KUANZISHA BIASHARA NA KUIENDELEZA. ~ 01.
- Mch. Gasper Madumla
- Oct 23, 2018
- 4 min read
Updated: Sep 29, 2022

Kwa kuwa wengi wametia mikono kuandika mambo ya biashara,nami leo ninaweka mkono wangu katika nyanja ya uchumi na biashara. Utofauti mkubwa kwa wale wanaoandika mambo ya biashara na mimi ninaekuandikia leo ni kwamba “ Wao huandika kikawaida,bali ninakuandikia kiroho,ingawa mengine ni kawaida kabisa“.Si vibaya ukajifunza mambo muhimu katika eneo la kibiashara.
Tatizo kubwa la kanisa la leo ni kwamba,kanisa limejisahau kufundisha masomo ya kiuchumi,wakidhani si mambo muhimu kiroho. Na bahati mbaya mchungaji utakuta akisisitiza watu wake walete sadaka,sasa wataletaje sadaka nzuri ikiwa hawajafundishwa njia sahihi za kupata pesa?? Ukitafakari hili vizuri utagundua,kanisa linalo wajibu mkubwa kuwafundisha watu wake juu ya kukua kiuchumi ili pesa/ mali ya kutosha ipelekwe kanisani.
• Namna gani utaanzisha biashara?
01. Mshirikishe Mungu,omba kwa Bwana. ( Wakolosai 3:17)
Awali ya yote huna budi kuomba kwa Mungu ili akusaidie. Neno linakutaka katika jambo lolote uanze na Bwana. Kabla ya kutafuta chochote,mtafute kwanza Mungu ukimuhusisha katika kile unachoanza kupanga. Kumbuka ; ukianza na Mungu katika jina la Yesu Kristo basi ujue huwezi kufeli kwa namna yoyote ile.
02. Tafuta wazo la biashara.
Jiulize unataka kufanya biashara gani? Na kwa nini unataka kufanya biashara hiyo? Je utakuwa na muda wa kuifanya? Umeiona wapi hiyo biashara, kwenye tv,kwa rafiki au wapi? Maswali hayo ni muhimu wakati wa kutafuta wazo la biashara.
Katika kutafuta wazo ni la zima utafiti kwa kina ni biashara gani unataka kufanya? Unaweza kutumia njia mbili za utafiti ;
a) Kutafuta mwenyewe kwa watu waliofanikiwa na waliofeli pia. – usiende kutafuta wazo la biashara kwa waliofaulu tu,bali nenda pia na kwa walioshindwa kwa sababu ujue kwa waliofaulu kwa vipi wamefaulu,na kwa walioshindwa kwa nini wameshindwa?
b) Tumia wataalamu kwa kuwalipa,wakuletee wazo lenye utafiti wa kina – Watu wengi wamekosa wazo zuri la biashara kwa sababu wamekosa kuwatumia wataalamu wa mambo ya utafiti kibiashara. Wapo watu ambao kazi yao ni kutafiti biashara kuanzia kwenye ngazi ya wazo hadi kwenye ngazi ya masoko.
03. Chunguza kujua uhakika wa mtaji na gharama zake.
Biblia inasema ; “Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?” Luka 14:28 .
Ni muhimu kuchunguza mtaji wako na kile unachotaka kufanya kabla ya kufanya kwenyewe. Sasa shida iko hivi, wewe badala ya kuchunguza kwanza, eti unaanza kwanza biashara, alafu baadae unajikuta mtaji hautoshi. Na hapo akili ndipo zinakujia,tena baada ya kuwaza na kuwazua,alafu anaenda kuchukua mkopo ( usiokuwa na malengo) ili ujazie kwenye mtaji wako!!! Sasa unajikuta badala ya kusonga mbele,unarudi nyuma. Chukua hatua sasa!
04. Eneo / location.
Mambo muhimu katika “eneo la biashara “
Wakfu wa ardhi – Ardhi ikombolewe.
Pima uhitaji wa bidhaa / huduma ( How demands are there)
Pima washindani wako (check the degree of competitions)
05. Thubutu sasa. ( Yoshua 1:7a)
Usiogope bali thubutu kuanza kwa ujasiri. Ni lazima ujifunze kuwa “risk taker” yaani uwe mtu wa kuthubutu. Kumbuka “kuthubutu” hakuna maana ya kupatia muda wote,bali kuna kuanguka au kupoteza muda mwingine. Na Kumbuka tena,kadri unavyoanguka na kuinuka ndipo unavyojifunza zaidi,kwa maana hakuna kujifunza vizuri kama uanguki na ili yatokee haya,unahitajika uthubutu sasa.
06. Anza biashara kwa udogo kwanza.
Unapoanza biashara usiipanue mara moja bali subiri hata miaka mitatu ili uizoee vizuri na ujue vyema kuitawala. Hii hoja ni muhimu sana kwa maana ukikimbilia kuipanua biashara yako mapema basi ujue itakuahinda tu,na utaanguka. Waulize wale waliofungua biashara leo kisha kesho kutwa kaenda kuifungua tena huku,na huko,watakuambia matokeo yake.
07. Tafuta jina zuri la biashara yako.
Leo watu wengine wanaziita biashara zao majina magumu ya kinyumbani nyumbani ( ya kilugha) kiasi kwamba wengine hawajui maana na wamekuwa wakisumbuka kujua maana yake. Ni vyema utafute jina jepesi na zuri kukumbukwa,jina zuri litakumbukwa rahisi,na kunaswa na watu wengi. Kumbuka; majina yana nguvu sana katika biashara.
08. Ubora / excellence.
Biashara yako lazima iwe na ubora ili iweze kuwanasa wateja wengi. Ninaposema ubora nina maana umaridadi wa biashara yako, yaani ile hali ya usafi,uzuri,mpangilio wa kuvutia n.k Sasa, Jamani kuna watu hawana ubora kabisa kwenye biashara zao,na kwa sababu hiyo wamejikuta wakipoteza wateja alafu bahati mbaya wajui wamekosea wapi wakidhani wamelogwa!!! Ndugu ubora ni kivutio cha biashara yako.
09. Uwajibikaji na nidhamu.
Umeshawahi kwenda ofisini alafu ukakuta wafanyakazi wapo kwenye kompyuta wanaangalia tamthilia kisha mapokezi hakuna hata mtu. Alafu akija huyo mdada wala hana time / muda na wewe,ndio kwanza yupo bize na kompyuta yake anacheza game la karata,kwa hiyo anaongea nawe kimkato kato huku anacheza game la karata ili uwahi kuondoka maana anaona unampotezea muda wake wa kucheza,huku yupo ofisini,lakini pia huku wewe ni mteja wao. !!!! Ofisi ya namna hii imekosa kitu kinchoitwa “ uwajibikaji pamoja na nidhamu“
10. Uaminifu.
Wewe mwenye biashara lazima uwe kielelezo cha uaminifu kwa wengine. Uwe mwaminifu wa kujipangia mshahara na sio kujichukulia tu. Kama utaweza kumpangia mfanyakazi wako mshahara basi na wewe mwenyewe ujipangie mshahara. Na nje ya mshahara ni marufuku kuchukua pesa yoyote,hiyo ndio nidhamu ya kwanza. La umepungukiwa andika barua rasmi ya mkopo kisha ukichukua ni lazima ulipe huo mkopo tena kwa wakati. Hakikisha umeweka nidhamu ya pesa,kiasi kwamba upunguze matumizi yako ya kila siku. Waweza kujipangia nguo chache tu za kuvaa na kuzirudia rudia hizo hizo pasipo kujirundikia nguo. N.k
11. Pumzika.
Kumbuka “ usipoupumzisha mwili wako,mwili wako utakupumzisha wewe” think about that! Ndio….Na ndio maana Kupumzika nayo ni dawa tena ni akili. Neno linatuambia Mungu alifanya kazi siku sita na siku ya saba akapumzika. Unafikiri Mungu alichoka? Lah! Mungu hakuchoka. Sasa jiulize kwa nini alipumzika? Au kwa nini imeandikwa hivyo? Jibu ni hili: Bwana Mungu anajaribu kutufundisha kwamba kupumzika nayo ni ratiba ya mwanadamu. Hivyo,jitengee muda fulani wa kupumzika….
ITAENDELEA…
Ikiwa fundisho hili limekubariki na umejifunza kitu,basi nifahamishe kupitia namba zangu + 255 683 877 900
WhatsApp ni +255 746 446 446
Mch. G.Madumla.
UBARIKIWE.
Kommentarer