top of page

BARAKA ZA WAZAZI.

“….Mwaka fulani nilikuwa nikipiga stori na marafiki zangu tukiwa katika dala dala moja hivi,tunaelekea Kimara. Mmoja wao alikuwa ni binti naye akawa akisema yeye kamwe hawezi kufuata ushauri wowote wa baba wala mama yake mzazi kwa sababu hawajaokoka na yeye ndie ameokoka katika familia yao.

Mimi sikumshangaa sana,kwa kuwa nilijua kwamba kuna eneo fulani la kimtazamo halijakaa vizuri kwake. Na inawezekana labda hajafahamu kile wazazi wake walichobeba katika maisha yake hata kama hawajaokoka….”

Kwa ufupi,

Labda inawezekana mtazamo huo na wewe ukawanao. Au labda umewahi kusikia hivyo, kwamba wazazi si kitu sana ikiwa wewe umeokoka nao bado hawajapata neema kama yako. Lakini kuna kitu cha kujifunza kupitia wazazi

Ukweli ni kwamba, wazazi ni watu wa muhimu sana kwako bila kujali hali zao za kiroho. Wana upekee fulani katika maisha yako. Kwa maana kupitia wao,wewe ulizaliwa. Upekee huu ni kuhusu “baraka” ambazo Mungu ameruhusu kuziweka kwa wazazi wako. 

Neno hili “Baraka ” linaweza kutafsiriwa kama  nguvu iliyo hai ya Kiungu iletayo mafanikio. Wazazi wa pande mbili ( wazazi wa kiroho na wa kimwili) wamepewa nguvu na Mungu ya baraka kwa mtoto. Lakini ebu tuone “ ni baraka za namna gani “ walizobeba wazazi wa kimwili wale waliokuzaa wewe,hata kama kwa sasa hawapo hai lakini kuna kitu walikibeba kwa ajili yako. 

Angalia mfano wa kuku anayetaka kutaga jinsi anavyoangaika kutafuta mazingira rafiki ya kutaga,na akiisha kuyapata anahakikisha atataga mayai yake yote mahali pamoja kwa maana mahali hapo anapaamini. Lakini ili aweze kutoa vifaranga vyake/ watoto itamgharimu kuyalalia mayai yake kwa muda usiopungua kama siku 21.

Sasa,vitoto vya kuku hutegemea sana nguvu ya mama yao ya kuwatoa katika mayai,pia nguvu ya kuwalinda dhidi ya mwewe / kunguru na wanyama wengine hatari. Hii yote ni kuonesha kwamba kuku kama atakuwa salama basi usalama wake umechangiwa na nguvu ya mzazi /mama yake.

Utaratibu huu ni mfano tu,unaoonesha mchango mkubwa sana wa wazazi hata hapo ulipofikia. Unajua hata kama mzazi alikuzaa na baadae alikukataa kabisa, lakini bado ana mchango mkubwa katika maisha yako,kwa maana kupitia huyo wewe ulizaliwa. Suala la kukataliwa ni matokeo tu ya mzazi binafsi lakini kusudi la Mungu wewe uzaliwe na mzazi huyo,hivyo hutakiwi kumzalau mzazi wako kwa sababu yoyote!!

  1. Tengeneza na wazazi wako,uchote baraka.

Ikiwa una neema ya kuwa na wazazi mpaka sasa, mshukuru Mungu sana bila kuangalia hali zao za maisha,au hali zao za kiroho / hali za kiimani. Kwa maana kuna watu ambao hawana neema hiyo ya kuwa na wazazi hai mpaka leo, tena wengine hata hawajafanikiwa kuwaona wazazi wao.

Jitahidi sana utengeneze nao/ upatane nao vyema kabla wao hawajafa kwa maana ikiwa wapo hai au ikiwa yupo hai,jiulize kwa nini yupo hai mpaka sasa? Mbona hakufa kama wengine? Ameshikilia kitu gani kwa ajili yako?

Hivyo jitahidi ujiungamanishe nao kwa kuwapelekea zawadi mara kwa mara zitakazo chochea wao kukutamkia mibaraka ( Kwa maana moyo wa mzazi ukifunguka juu yako,hiyo tu ni dawa tosha ya kile unachokitafuta siku zote. ). Hata Isaka “alipokula kwanza chakula kitamu” cha mwanaye Yakobo,alimtakia mibaraka ya kutosha.

Nawe pia tafuta njia ya kuchota baraka kwa wazazi wako kabla hawajafa. Mfano,walishe vizuri,wavalishe nguo nzuri n.k Nao watafungua moyo zaidi kwako na mibaraka itakuwa sehemu Yako.

  1. Usitishwe na imani ya mzazi.

Inawezekana mzazi wako ni mshirikina,au ni mganga wa tunguli. Au labda ni mtu asiyekuwa na dini, kwamba ana Jina la kikristo lakini hata mlango wa kanisa haujui!!! Hayo yote hesabu ni matokeo tu,na yasikunyime baraka zako. Kwa maana ukiweza kuchukuliana na mzazi wa namna hiyo,basi uwe na uhakika mtaishi vizuri naye atakubariki.

Angalia mfano kwa Yakobo na baba mkwe wake mzee Labani. Biblia inasema Yakobo alikuwa mcha Mungu lakini baba mkwe wake alikuwa mwabudu sanamu,kama mshirikina tu wa kawaida. Kwa hiyo Yakobo na Labani ni watu wawili tofauti kiimani hata kimtazamo. Lakini Yakobo alijua kula naye Labani vizuri hata akafanikiwa kuchota baraka zake pamoja na kwamba walitofautiana.

Labani akaondoka asubuhi na mapema, akawabusu wanawe na binti zake, akawabariki; kisha Labani akaenda zake, akarudi kwao.” Mwanzo 31:55

Sasa,vipi jambo hili lingelikuwa kwako, yaani wewe ni mtu mwenye hofu na Mungu/mpendwa lakini baba mkwe wako ni mganga wa tunguli, halafu huyo mzee anajisogeza kwa mwanae uliyeoa /aliyekuwa. Hivi itakuaje hapo? Si utamkemea mwenzako kwamba ajitenge na baba yake?!! 

  1. Ni nani anayeweza kumbariki mwingine?

“  Wala haikanushiki kabisa kwamba mdogo hubarikiwa na mkubwa.” Waebrania 7:7.

Huo ndio utaratibu wa kiungu. Wewe kama mtoto unastahili ubarikiwe na mzazi wako. Hata kama mzazi bado yupo gizani,wewe ambaye ni mtoto wapaswa kutumia hekima umwelekeze mkubwa/ mzazi wako akuachilie kwa mibaraka kwa maana wewe umelifahamu hili.

  1. Kama wazazi walishakufa,utapataje baraka zao?

Kuna namna ambayo Mungu anapitisha baraka zako za wazazi kwa walezi au hata wazazi wako wa kiroho ikiwa kama wazazi wako wa kimwili walishakufa miaka mingi. Kupitia walezi wako wenye kusimam katika nafasi za wazazi,hao wamebeba baraka zile zile. Au kupitia baba au mama wa kiroho, hapo kwa mikono yao Mungu  huachilia baraka zako za wazazi. Hivyo kwa namna yoyote ile baraka za wazazi wako zipo tu. ( Ukijiungamanisha nao hao,utazipata baraka zote.)

Kumbuka;

Waheshimu baba na mama yako upate baraka ( Waefeso 6:2-3). Kuna mambo mengine unayopitia ni kwa sababu mioyo ya wazazi wako ( wa kiroho au wa kimwili) imefunga! Ujue kufanikiwa kwako kutakuwa ni kugumu sana. Maana kuna watu ambao waliondoka nyumbani kwa wazazi au walezi wao kwa mafarakano kisha hawajarudi mpaka wazazi wamekufa,au hawajarudi mpaka leo.

Ujue ni wewe ndio unajiwekea ugumu wa utafutaji wako. Ni vyema leo uchukue hatua ya kuwarejea wazazi au walezi wako, kisha utengeneze nao na hapo utaona baraka.

Kwa msaada zaidi,usisite kunipigia kwa simu hizi ; +255 683 877 900

What’s app number ni +255 746 446 446

Mch.Gasper Madumla.

UBARIKIWE.

Commentaires


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page