top of page

USIMLAZIMISHE MUNGU AONE UTAKAVYO!

Shalom…

Kwa ufupi.

Leo imekuwa ni shida kubwa sana inayotusumbua kwa kumtaka Mungu aone vile tunavyotaka tena kwa kumlazimisha kweli kweli. Ukumbuke jambo moja kwamba,Mungu aonavyo ni tofauti sana na uonavyo! Ninajua unaweza ukawa na maswali sasa,kwamba;

“ kwa nini Mungu asione kama nitakavyo? Kwani mimi si mtoto wake lakini?…mimi naona ni sawa tu kumtaka Mungu aone nitakavyo kwa sababu nimepewa mamlaka ya kuomba..” maswali ya namna hii yanaweza kuwepo ndani yako hasa tunapojifunza somo hili. Nami sishangai ukiwa na maswali mengi kwa maana ninajua wewe u mwanadamu kwa sababu mwanadamu ana tabia ya kuuliza maswali,ndio maana kila mtu ameumbwa mfano wa alama ya kiulizo “ ? ” ( question mark)

Unakumbuka habari za Yakobo / Israeli kumbariki Efraimu badala ya Manase? Bila shaka umesahau,ni hivi; Mzee Yakobo alipofika Misri kwa mwanaye Yusufu ambaye alikuwa waziri mkuu wa nchi yote,aliletewa watoto wa Yusufu wawili Efraimu na Manase ili awaone. Na alipowaona wale watoto alipendezwa nao sana hata akawafanya kuwa wake ( maana alihamisha mbaraka na haki ya uzaliwa wa kwanza wa Reubeni mwanaye mkubwa na kuwapa watoto hawa wawili 1 Nyakati 5:1 ),na kuwabariki.

Alipoletewa wale watoto wawili akitangulizwa Manase mzaliwa wa kwanza na kuwekwa kwenye upande wa mkono wa kuume wa Yakobo babu yao,kisha mkono wake wa kushoto akawekwa Efraimu kama mtoto wa pili asiyestahili haki ya uzaliwa wa kwanza. Lakini mzee Yakobo akapindisha mikono yake kama kuweka alama ya x,yaani mkono wake wa kuume akauweka kwa Efraimu na mkono wake wa kushoto akauweka kwa Manase ( Mwanzo 48:8-16). Sasa angalia kile kilichotokea hapo;

“Yusufu alipoona kwamba babaye anaweka mkono wake wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, ikawa vibaya machoni pake. Akauinua mkono wa babaye auondoe katika kichwa cha Efraimu, ili auweke juu ya kichwa cha Manase.“ Mwanzo 48:17

Maandiko yanasema Yusufu alipoona babaye anaweka mkono wake kwa Efraimu, ikawa ni vibaya kwake. Jambo hili lilimsumbua Yusufu, bila shaka alijiuliza ndani yake “… kwa nini baba / mtumishi aa Mungu anamwekea mkono huyu ambaye ni mdogo asiyestahili baraka hizi? Hivi kwa nini jamani? Ina maana mtumishi babangu hujui kuwa huyu hastahili,au uoni ninavyoona?… ” na baada ya hapo,Yusufu akanyanyua mkono wa mtumishi wa Mungu babaye na auondoe kichwani katika kichwa cha Efraimu. Ni kana kwamba anataka Yakobo babaye anayesimama kama mtumishi wa Mungu aone vile atakavyo yeye!!!

Biblia inatuambia mzee Yakobo / Israeli inagawa alikuwa haoni kwa maana alikuwa mzee,macho yake yakapoteza nguvu ya kuona; lakini alikuwa akijua atiavyo mikono yake ( Mwanzo 48:14). Kama alikuwa akijua atiavyo mikono yake,basi ni dhahiri alikuwa kiona rohoni yote yanayoendelea na alimwona Efraimu kisha akamwona Manase kiunagaubaga,hata hivyo Yusufu alikuwa hayajui yote haya.

Yusufu alikuwa akimlazimisha babaye mwenye kuona kiroho,kwamba aone kama yeye asiyeona rohoni kwa kipindi kile cha mbaraka. Yusufu anatupa picha safi kabisa kwa kile unachokifanya leo kwa kutaka kuondoa mkono wa Mungu kwenye kile ambacho afanyacho na kutuka afanye katika yale tu unayoyaona wewe sasa.

Kama vile Yakobo anavyosimama na kubariki,ndivyo asimamavyo leo mchungaji au mtu yoyote mpakwa mafuta wa Mungu kubariki au kuweka sawa jambo fulani katika hali ya kiroho. Lakini hapo ndipo penye shida,kwa maana wengi husimama na kujaribu kushika mikono yao,kuiondoa mahali ambapo wamepewa maelekezo ya kiungu;

tena kama vile Yusufu kuona jambo hili si sawa kwamba baba ambariki huyu mbaye hakustahili,ndivyo na leo unavyoweza kuona kwamba kwa nini mchungaji amwinue huyu mtu asiyefaa kabisa!!! “ Yaani mchungaji angemjua huyu vizuri,asinge mwinua,huyu ni mtu mbaya sana nakwambia…” Hayo ndio maneno ya watu wasemayo pale wanayemtegemea kuinuliwa asiinuliwe,na yule wasiomdhania kuinuliwa.

Kumbuka jambo hili; “Mungu huviinua vinyonge na kuviaibisha vyenye nguvu” Lakini katika yote,usitake kumlazimisha Mungu aone vile utakavyo wewe,kwa maana wakati mwingine wewe huona vibaya. Lakini kwa sababu hujui mapenzi ya Mungu basi unajikuta ukilazimisha mambo fulani,leo hii,jifunze kwa mfano wa Yusufu.

Ikiwa kama umejifunza kitu hapa,nifahamishe. Pia kwa huduma ya maombezi nipigie sasa kwa +255 683 877 900

Whatsapp namba ni +255 746 446 446

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page