top of page

UONGO NI SUMU YENYE KUUA.

Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi.

“Sumu ” inaweza ikawa ya kunywa,kula,kutupiwa,au sumu inaweza kuwa ile itokayo ndani ya moyo wa mtu. Mojawapo ya sumu mbaya ni ile itokayo ndani ya moyo wa mtu,hiyo ndio yenye kuleta… maangamizo makubwa na mabaya kuliko sumu ya aina yoyote. Fikiria ikiwa ndani ya mtu mwovu kukatoka jambo baya hata kufanya watu wengine kushiriki ubaya huo. Mfano angalia pale watu wanapoingia kwenye mgomo fulani,ujue mgomo huo ulianzia ndani ya mtu mmoja,kisha na kuambukiza wengine na hatimaye kundi kubwa la watu wakijikuta wanagoma,;

tena mbaya zaidi utakuta kuna watu watakaogoma bila kujua wanagoma nini,ukiwauliza kwa nini mnaandamana watakwambia “tunataka haki zetu” ukimwuliza haki zipi hizo,atakwambia “ sijui bhana!,lakini nataka haki zangu” !!! Duh!. Kuna sumu moja ambayo imeangusha wengi hasa wale waaminio,sumu hiyo inaitwa “uongo” ,lakini nataka nizungumzie hasa “kumwambia uongo Mungu kupitia watumishi wake“,eneo hili ndilo muhimu sana katika maisha yako.

Najaribu kutafakari jinsi gani watu wengi wamepoteza maisha yao kwa sababu ya kumwambia uongo Mungu. Wengine walikuwa hawajui kwamba kumdanganya mtu wa Mungu ni kujiangamiza nafsi zao. Lakini wengine wengi hali wakijua kwamba Mungu hadanganywi wala kudanganyika lakini bado wanakaza kumwambia uongo,na hatimaye hujikuta wakivuna mauti kama mshahara wao.

  1. Hali ilikuwaje kwenye kanisa la kwanza?

Kwenye kanisa la kwanza, waaminio wote walikuwa mahali pamoja na kuwa na vitu vyote shirika. Wamini walikuwa na roho moja na moyo mmoja,hapakuwa na mhitaji yeyote kwa maana waaminio waliuza mali na vitu walivyokuwa navyo na kumgawia kila mtu jinsi alivyohitaji. Siku zote walidumu ndani ya hekalu,wakimega mkate yaani ( wakishiriki neno), na kula chakula chao kwa furaha na moyo mweupe huku wakimpendeza kila mmoja, Bwana akalizidisha kanisa kila siku ( Matendo 2:44-47,4:32-35)

Kulikuwa na kijana mmoja ambaye aliitwa Yusufu ( Barnaba),huyu alikuwa na shamba lake,naye aliliuza kisha akapeleka pesa ya shamba lake kwenye utaratibu wa mitume ( miguuni pa mitume) ( Matendo 4:36-37). Hata hivyo kulikuwa na mtu mmoja alikosa uaminifu yeye na mke wake. Mtu huyu alikwenda na kumwambia uongo Mungu naye akafa yeye pamoja na mkewe.

“ Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira mkewe, aliuza mali,akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume.Petro akasema, Anania, kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja? Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote walioyasikia haya.” Matendo 5:1-5

Anania alikuwa amepiga “dili “na mke wake “wakamdanganye Mungu“. Walipokiuza kiwanja na kuziona pesa nyingi namna ile bila shaka walisema “hata,pesa zote hizi tuzipeleke kwa mitume, tutatumia akili ya kuzaliwa,ngoja tutabanana hapa hapa” kitu kimoja ambacho anania maskini hakujua ni kwamba, Roho mtakatifu alikuwepo pale pale walipokuwa wakipanga madili yao,yeye na mkewe. Yeye Anania alidhani wapo wawili walipokuwa wakipanga mikakati ya kusema uongo,bila kujua walikuwa watatu ( mzee wa siku alikuwa akiyaangalia yote waliyokuwa wakiyapanga).

Jambo hilo hilo,ndilo linakufelisha hata wewe kwa maana pale unpoketi na mwanandoa mwenzako na kuanza kusuka mipango ya udanganyifu kwamba ukienda kanisani,basi utamficha mchungaji wako,ujue katika mipango hiyo mzee wa siku yupo hapo hapo ( Yeremia 23:23)./ Mungu yupo hapo hapo akiwaangalia na uongo wenu mnaopanga juu ya mchungaji.

Petro kama mtu wa Mungu namwambia Anania kitu cha ajabu sana. Anamwambia “… Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.“. Bila shaka Anania alishtuka “ Eeeh,Mungu?Mbona sijawahi kwambia uongo jamani!!!” Hakujua kwamba, Roho mtakatifu yule yule aliyekuwa akiona yote waliyoyapanga na pesa waliyoficha pamoja na uongo wote ndiye huyo huyo Roho mtakatifu aliyepo ndani ya Petro.

Na kwa sababu hiyo, uongo waliokuwa wakimweleza Petro ni sawa na walikuwa wakimweleza Roho Matakatifu,na ni sawa na kumweleza Mungu. Mlolongo huo hawakujua!!! Kama vile wengi leo wanavyokufa kwenye maeneo mengi kwa sababu hiyo hiyo ya kupanga uongo kisha kwenda kumweleza mtu wa Mungu labda mchungaji wakidhani wanamweleza mwanadamu,kumbe wanamwambia uongo Mungu,na hatimaye hujikuta wakianguka na kufa katika mambo yao binafsi.

Wakati mwingine watu wakipokea laana badala ya baraka pale wanapopeleka fungu la matoleo kwa sababu ya kuficha kwa siri fungu,na yale mabaki ndio huenda kuyatoa kwa Mungu hawajui kuwa wanamwibia Mungu tena kusema uongo mbele za Mungu. Angalia sana hili,ni muhimu sana kwako. Hivi unajua kwamba, mambo yako ynaweza kufungwa kwa sababu ya udanganyifu wako unaoufanya mbele ya Mungu kupitia mtumishi wake? Ndio ,; mambo hufunga sana kama utathubutu kumdanganya Mungu.

  1. Ukimwambia uongo mtu wa Mungu, umemwambia Mungu.

Kuna watu mimi sijui kama wanajua kwamba ukimwambia uongo mchungaji ni sawa na kumwambia uongo Mungu. Maana unaweza ukamkuta mtu amepanga “kumpiga chenga mchungaji” / kumdanganya. Tena hali akijua yote asemayo,kwamba ni uongo mtupu,lakini ndio utakuta kingangania kusema na kusema uongo. Halafu Mungu alivyo wa ajabu,mchungaji utakuta anajulishwa kuwa yote uyasemayo ni uongo mtupu!!! Hakuna hata kweli. Kwa hiyo wewe unajitahidi kumficha,lakini mwenzako anajua kila kitu,tena anajua hata kule unakoelekea. Sasa huku ndiko kufa kwenyewe ninakokuzungumzia!!!! Kwa nini usiseme kweli kwa mtu wa Mungu ili usiangamizwe na sumu hii ya uongo??? Mimi ninakushauri sema kweli siku zote ili uwe mbali dhidi ya mauti itokanayo na uongo – Waefeso 4:25

Ikiwa kama umejifunza kitu nifahamishe,nataka kusikia kutoka kwako. Huduma ya maombi ipo pia piga kwa namba hizi hizi +255 683 877 900

WhatsApp namba ni .+255 746 446 446

Mch.G.Madumla.

UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page