top of page

UPAKO WA KUTAMBUA FURSA

Updated: Aug 30, 2022



  • Kila mtu wa Mungu amezungukwa na fursa mbali mbali lakini wazionazo na “kutambua” ni wachache mno. Wengi huzipita,au wakiona hawana “nguvu” ya kutambua.Kumbe suala sio uwepo wa fursa Bali suala ni “kuona na kutambua” kisha kuchukua hatua.


Kumbe suala la “kuona” ni kitu kingine na “kutambua” ni kitu kingine kabisa. Kwa maana waweza kuona fursa fulani na usitambue kuwa ni fursa kwako! Unahitaji upako wa kuona na “kutambua ” ,upako huo ni nguvu ya kiroho ya kuona wakati wengine hawaoni.

Unajua fursa ni kama vile dhahabu iliyojificha chini sana wengine wasemapo “mahali hapa hakuna dhahabu” lakini Wewe ukipacheki hivi,unaona kuna dhahabu. Ebu jifunze katika – Mathayo 13:44


Unajua huyu jamaa aliona kitu ambacho wengine hawakuona,na alipoona hakufanya mchezo!!! Kawaida kabisa suala la kutafuta fursa mbali mbali kila mmoja anatafuta lakini kuna watu wana upako wa kuona kwa haraka na kutambua/kuona thamani yake.

Ikiwa mtu wa kawaida kawaida ni ngumu kuona fursa na kutambua lakini ukipata upako wa kuona,nataka nikwambie wewe ndio utakuwa ukiwaelekeza watu fursa mbali mbali. Kuna wakati adui anafunga ufahamu,ili kusudi usione na kutambua thamani ya fursa ulizonazo karibu


ebu angalia mfano wa mababu zetu walikuwa wakichezea dhahabu wao waliona ni kama nawe fulani hivi, lakini walipokuja wazungu wakapigwa na butwaa!

Wakaomba wapewe hayo nawe Kisha wao wakawapa mitumba,vitu,na meza (wakabadilishana) . Mababu zetu wakawa wanawacheka wazungu na kuwaona hawana akili,yaani mawe tu kubadilishana na nguo!!


Kumbe wao ndio hawana akili,wamepigwa pabaya! Kwa sababu waliona kama mawe, lakini hawakutambua thamani ya mawe hayo. ( Haina maana kwamba wazungu walikuwa na upako,lah! Walituzidi ujanja tu)

Wale wote waliotambua fursa hawakubaki kama walivyokuwa!

Biblia ina mifano mingi ya watu ambao walipotambua fursa walibadilika. Lakini Kwa ufupi tu,angalia mifano hii


  1. Mjane – aliyekuja kuwa mfanyaniashara wa mafuta ( 2 Wafalme 4:1-7)

  2. Mjakazi wa ndani, Hajiri – aliyeona fursa ya kisima cha maji,akamwokoa mwanaye na mauti (Mwanzo 21:14-19


Katika hao wawili,tunaona hali zao za maisha kwamba hazikuwa ni hali nzuri. Walikuwa ni watu wenye maisha ya chini sana. Kuonesha kwamba Mungu huwainua watu waliokataliwa. Tujifunze kwa mmoja wao kati ya hao wawili, tujifunze kwa Hajiri  mwanamke wa Kimisri aitwae Hajiri,


Hajiri alikuwa ni mdada wa ndani katika nyumba ya boss wake Sara ambaye mumewe alikuwa ni Ibrahimu baba wa Imani. Biblia inatuambia Hajiri alifukuzwa na boss wake pamoja na mwanaye Ishimaeli ( mtoto wa Ibrahimu Kwa Hajiri).

Maskini Hajiri na mwanaye hawajui wanaelekea wapi,wakafika mpaka jangwani na yale maji ya kijana Ishimaeli yakaishi,kwa hiyo Hajiri akalia maana aliona mauti ya mwanaye inakuja. Mawazo na mtazamo wake aliona ndio mwisho wa maisha ya mtoto wake.


Ni sawa kabisa na mtu mmoja wa zama hizi,anayelia na kuona maisha yake yamefika mwisho kwa sababu ya “njaa au hali mbaya ya uchumi” na ndivyo alivyokuwa akilia Hajiri. Lakini kumbe alipokuwa Hajiri akilia kulikuwa na “kisima cha maji” halafu Mungu akamfumbua macho,naye akaona kisima hicho,halafu akafanya haraka akakijaza kiriba maji akamnywesha kijana. – Mwanzo 21:19


“kisima cha maji” kilikuwa ni fursa muhimu sana kwa Hajiri lakini kwa bahati mbaya macho yake yalifumbwa hakukiona. Halafu fikiria kwamba fursa hiyo ilikuwa karibu sana naye. Kumbe unaweza ukawa karibu sana na fursa na usione,but ukiona hiyo fursa na kutambua umuhimu wake,hakika maisha yako hayawezi kubaki hivyo hivyo,lazima kuwepo na badiliko!!! 


Kama ni hivyo,basi kitu cha kwanza unachohitaji ni “nguvu ya kutambua fursa “ ninaamini kama Hajiri angelikuwa ametambua uwepo wa kisima hicho,asingelia na kukata tamaa ya maisha ya kijana wake.  Lakini Hajiri alipopaza sauti ya kilio, Mungu alimsikia na kumjibu. Na aliposikia alishuka kwa kazi ya moja tu,nayo ni kuhakikisha macho yake Hajiri yanafumbuliwa.


Hii ina maana nguvu ya kuona fursa ni nguvu ya Mungu kwa maana bila hiyo Hajiri kamwe asingeona kisima hicho. Kumbe hata wewe,unahitaji sana nguvu ya Mungu ikufungue “macho yako “ Ili uone na kutambua fursa zako zilizokaribu sana na wewe.

Kama Mungu alimfumbua macho Hajiri ili alone kisima cha maji,basi ni dhahiri kabisa macho yake yalifumbwa kwa kusudi asione. Biblia haituambii kwamba ni nani aliyemfumba macho. Yawezekana ni Mungu mwenyewe au shetani. Lakini kitu muhimu hapo ni kwamba alifumbwa macho.


Leo kuna wangapi wamefumbwa macho,hawaoni “kisima cha maji”

Tena wakati mwingine wanapishana na kisima hicho,huku wakilalamika “maisha magumu,….naona kufa” kumbe yupo Mungu afunguaye macho, lakini lazima “uombe” kwake ili upate upako wa kuona kwa haraka. Hivyo, leo unaona nini?


Kuna kisima cha maji unakiona? Ikiwa hapana huoni chochote ni vyema sasa uingie katika maombi.

Na waweza kunipigia simu ili tuombe pamoja,ninaamini tukiomba,kuna kisima cha maji utakiona tu.


Kwa msaada zaidi na maombi +255 683 877 900

What’s app+255 746 446 446


Na Mch. G. Madumla


UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page