NAMNA YA KUANZISHA BIASHARA NA KUIENDELEZA. ~ 02. Tamati.
- Mch. Gasper Madumla
- Oct 25, 2018
- 3 min read
Updated: Sep 29, 2022

Kumbuka,ikiwa wewe ni mwajiliwa basi ujue kuna siku hautakuwa hapo ofisini kwa maana sio ofisi yako. Swali la kujiuliza,kazi ikiisha hapo utakuwa wapi?. Au mwenye mwajiri akisema leo “sikutaki tena kwenye ofisi zangu,nasitisha mkataba na wewe,kwa heri…” wewe utaenda wapi? Utakuwa mgeni wa nani? Usijibu kwa haraka haraka eti unasema utaenda kutafuta kazi ofisi nyingine!!! We unajua gharama ya kutafuta kazi leo?
Hapo ukumbuke,unaajiliwa ili ujifunze tu nidhamu ya maisha na ndio maana kuna siku utaondolewa kazini. Hivyo kumbe una kila sababu ya kujifunza namna ya kuwa na kbiashara kako mpendwa,ili kusudi mwenye ofisi akisema “basi” ujue wapi pa kukimbilia. Unaelewa lakini?? Haya bhana,mimi nasema tu na wewe,ukielewa hiki nikisemacho,utatoka kimaisha! Leo tujifunze hiki;
Namna ya kupata mtaji.
Shida kubwa kwa watu ni mtaji. Tunashuhudia watu wengi wakishindwa kuanzisha biashara kwa sababu ya kukosa mtaji. Lakini ebu tuangalie njia muhimu za kupata mtaji,nazo ni kama ifuatavyo;
01. “Kudunduliza” kidogo kidogo.
Ninaposema neno“Kudunduliza ” bila shaka wale wenye hasira ya kutoka kimaisha watakuwa wananielewa. Hii ni njia ya kujiwekea kiasi fulani,si kingi lakini kidogo kidogo. Waswahili wanasema “ ndo ndo si chululu” ebu chukua mfano wa bomba la maji lililokuwa limefungwa lakini kwa sehemu kuna matone tone ya maji yakichuluzika kidogo kidogo na kisha ukaweka ndoo tupu ambapo matone yakidondokea kwenye ndoo “ndoo…ndoo…ndoo ….” hatimaye ukija baadae sana,utakuta kandoo kamejaa maji ijapokuwa ilikuwa imechukua muda kujaa.
Na ndivyo ilivyo hatua hii ya kupata mtaji ya “kudunduliza” au kujiwekea akiba kwa kidogo kidogo. Fikiria una Tshs 2,000/= kisha ukatoa tshs 500/= na kuiweka akiba kwenye kopo lako,ukafanya hivyo mara kumi,ujue utakuwa na tshs 10,000/= tayari. Sasa 10,000/= si haba!
02. Kujiwekea akiba stahiki.
Njia hii inafanana na ile ya Kudunduliza, utofauti wake ni kwamba njia hii ni ya kitaalamu zaidi na ya kwanza. Njia hii inamuhusisha hasa yule anayefanya kazi fulni. Hapa ndipo unaweza kujiwekea akiba kwa namna tatu,nazo ni;
Toa sehemu ya 10 ( fungu la kumi la pato lako la mshahara,ni la kanisa,maana unapaswa kulipa fungu la kumi) ya kila mshahara wako.
Hifadhi pesa ya dharula ya 10% ya kila mshahara wako. Usije ukatumia kiasi hiki.
Weka akiba ya 10% ya kila mshahara wako.
Sasa, pesa zilizobaki zitengenezee bajeti yako ya matumizi ya mwezi mzima. Hakikisha bajeti yako inakuwa ndogo. Pia hakikisha matumizi yako yanalingana na bajeti yako. Sehemu ya akiba ya 10% ya mshahara wako inabaki kama mtaji.
03. Mkopo.
Njia hii inafahamika na wengi lakini wengi wamejikuta wamekosa nidhamu ya fedha wanapokopa au wamejikuta wakikosa malengo ya kile wanachokopa. Ikiwa umepata pesa leo,unaweza ukanunua kwanza kiwanja au shamba hata kama lipo nje ya mji,ili kusudi uweze kukopeshwa kwenye taasisi za kibenki kwa kutumia hati au documents za kiwanja / shamba.
04. Uza baadhi ya vitu vyako vya thamani.
Kuna watu ambao wanatafuta mtaji wa biashara huku wakiwa na vitu vingi vya thamani ambapo wanaweza kuvipunguza kwa kuuza na hatimaye kupata pesa kama mtaji. Ebu chukulia mtu ana simu mbili, alafu zote ni simu za bei kali,kisha hajui anaweza kuuza zotd na kununua kisimu kidogo tu kwa ajili ya mawasiliano ya kupiga na kupigiwa kisha akakusanya pesa. Au chukulia mtu ana vyombo vya kisasa ndani kama radio,Tv,Washing mashine,n.k. ambapo anaweza kupunguza na kukubali kuishi maisha ya kawaida ili apate mtaji.
05. Akiba kwenye bonus ( allowance) zako.
Kuna wakati unapokea allowance fulani fulani hivi usiyoipangilia,basi hiyo hiyo unaweza ukaigeuza kuwa mtaji wa kuanzisha biashara yako. Hasa kwa wafanyakazi ofisini,wanapewaga bonus kama motisha wa kazi wazifanyazo,basi hapo ikiwa ni wewe uione bonus / motisha kuwa ni mtaji wako.
06. Uaminifu,na kuomba msaada kwa rafiki ndugu na jamaa.
Ingawa jamii ya leo ni ngumu kumsaidia mtu hasa kwenye eneo la kufungua biashara ( watu wanapenda wakusaidie kukupa pombe,sigara na uhuni ila sio pesa ya kufungua biashara au kumsomesha mtoto) Lakini bado unayo nafasi ya kutumia uaminifu wako,kuomba kwa ndugu yako au rafiki akukopeshe pesa kidogo ya mtaji kisha utamlipa. Wako watu waliofanya hivi kwa uaminifu na walepewa na hatimaye wamekwisha rudisha.
07.Tafuta mentor / mkufunzi wako.
Ni vyema utafute mtu aliyefanikiwa kwenye biashara unayotaka kufanya na umfanye huyo mtu kuwa kama baba / mama kwako,atakaye kufundisha kwa usahihi juu ya hiyo biashara. Mtu huyo kwako ni mtaji tosha.
08. Tumia vyema kipawa chako.
Ikiwa umegundua kipawa chako ulichozaliwa basi unaweza kukitumia kama mtaji wako wa kuanzisha biashara. Mfano wewe una kipaji / kipawa cha kupamba ukumbi. Kupitia kupamba basi jikusanyie pesa itakayokuwa mtaji wa biashara yako. Sizungumzii “karama” bali nazungumzia “kipawa / kipaji” kama uwezo wa kimwili wa kuzaliwa nao.
Ikiwa fundisho hili limekubariki na umejifunza kitu,basi nifahamishe kupitia namba zangu + 255 683 877 900
WhatsApp ni +255 746 446 446
Mch. G.Madumla.
UBARIKIWE.
コメント