top of page

USIDHARAU MAONYO

Updated: Aug 30, 2022



Maonyo”ni maelekezo binafsi apewayo mtu akitaadharishwa juu ya jambo/kitu kibaya kinachotazamiwa kutokea. Wakati mwingine maonyo ni “makemeo” hata hivyo maonyo ni maneno yenye kutoa hali ya tahadhali. Mungu ambaye ni Baba yetu,hutuonya kila siku kupitia njia mbali mbali kwa lengo la kutufanya tuwe pamoja na Yeye,ingawa mara nyingi tunayakataa maonyo yake.


Tunaweza kuyaona maonyo ya Mungu kwa mara ya kwanza pale alipomwonya Adam juu ya kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya (Mwanzo 2:17). Mpaka Bwana Mungu anamwonya mwanadamu,kwamba asije akala matunda ya mti huo,maana akila atakufa hakika,alikuwa anajua moyo wa manadamu una shida ikiwa kama mwanadamu atakuwa mbali naye,na ndio maana akamtahadharisha mapema na kumwambia adhabu ya tendo hilo kama litafanyika. Mauti aliyoipta Adamu ilikuja kwa sababu Adamu aliyaacha maonyo ya Bwana,kwa maana alikwishaambiwa maelekezo yote. Hata sasa,majanga mengi hutukuta kwa sababu tu tumeyasukumia mbali maonyo ya Bwana.

  • Mungu ni Mungu wa maonyo.


Kwa sababu ya “pendo” la ajabu alilonalo Bwana Mungu,Yeye hujidhihilisha katika sura ya maonyo kwa watu wake kila siku. Kumbuka;yeyote anayekuonya vyema,huyo anakutakia mema!Mbali na Mungu kushughulika sana na Adamu pia aliendelea kuhakikisha anashughulika na uzao wake ili urejee kwake kwa kuwapa njia sahihi katika maonyo mbali mbali. Biblia inarekodi kisa cha kwanza cha ibada ya matoleo walioifanya akina Kaini na Habili mbele za Bwana.


Katika ibada hii,Bwana anamwonya Kaini kwa upendo kabisa,pale ambapo sadaka yake ilipokataliwa pamoja naye,Bwana akamwambia  “Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.” Mwanzo 4:7 Maneno haya yalikuwa ni maonyo kamili kwa Kaini kwa maana yanaonesha na matokeo ikiwa kama Kaini hatafanya aliyoambiwa.

Ingawa Bwana alimwonya Kaini lakini,kwa makusudi Kaidi hakutaka kutii, na hatimaye Kaini akaangukia dhambini. Kaini hakupata dawa ya kurejea maana aliamua kutokubadilika kama wengine wafanyavyo,biblia imeweka wazi kwamba “ onywaye mara nyingi akishupaza shingo, Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.” Mithali 29:1.


Kaini aliamua kukataa na kwenda kwenye njia zake binafsi,hali akijua njia gani anapaswa kwenda. Alipokea maonyo mengi,lakini hakutaka kutubu. Je leo,ikiwa umeonywa mara nyingi na huna mpango wa kutubu,hufanani na Kaini? Je maanguko yako hayatakuwa makubwa?

  • Kwa nini watu hudharau maonyo?


Ukweli ni kwamba watu hawapendi kuonywa,wala kusemwa. Na ndio maana ukitaka ugombane na watu hata wapendwa, basi wewe simama katika eneo la kuonya/kukalipia tena katika haki tu. Nataka nikwambie;Hapo watakuchukia kwa sababu ya kweli uisemayo na kwa sababu ya maonyo yako. Lakini hata hivyo,watu hudharau na kukataa maonyo kwa sababu “wamefungwa na ibilisi”. Moja ya furaha ya adui/ibilisi ni kuona kwamba unatembea kinyume na maonyo,ili baadae uanguke kama alivyoanguka Kaini.


Kumbuka;kiburi ni tabia ya shetani,hivyo wale wanaokataa maonyo ni wale wanaoona kwamba wanajua sana,na ndani yao ibilisi amechukua nafasi ya kupanda kiburi,na kwa kiburi hicho kamwe hawawezi kukubali kuonywa au kuongozwa,na matokeo yake ni maanguko tu! Ebu cheki mtu yeyote mwenye kiburi kama anakubali kuonywa/kurekebishwa,kisha utagundua!


  • Asiyedharau maonyo,huvuka zaidi.


Tazama lile tukio la kuangamizwa kwa miji ya Sodoma na Gomora. Biblia inatupa maelezo mazuri kwamba Bwana alimshukia Ibrahimu kabla ya kwenda kuipiga miji hiyo. Wakiwa njiani pamoja na Ibrahimu,biblia inasema Bwana amfunulia Ibrahimu juu ya maangamizi hayo. Maelezo ya kuangamizwa kwa Sodoma na Gomora ni maonyo makali,lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana akiomba,kunusuru wale wenye haki wasije wakafa na waovu. Kuomba kwake kulisikiwa hatimaye mwenye haki akaachwa na mwovu akaangamizwa ( Mwanzo 18:16-33).


Laiti Ibrahimu angelidharau maonyo hayo,basi labda mwenye haki angelikufa na mwovu,lakini hata hivyo haukuwa utaratibu wa Bwana kumwua mwenye haki na mwovu. Lakini kuomba kwake Ibrahimu kulisaidia. Hata leo,pale penye maonyo ya namna yoyote ile,hapo hapo ukisimama na kufanyia kazi maonyo hayo,uwe na uhakika utavuka tu katika eneo hilo.


Ikiwa umebarikiwa na ujumbe huu,nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja.


Na kwa huduma ya MAOMBI ushauri na msaada zaidi,piga sasa +255 683 877 900


What’s app namba +255 746 446 446.


Na Mch.G.Madumla.


UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page