top of page

UPONYAJI WA MOYO ULIOJERUHIWA ~ 01

Updated: Aug 30, 2022


Kwa takwimu ya haraka haraka inaonesha kwamba watu wengi wamejeruhiwa mioyoni mwao. Kwa maana kuna kundi kubwa la watu katika ndoa siku za leo,wamejeruhiwa. Wengine wamejeruhiwa vibaya na wazazi wao,wengine wamejeruhiwa vibaya na mabosi wao,wengine na wachumba zao,wengine ni ndugu tu wamewajeruhi,na mbaya zaidi hata wachungaji wamejeruhi sana mioyo ya watu,… Vipi ndani ya kanisa la leo,limepona? Lah! Hata kidogo halijapona kwa maana ndani ya kanisa watu wamejeruhiwa mioyo sana,yaani hiyo ni ndani ya kanisa tu.


Unaweza ukaona ni kiasi gani hali ilivyo hivi sasa,kwa maana ikiwa ndani ya kanisa mchungaji kajeruhiwa moyo,mshirika naye analia kwa majeraha ya moyo,mzee wa kanisa kwa upande wake kilio hakiishi,moyo wake umejeruhiwa! Mwanakwaya/mwana praise naye analia kwa majeraha,sasa hata mwamini wa kawaida naye hatulii kwa mateso makali ya moyo wake,kwa maana amejeruhiwa!!! Sasa,fikiria ibada inaendaje hapo? Je ni kweli kuna ibada katika roho na kweli?.


Ukitaka kuona kwamba hakuna ibada au ipo,tazama kuomba kwao!Kwa maana mtu aliyejeruhiwa moyo wake hata kuomba kwake kunabadilika,kwa sababu ya maumivu! Hawezi kuomba katika roho na kweli! Sasa hali hii inatisha sana,na haivumiliki hata kidogo!

Wengi wetu hatujui nini cha kufanya kwa kweli! Kwa hiyo tunabakia kulia tu! Mimi nimetafakari kwa kina katika vilio tunavyolia na nikagundua “kulia sio dawa!” kwa maana ukilia weeh na ukimaliza,unagundua tatizo bado lipo pale pale.


Tatizo haliwezi kuondolewa na kilio chako,kuna kitu unatakiwa kufanya baada kulia kwako. Wapo baadhi yetu wachache ambao wamegundua siri ya uponyaji wa moyo uliojeruhiwa,na baadhi yetu hatujui tunafanyeje kutoka huko!!!


“Moyo uliojeruhiwa ni moyo uliobeba uchungu mwingi na huzuni pamoja na maumivu yasikoma “-( Warumi 9:1-2). Biblia inasema ni kwa namna gani Paulo alivyojeruhiwa moyo kwa sababu ya makosa na dhambi za watu wa taifa lake yaani Wayahudi,watu walioisukumia mbali injili,waliomkataa Yesu na kuigeukia dunia kwa kufuata sheria zisizoweza kuwaokoa. Kitendo hicho pekee kiliweza kuumiza moyo wa Paulo.


Ikiwa mtu kama Paulo,mtu aliyepakwa mafuta na Roho mtakatifu,

mtume,yeye aliyetokewa na Yesu Kristo mwenyewe,mtu huyo ameumizwa moyo,basi kumbe hata watumishi wa Mungu wanaweza kuumizwa mioyo yao. Biblia inajaribu kwanza kutueleza kwamba suala la kujeruhiwa moyo linaweza kuwapata pia wachungaji,walimu,mitume na watumishi wote! Hakuna aliyepona!!!


Kwa sababu ya pendo la Kristo alilonalo Paulo juu watu wa taifa lake, akajikuta akiumizwa moyo wake kwa makali sana. Hii inatufundisha kwamba,“ ukiwa umekamatwa na pendo la Kristo, moyo wako unaweza ukajeruhiwa kwa sababu ya dhambi za mtu/watu wengine wasiokuwa na haja ya kutibu” watu hao pasipo kukukosea wewe kwa neno au jambo lolote,lakini unajikuta ukiumia moyo sana,kwa sababu tu ya yale maovu wanayoendelea kufanya pasipo kutaka kugeuka.


Hujawahi kujeruhiwa moyo wako kiasi cha kupata maumivu makali hata kulia sana juu ya mtu ambaye afanyaye uovu,nawe umejaribu mara nyingi ageuke lakini majaribio yako yote ni kama “unampigia mbuzi gitaa” ?


Bila shaka umewahi. Fikiria mtu kama mume/mke ambaye tabia zake ni mbaya sana,nawe unajitahidi kumrejeza,lakini hakuelewi kabisa! Hapo ndipo unapojeruhiwa moyo wako!

Biblia imeweka wazi juu ya majeraha ambayo tunakumbana nayo. Majeraha ya aina mbili yanatajwa kwenye biblia;


  1. Majeraha ya mwili – Luka 10:30-31 ( majeraha ya kupigwa huitwa ni majeraha ya mwili)

  2. Majeraha ya moyo – Zab.147:3 ( Jeraha zinazozungumzwa hapo,ni jeraha za moyo)


Hatua ya kwanza ya “majeraha ya moyo” haitokani na sababu za nje ( kwamba uumizwe na mtu au watu) bali majeraha ya moyo katika hatua ya kwanza yanatoka na mtu mwenyewe ndani ya nafsi yake. Ni muhimu kuelewa vizuri! Moyo unapoanza kuugua tu,huo ndio mwanzo wa utungu na majeraha ndani yako.


Neno linasema“ Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua.Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.” Mithali 13:12


Hiyo ndio kawaida ya moyo kuugua kwa maumivu katika kile ulichokitarajia,halafu kikachelewa kuja. Nenda kamwangalie mtu aliyekuwa akitarajia kupata mtoto mara baada ya ndoa! Kadri ya muda unavyozidi kusogea bila tarajio lake,moyo wake ndivyo unavyougua. Na ikiendelea hali hiyo,utamwona akilia sana,kwa uchungu na kwa maumivu na hata kudhani Mungu amemwacha,lakini ukweli ni kwamba kinachomjeruhi ni tarajio lake yeye mwenyewe!


Hajasemwa wala kupigwa,lakini moyo wake umebeba maumivu makali kiasi cha kutama kufa! Majeraha ya namna hii yametoka ndani ya nafsi. Fikiria ni uchungu wa kiasi gani aliokuwa nao mwanamke Hana mke wa Penina,pale alipokuwa ametarajia kupata mtoto na mtoto kachelewa kuja,biblia inasema;“Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi?” 1 Samweli 1:8.


Kilio kilikuwa hakiondoki kwa Hana,ujue huyu hajapigwa wala kusemwa bali anacholia ni tarajio lililochelewa!!! Sasa unaelewa mtu mzima anapolia,kumbe mtu mzima anapolia ujue yamemfika makubwa ndani ya moyo,na hajui nini afanye?!


Sio rahisi kujiliza !!! Elkana anaamua kumjibu mkewe kwa hekima kubwa,lakini hekima yake hamyamazishi Hana kulia. Jiulize wewe mwenyewe,ni mara ngapi moyo wako unaugua kwa sababu tu,ya kile ulichokitarajia kuja kimechelewa?


Wapo wachumba ambao wanalia mioyoni mwao kwa maana matarajio yao hayakwenda walivyotaka wao….


ITAENDELEA.. (mwendelezo wake,tafadhali nitafute kwa mawasiliano ya hapa chini.)


Ikiwa umebarikiwa,nifahamishe.


Na kwa msaada zaidi pamoja na MAOMBI,piga sasa kwa namba hizi + 255 683 877 900

Whatsapp namba +255 746 446 446


Mch.G.Madumla.


UBARIKIWE.


Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page