USHAURI WA MEMUKANI – 02. (Tamati)
- Mch. Gasper Madumla
- Nov 25, 2019
- 3 min read
Bwana Yesu asifiwe….
Kwa ufupi,
…Neno la Memukani lilikuwa na nguvu na kibali kwa mfalme Ahasuero,kwa hiyo hii inaonesha kuwa kile alichokisema Memukani kinasikilizwa mno. Biblia inatupa simulizi nzuri juu ya Vashti Malkia kukataa mwaliko wa mfalme Ahasuero katika moja ya sherehe kubwa ya kifalme. Kwa maana mfalme alipofulahiwa moyo wake kwa divai (Esta 1:10),ndipo alipotuma watu wakamwite Vashti malkia kwa kusudi moja tu,kwamba huyo Vashti malkia aje na ajipitishe mbele ya wageni waliokuwa wamelewa. Hii ilikuwa ni moja ya dhihaka kwa mwanamke Vashti malkia kwa maana watu waliokuwa wakimsubiri walikuwa “tungi”/wamekunywa divai,bila shaka wamelewa “tila lila”.Katika mazingira kama hayo,ndipo mfalme anatuma watu wamlete malikia apite mbele ya walevi,(Na si kupita hivi hivi tu,bila shaka mfalme alimtaka malkia na ajifunue kidogo ili watu wauone uzuri wake,sasa huu ni udhalilishaji wa mwanamke).
Lakini hata hivyo,Vashti alikataa ujinga huo,na hapo ndipo mzee Memukani akapata nafasi sasa ya kumshauri mfalme. Umeona hapo! Kumbe akina Memukani wapo wakisubiri mahali ukosee kidogo tu wapate nafasi ya kuleta uharibifu! Lakini ukichunguza kwa umakini,utaona kwamba Memukani alikuwa mmoja wa kisababishi cha kumwondoa Vashti kwenye umalkia wake katika yale yote aliyoyasema. Huyu Memukani ameandikwa kueleze vile ambavyo watu wa namna kama hiyo leo ambao ndio kisababisho kikubwa cha kukufanya utolewe kwenye maeneo yako ya kazi.
Ukisoma kile alichosema Memukani kwa mfalme, utaona kilikuwa hakimlengi Vashti malkia peke yake bali kiliwalenga wanawake wote maana alisema “ Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja. Hata na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliokwisha kuzisikia habari za tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maakida wote wa mfalme. Hivyo kutatokea dharau nyingi na ghadhabu tele.” Esta 1:17-18
Ni kweli kabisa,labda wanawake wangesikia habari hiyo labda wangewadharau wanaume wao. lakini si vyema kuwajumlisha wanawake wote,hata hivyo bado busura za kawaida zilihitajika katika ushauri wake,labda moja ya busara ni kwamba,wangelimuoji malkia kwa nini amekataa kuja? Ni kweli mfalme ni mfalme na ana mamlaka yote,lakini bado Memukani alikuwa na nafasi ya kumshauri vyema mfalme. Lakini aliona dawa ya Vashti ni kufukuzwa kwenye umalkia! Ukiendelea kufuatilizia kisa hiki utagundua maneno ya Memukani yalipandisha juu hasira ya mfalme kiasi kwamba alimwondosha mara moja malkia. Biblia inasema “hasira ya mfalme Ahasuero ilipotulia,alimkumbuka Vashti na vile alivyotenda,…” Esta 2:1. Kumbe,ushauri mbaya huchochea ghadhabu (Mithali 15:1)
Akina Memukani hata leo wapo,wapo tu kwa ajili ya kuleta uharibifu kwa ushauri wao usiofaa. Memukani wa leo anaweza akawa ni boss wako wa kati mtu ambaye ana nafasi ya juu ya kukaa na uongozi wa kazini,mtu anayesikilizwa asemacho kisha bosi mkuu au uongozi ukafanyia kazi mara moja. Sasa akishauri mabaya ujue yataleta madhara makubwa ambayo yatamfanya boss mkuu kujutia maamuzi hayo baada ya kupitishwa! Memukani anaweza akawa ni mtumishi mwenzako kanisani ambaye amepata kibali kikubwa kwa mchungaji wako,mtu ambaye anasikilizwa mno,nao watu wa namna hii mara nyingi wanakuwa ni “mwimba”,yaani ushauri wao unaumiza watu wengine.Au Memukani anaweza akawa ni mmoja wa familia yako ambaye ana kibali katika maamuzi ya juu. Hata nafasi yake ya ushauri ikaleta uharibifu badala ya kujenga!
Ni namna gani unaweza ukamshughulikia Memukani?
Kwa kuwa Memukani ana kibali kikubwa kwa boss/kiongozi,basi huwezi kushindana naye kwa jinsi ya mwili. Kwa maana ukijaribu kuwa kinyume naye,ujue wewe ndio utakayetoka hapo wala si yeye.Na unaweza ukatolewa kwenye nafasi kwa aibu kubwa ukiwa umechafuliwa wadhifa wako. Isipokuwa Memukani anapingwa kiroho tu. Kwa njia ya maombi waweza kuzipinga hila,shauri zake. Lakini pia, moja ya njia kubwa ya kumshinda Memukani ni wewe kuwa mwenye haki,ili Mungu akupiganie. Kuwa mwenye haki,ni kuokoka,na kutembea na Mungu kikamilifu,kisha hapo Memukani hatakuwa adui wako,bali atakuwa ni adui wa Mungu,na hapo hakika utamwona Mungu akikushangaza kwa kukupigania.
Ikiwa umebarikiwa nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja. Kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI piga kwa +255 683 877 900.
Na.Mch. G.Madumla
Whatsapp namba +255 746 446 446.
UBARIKIWE.
Comments