top of page

UONGOZI KATIKA KANISA.~01


Mch.Madumla.

Mchungaji Gasper Madumla.


Bwana Yesu asifiwe…

Fundisho hili si la watu wote bali ni la wachache tu hususani wale ambao ni viongozi mbali mbali wa makanisa,fellowship na vikundi mbali mbali vya wokovu. Dhumuni kubwa la fundisho hili ni kukupa maarifa wewe kiongozi kujua nini maana ya uongozi na jinsi ya kuenenda uwapo kanisani.

Ni fundisho lefu sana,lakini ninajaribu kukupa kwa sehemu tu ili usikose maarifa haya. Hivyo tuanze fundisho hili kwa kuangalia wito wa uongozi.

01.WITO WA UONGOZI. (A call to leadership)

Uwezo wa kanisa lolote au organasation yoyote,katika ukuaji unategemea ubora wa uongozi uliopo. Uwezo wa Kanisa letu unategemea na uongozi tuliokuwa nao. “ Uwezo mkubwa ukuaji mkubwa”. Kila kitu kina kuwa na kuanguka kutegemea uwezo wa uongozi uliopo. Kwa maana kila kitu kimejengwa katika uongozi.

~Mara nyingi tunachanganya maana halisi ya uongozi na nafasi ( leadership and position),uongozi sio nafasi kwa sababu kuna kipindi watu wanaweza kuwa na nafasi lakini hawafanyi kazi kama viongozi,lakini tunaweza kuwa na watu wasiokuwa na nafasi lakini ni wachapa kazi kama viongozi.

Tazama;kuna watu wanakuja kanisani wakitazamia wawe viongozi lakini hawana chochote cha kiuongozi. Uongozi hauna uhusiano na nafasi. Uongozi ni uongozi,nafasi ni nafasi.

~ Tena,muda mwingine tunachanganya neno uongozi na umaarufu. Tujue kwamba;uongozi sio umaarufu. Kwa maana mtu anaweza kuwa ni marufu lakini asiwe kiongozi. Tena,uongozi sio kutumia mabavu,(nguvu),kwa maana uongozi hauna uhusiano na nguvu.

Hivyo basi,katika makanisa yetu tuna hali fulani hivi ambayo si nzuri kuhusiana na suala zima la uongozi kwa maana utakuta mchungaji amezungukwa na watu wanaojiita ni viongozi lakini hawajui kitu gani cha kufanya. Viongozi katika kanisa,ni lazima wajue namna ya kuongoza wao wenyewe.

~Changamoto kubwa ya ukuaji wa kanisa iliyopo leo ni suala la uwezo wa uongozi. Ni muhimu kushughulikia suala la uongozi.Tazama; Katika kipindi cha nabii Ezekieli,Waisraeli nao walikuwa wakikumbana na tatizo la uongozi.

Tunasoma; “Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.” Ezekieli 22:30

~Mungu alitafuta mtu mmoja tu atakayesimama kwa ajili ya wengine lakini alikosa. Kwa maneno mengine ni kwamba; Israeli walikuwa na watu wengi wenye nafasi lakini sio viongozi.Kitu kinachowatisha watu wengi ni hali ya kutokukua kiroho.

Wakati unapokuwa hukui wala husogei mbele,mchungaji huogopa hali hiyo lakini hata MUNGU huishangaa hali hiyo isiyokuwa ya kawaida,kwa sababu MUNGU hapendi kukaa bila ukuaji. Ndio maana katika Kumb. 1:6 Neno linasema;

“BWANA, Mungu wetu, alituambia huko Horebu, akasema, Mlivyokaa katika mlima huu vyatosha;”  Mungu anataka watu wake waanze kusogea mbele kimaendeleo ya ukuaji na kamwe wasidumae. Hivyo,kuna kazi kubwa ya kufanya lakini lazima tujue nafasi zetu.

Muda umefika wa kutoshindana sisi kwa sisi katika nyumba ya BWANA wala huu sio muda wa kusengenyana bali ni muda wa kusonga mbele. Ukisoma katika Mathayo 16:18,biblia inasema;

“Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.” Yesu anasema “Yeye” atalijenga kanisa,sio wewe,bali ni “Yeye” kwa maneno mengi ni Yesu ndiye ajengae kanisa, wajibu wako wewe kama tofali ni kukubali kuwekwa mahali pale Yesu atakapo.

Nami sitakiwi kukataa kuwekwa eneo lolote.Kwa hiyo,Yesu anahitaji kila kiongozi awe na nguvu ya Mungu na kukubali kuwekwa mahali popote pale. Mungu anapokuambia ufanye usafi,basi fanya. Ndani ya nyumba ya Mungu sisi sote tunakuwa ni watoto pasipo kuangalia vyeo vyetu tulivyonavyo.

Sasa,ni majukumu ya viongozi wa kanisa kuanzisha ukuaji na kusimamia ukuaji. Ni jukumu letu kuwapokea wanaokuja,lakini ikiwa watu watakuja na kuondoka ni lazima tujiulize ni kwa sababu gani wameondoka. Ni jukumu letu kuwaonesha upendo na kuwaweka wote hao nyumbani mwa Mungu.

Wala siamini kwamba ukubwa wa mlango ambao watu hutumia kuingia ni sawa na ukumbwa wa mlango wa kutokea.( Kwa maana yapasa mlango wa kuingia uwe mkubwa kuliko wa kutoka) Mungu anataka kuona ukuaji.

~Katika ukuaji wa kanisa,mambo yafuatayo ni mambo muhimu;

01.Mfumo wa ki-Mungu katika ukuaji wa kanisa.

02.Mahusiano kati ya fedha na ukuaji wa kanisa

03.Namna ya kuimarisha na kuwajenga imara watu wanaokuja kanisani kwa mara ya kwanza.

04.Kutengeneza darasa la washirika.

Swali; Kiongozi anazaliwa au anatengenezwa? Je ulizaliwa  kuwa kiongozi au ulitengenezwa kuwa kiongozi?

JIBU; Viongozi hawazaliwi kuwa viongozi,bali wanatengenezwa. Kuna watu ambao wanakipawa cha kuwa viongozi lakini kuna watu wengine hawana kipawa na wapo tayari kujifunza. Tabia njema na mtazamo mzuri ni muhimu kwa yeyote anayekuwa kiongozi.

MSINGI WA UONGOZI.

~Msingi wa viongozi wote ni maono,kwa maana hakuna uongozi bila maono.“ Pasipo maono, watu huacha kujizuia;Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.” Mithali 29:18

Maono ni nini? Tafsiri nyepesi ya maono ni kile unachokiona kinachokuja,ni picha au taswira ya mambo yajayo. Kuwa kiongozi ni tofauti na mfanikiwaji. Kiongozi huwa anakuwa na malengo ya kuzidi kuendelea kwa maana hajafanikiwa bado,naye uwahitaji watu kisha na kushirikiana nao katika maono yake. Mungu ametuita kuwa viongozi na si wafanikiwao tu.

Hivyo ni lazima kuwe na commitment kwa viongozi katika maono yote. Maono ya viongozi huwa ni mema,na neno linasema ;“ Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.“Yakobo 1:17
maono yanatoka kwa Bwana na mtu yule mwenyekubeba maono huitwa mbeba maono. Akiwa ni baba huitwa baba mbeba maono,naye huwa ni baba yetu nasi tunakuwa ni watoto kwake.

Maono yanakujaje?

~Maono yanakuja kutoka katika mzigo. Mungu anaweka mzigo ndani ya mtumishi wake. Kisha Roho mtakatifu anawezesha namna ya kushughulika na huo mzigo na namna ya kumpa taswira hiyo na taswira hiyo inakuwa ni maono. Hivyo hakutakuwa na maono bila mzigo. ~Jukumu la viongozi katika kanisa ni kujua mzigo wa mchungaji wao,kama hatutaelewa mzigo wa mchungaji basi hatutauweza kuubeba.

~Jukumu la mchungaji ni kueleza mzigo wake na maono yake kwa viongozi. Hivyo,mzigo na maono ndio kanisa lenyewe,kwa sababu pale mzigo ulipo ndipo nguvu zetu zipo. Mfano mzigo wetu ni kufundisha neno la Mungu na ndio nguvu yetu ilipo. Watu wakija wakute neno la Mungu kwa sababu ndio mzigo wetu….

ITAENDELEA…

Kwa ushauri na maombezi,nipigie sasa+255 655 11 11 49. Mch.G.Madumla.

Beroya bible fellowship church(Kimara,Dar,TZ)

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page