyekukanyaga huomba msamaha au wakati mwingine aliyekukanyaga hakuombi msamaha na utajua wewe mwenyewe. Tena mtu wa namna hii ukimwambia “unanikanyaga bhana” tegemea atakujibu “kama unataka usikanyagwe panda taxi,au nenda kapande UBA” Hii ni kuonesha kwamba hata kama wewe utakuwa mwema kiasi gani lakini kuudhiwa ni lazima ( 2 Timotheo 3:12).
Hivyo,suala sio kuudhiwa bali suala unachukua hatua gani / unalipa nini baada ya kuudhiwa? Kumbuka : ukitaka kuushinda ubaya wa aina yoyote,wewe tena mema tu. Na hapo utauzimisha ubaya wa kila aina.
Roho mtakatifu,awezaye kukupa kuushinda ubaya kwa wema.
Unatambua wewe mwenyewe huwezi kuushinda ubaya huo bila Roho mtakatifu? Ndio huwezi peke yako kwa sababu hata sasa umejitahidi kujizuia lakini bado upo kwenye uharibifu,hivyo ni vyema umwombe Baba akusaidie kwa Roho wake,uwe na nguvu ya kuushinda ubaya huo. Bila Roho wa Bwana, utachemka ndugu,unamwitaji sana akusaidie.
Mimi najua kuna haja kubwa kwako ya kusaidiwa hasa kiushauri na maombezi ili uweze kuyashinda hayo unayopitia sasa. Nami nipo nawe sasa,ukiamini kwamba Yesu yupo kukusaidia leo,ebu usisite mpendwa kunipigia simu sasa ili tuombe pia pamoja.
Ikiwa fundisho hili limekubariki na umejifunza kitu,basi nifahamishe kupitia namba zangu + 255 683 877 900
WhatsApp ni .+255 746 446 446
Mch. G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comments