SIRI YA KUFANIKIWA NA KUSTAWI SANA.
- Mch. Gasper Madumla
- Dec 20, 2018
- 4 min read
Updated: Sep 29, 2022

Kila aliyefanikiwa anajua namna gani alifanikiwa. Na ikiwa kama utabahatika kumuuliza aliyefanikiwa,atakwambia “siri” ya mafanikio yake ijapokuwa wengine hawatakwambia kwa sababu za ubinafsi wakiona kwamba usije na wewe ukafanikiwa na kuwapita. Lakini wengi watakwambia. Na jambo la ajabu utashangaa wengi wamefanikiwa kwa njia za uovu fulani bali wachache wametumia njia za haki katika mafanikio yao. Katika kila mafanikio kuna “ siri” na ndio maana hata kama unataka kuwa mtumishi mkubwa ujue kuna mambo lazima uyafanye na kuna mambo lazima uyaache. Hayo mambo yote huitwa “siri“
Ukifanikiwa kumwuuliza siri ya kufanikiwa mtu mbaye ni mpiganaji wa ulingoni ( boxer) kama akina Matumla,au tyson watakwambia kwamba kuna mambo walikatazwa kuyafanya kabisa na kuna mambo waliambiwa wayafanye. Mfano ukirudi kwa mwimbaji mzuri,utagundua amekatazwa kunywa vimiminika vya baridi kulinda sauti zao bali wajitoe kwenye zoezi kila siku. Hivyo umegundua katika hatua yoyote ya kufanikiwa kuna taratibu zake za kufuatwa hizi huitwa“ siri“
Biblia haikunyamaza kwa kueleza namna yako ya kufanikiwa. Na leo tunajifunza jambo la ajabu sana kupata kuelezwa kwenye biblia. Hili ni “siri ya kufanikiwa na kustawi sana” katika yoyote uyafanyayo. Biblia imeweka taratibu muhimu za kufanikiwa tofauti kabisa na zile za dunia hii. Kwa maana biblia inasema;
“ Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.“ Yoshua 1:8
Bila shaka watu wengi hupita tu,bila kuutafakari mstari / andiko hili kwenye biblia. Hapo mwanzo watu wa Mungu walipewa torati kama kiongozi wao kwa kuwaongoza na kuwapa taratibu za kimaisha ya uchaji wa Mungu. Haikuwa rahisi,lakini ilibidi waishike torati kwa gharama yoyote ile. Hata hivyo walishindwa kuiishi torati, na Bwana Mungu akaleta mpango wa agano jipya ( Yeremia 31:31-34).
Ndani ya agano jipya leo,tuna mfano wa torati ambao ni “Neno la Mungu” . Neno,ndio sheria,taratibu na ustaarabu wote wa Mungu.
Ukirejea katika Yoshua 1:8,Neno la Mungu linakufunulia siri kubwa ya kufanikiwa na kustawi sana,katika kulihifadhi Neno la Mungu ( torati),na kulitafakari tena usiku na mchana na kutenda yote yaliyoandikwa humo. Katika andiko hilo,tunayaona baadhi ya mambo muhimu,nayo ni;
Kuhifadhi neno la Mungu
Kulitafakari mchana na usiku
Kuliishi / kulitendea kazi.
Ukifanikiwa kuzifanya hatua hizo tatu,ujue umefanikiwa tayari katika kila ulifanyalo. Yaani iwe ni biashara au utumishi,hizo ni siri za kupabda kwako. Ni ajabu kama nini kuyajua mambo haya ambayo wenye hekima ya dunia hii wamefichwa,bali yamefunuliwa kwako kama siri,ili upate kufanikiwa na kustawi sana. Kumbuka kazi yote hii,hufanywa na Roho mtakatifu pamoja nawe.
01. Kulihifadhi neno la Kristo.
Nilipokuwa sijaokoka nilikuwa ninakamata “vesi za nyimbo za bongo fleva” ( mistari mingi ya nyimbo za bongo fleva). Ninaweza nikapiga nyimbo mbili tatu hivi bila kuchoka tena mwanzo mwisho. Maandishi / mistari ya nyimbo ilikuwa mirefu,hivyo wakati mwingine ninaimba pamoja na mwimbaji mwenye huo wimbo na mambo yanakuwa sawa kabisa!!!. ( Hakika ulikuwa ni ujinga fulani,kwa maana hakuna faida ya kushika nyimbo za dunia hii na kuziimba kana kwamba wewe ndio mtunzi!!! Ni upuuzi!!!!)
Nilipookoka nilishangaa kwa kuwaona walokole wenzangu wakishindwa kuwa na maandiko japo maandiko mawili tu!!! Hii inatisha sana. Na cha ajabu hali hii ipo hata sasa,yaani hata kwako inawezekana unayo kwamba “huna hata andiko moja ulilolihifdhi ndani yako“. Ebu fikiri mtu akujie sasa hivi hapo ulipo kisha akwambie umtajie ndiko lilote kwenye biblia kisha uliseme jinsi lilivyo! Utaweza sasa????
Bila shaka kama ukiweza wewe basi ujue si wengi wakristo wa leo wanaweza kuyatamka maandiko!!. Halafu kisibgizio cha wapendwa wengi walioshindwa ni “ unajua mimi sasa hivi nimekuwa mtu mzima….” Au “ tatizo nipo bize sana hivyo siwezi kushika” Au “ Kulili sio mzuri bhana,ndio maana mimi sina neno lolote nililolikariri./)
Huko ni kushindwa tu! Kwa sababu haiwezekani jamani ushindwe kuhifadhi neno la Mungu japo mstari mmoja tu. Ikiwa umefikia wakati kwamba hukumbuki maandiko kwa kuyasema jinsi yalivyo,yaani mstari mzima wa biblia. Basi hakika itakuwa ni shida hata kukua kiroho tena utaangamizwa. Biblia inakutaka uhifadhi Neno kuanzia leo,fanya mazoezi sasa.
02. Kutafakari.
Kitendo cha kulimengenya Neno ili kuangalia kile unachojifunza, unacho-ongozwa,unachoelekezwa au kuadabishwa huitwa “ kutafakari Neno “. Kutafakari kunahitaji muda wa zaida sana sana peke yako,au lah! Unaweza kufanya kwenye kundi. Asilimia kubwa ya watumishi wa Mungu tulionao leo hawatafakari neno bali wanatoa kile tu wanachoona chepesi kukitoa basi n huishia hapo. ( Kipengele hiki muhimu, soma kwa urefu kwenye somo linaloitwa “ Kuliishi neno”,tafuta hapo chini kwa kundika kwenye kitafutio)
Na ndio maana hawawezi kufanikiwa wala kustawi sana kwenye huduma zao.
Hata kwako,ikiwa kama utakosa muda wa kutafakari neno,ujue huwezi kusogea mbele,bali utabaki eneo moja hilo hilo siku zote. Kwani hujawahi kuona mchungaji akihubiri neno hilo hilo kila siku? Basi ujue mtu wa namna hiyo hana muda wa kutafakari neno.
Ndani ya tafakari kuna mengi utakayoyapata,kwa maana hata ufunuo wa nini na nini cha kufanya hupatikana ndani ya tafakari. Hii ni suri ya ajabu ya kufanikiwa na kustawi sana katika nyanja yoyote ile. Jaribu leo uone!!!
03.Kuliishi neno.
Ikiwa neno ndio dira ya maisha yako ( Zab.119:105). Basi huna budi kuliishi sawa sawa na yote yalioandikwa humo. Ninafahamu kwamba si rahisi kuliishi neno au kufanya yote yalioandikwa humo,lakini kwa msaada wa Roho mtakatifu ni rahisi sana.
Biblia haikuficha njia ya kufanikiwa na kustawi sana katika kila ulifanyalo.
Kwa maana mambo matatu endapo utayafanya kikamilifu,basi ujue kufanikiwa na kustawi sana kila mahali ni sehemu yako. Kwa maana hakuna mtu yeyote duniani aliyeyafanya hayo na asifanikiwe,hakuna!! Biblia imesema kufanikiwa ni lazima tu. Jaribu leo kufanyia mazoezi hayo matatu,na utaona matokeo yake.
Kwa msaada zaidi +255 683 877 900
WhatsApp namba .+255 746 446 446
Mch. G.Madumla.
UBARIKIWE.
Comentarios